26 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mtangazaji Gardner alivyoukwaa kiaina msala wa T.I

Christopher Msekena na Beatrice Kaiza

UPENDO wa baba kwa bintiye ni mkubwa kiasi kwamba hauwezi kupimwa kwa mzani wa kawaida, wale wanaume waliojaaliwa kupata watoto wakike watanielewa vizuri hapa.

Unaweza kuliona hilo kwa uzuri zaidi ukitazama mastaa wa kiume wanavyoishi na watoto wao wa kike, utabaini wamekuwa wakiwaonyesha upendo, kuwajali na muda mwingine kuingia katika maisha binafsi ya watoto wao.

Mapema wiki hii mtangazaji mwenye heshima Bongo, Captain Gardiner  G Habash, aligonga vichwa vya habari za burudani kupitia mahojiano aliyofanya na Zamaradi Mketema kuhusu mambo mbalimbali yakiwamo maisha binafsi ya mtoto wake pekee, Malkia Karen.

Kama unavyojua, Karen ni miongoni mwa wasanii wanaofanya poa kwenye Bongo Fleva na Gardner kama baba amebeba jukumu la kusimamia nyimbo kadhaa za  binti yake zinafanya vizuri.

Hivyo amekuwa akizunguka katika vyombo mbalimbali vya habari na mwanawe kufanyia promo video mpya, Tabu ambayo inafanya vizuri na katika mahojiano hayo yenye urefu wa saa 1 na dakika 15, Gardner alizua gumzo.

Mtangazaji huyo mwenye ushawishi hakuwa na noma kabisa alipoulizwa anataka kuona binti yake, Karen yupo kwenye uhusiano na mtu wa namna gani na yeye akasema: “ Mimi ningetamani awe na mtu mzima mwenye umri kama wangu, sugar daddy ili amtunze sababu watu wenye umri kama wake hawawezi kumuelewa, wala hawawezi kumsaidia kwa chochote.

“Mtu mwenye umri kama wake labla amemzidi miaka miwili mitatu minne ana nini, yeye mwenyewe anatafuta maisha harafu unapewa mzigo kama huu kuna kijana gani anaweza kubeba, utakuta yeye mwenyewe amepanga nyumba, anatafuta kodi, mshahara laki tano au milioni 1 hapo hapo umgharamie Karen ni ngumu kusema kweli.”

Kauli hiyo ambayo bila shaka Gardiner aliitoa kwa upendo akitaka kuwa binti yake asipate shida kwenye mapenzi hivyo mtu mzima (sugar daddy) mwenye umri kama wake atakava vizuri nafasi yake kimatunzo.

Ila mtaani hali imekuwa tofauti, watu wamegawanyika makundi mawili yanayokinzana. Wapo wanaomponda Gardner na wapo wanaompongeza kwa kuwa muwazi na kumuwazia mema binti yake.

Miongoni mwa watu maarufu waliomponda Gardner ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye alisema kwa ukubwa wa mtangazaji huyo hakupaswa kusema hivyo kwani kauli hiyo inaonyesha ni namna gani watoto wakike wanapitia changamoto kwenye jamii.

“Kama mtu mwenye uzoefu kama ya Gardner anaweza kuzungumza upupu wa kiwango hiki kuhusu binti yake unaweza kuwaza tu ni kwa namna gani watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto kubwa katika nchi yetu,” anasema Mdee.

UNAUKUMBUKA MSALA WA T.I?

Novemba mwaka jana, rapa nyota nchini Marekani, T.I alitikisa ulimwengu baada ya kufanya mahojiano na watangzaji wa podcast ya Ladies Like Us na kuzungumza mazito kuhusu binti yake Deyjah Harris mwenye umri wa miaka 18.

T.I aliulizwa na watangazaji hao kuwa ni  zawadi gani anaweza kuitoa kwa binti yake simu ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake na ndipo rapa huyo akajibu: “Nafikiri kwenye siku yake ya kumbukumbu ya kuzaliwa nitawambia watu kuwa binti yangu hajachezewa. Siyo tu huwa nakaa naye na kuzungumza kuhusu mapenzi, bali kila mwaka huwa nampeleka kwa daktari wa wanawake (Gynecologist) kwa lengo la kukagua bikra yake,”.

Rapa huyo aliendelea kufafanua kauli hiyo tata kuwa huwa anafanya hivyo kwa siri bila mtoto wake kujua lengo likiwa ni kutokumuathiri kisaikolojia.

 “Kwa mara ya kwanza daktari alikuwa ananishangaa sana nilivyokuwa naomba majibu ya mtoto wangu, akaanza kuniambia sijui bikra inaweza kutoka kwa binti kupanda baiskeli, farasi na aina fulani ya michezo. Mimi nikamwambia mwanangu siyo mwanamichezo wala hajawahi kupanda farasi wala baiskeli, hivyo nikiona hali yake imebadilika lazima niulize, nashukuru mpaka sasa ni bikra,” anasema T.I.

Huo ulikuwa msala mkubwa kwa T.I kwani taasisi zinazoshughulikia haki za wanawake zilimjia juu mpaka huku watangazaji wa podcast hiyo  Nazanin na Nadia kuomba radhi na kukiondoa kipindi hicho mtandaoni.

Hiyo yote ilitokana na mitazamo tofauti waliyonayo watu kwenye jamii juu ya mapenzi ya baba kwa mtoto wa kike hasa anapotengeneza mazingira ya binti yake asiharibike.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles