Mtanzania ateuliwa nafasi nyeti Umoja wa Mataifa

0
756

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

MTANZANIA, Elizabeth Maruma Mrema, ameteuliwa kuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Sekretarieti inayosimamia Mkataba wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa tofauti za kibiolojia (CBD) yenye makao yake makuu Monteal, Canada kuanzia Desemba Mosi, mwaka huu.

Uteuzi huo umefanywa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, baada ya kujiuzulu kwa Cristiana Pasca Palmer, raia wa Romania kutokana na sababu za kiafya.

Taarifa iliyotolewa jana na kuwekwa kwenye wavuti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP), uteuzi huo unatajwa kuwa unaongeza matumaini katika uhifadhi wa masuala ya bayonuai ya kibaiolojia, matumizi endelevu ya baiolojia hizo, na ugawaji wa faida zitokanazo na rasilimali za kijenitiki kwa kuzingatia usawa na haki.

Kabla ya kuteuliwa kwa Mrema alikuwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Makao makuu ya UNEP jijini Nairobi, Kenya ambapo amefanya kazi kwa zaidi ya miongo miwili.

Majukumu yake katika Idara ya Sheria ya UNEP ni pamoja na uratibu wa ujenzi wa uwezo, maendeleo, utekelezaji na pia kufuatilia utekelezaji wa sheria za mazingira na mikutano ya kimataifa ya mazingira. Pia aliongoza masuala yanayohusiana na utawala wa kimataifa wa mazingira.

Mrema ni Mwanasheria kitaaluma na Mwanadiplomasia akiwa na Shahada ya Sheria (LLB) (Hons) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam, Shahada ya Uzamili (LLM) kutoka Chuo Kikuu cha Dalhousie, Canada na Stashahada ya Juu katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa na diplomasia (Summa Cum Laude) kutoka Kituo cha Mahusiano ya Kigeni na Diplomasia jijini Dar es Salaam.

Pamoja na hili Mrema amechapisha nakala kadhaa zinazohusiana na sheria za kimataifa za mazingira, ufuatiliaji na utekelezaji wa mikataba na maendeleo ikiwemo makubaliano kadhaa ya mazungumzo kuhusu hali mazingira ya kimataifa pamoja na miongozo inayotumika sasa na UNEP katika mipango yake ya kujengeana uwezo.

Kabla ya kujiunga na Kitengo cha Sheria cha UNEP mnamo Juni 2014, alikuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mazingira, anayesimamia uratibu, shughuli na utoaji wa programu kuanzia mwaka 2012 na kwa mwaka mmoja, pia aliwahi kuwa Kaimu Mkurugenzi  wa Idara hiyo.

Mnamo mwaka 2004 alipewa tuzo ya Meneja wa UNEP bora zaidi wa mwaka kuwahi kutokea, aliyotambulika kama Tuzo ya Wafanyikazi ya UNEP Baobab kwa utendaji bora na kujitolea kufikia malengo ya UNEP.

Mnamo mwaka wa 2009 aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa UNEP/ Sekretarieti ya Mkataba juu ya Uhifadhi wa wanyamapori wanaohama (CMS)

Kabla ya kujiunga na UNEP, Mrema alifanya kazi na Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Tanzania na hadi anaondoka alikuwa  Mshauri Mwandamizi wa Sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here