VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA DODOMA
UMBALI wa kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam kwa njia ya ndege ni wastani wa maili 246 ambayo ni sawa na kilometa 397, ikiwa utatumia usafiri wa barabara ni wastani wa umbali wa kilometa 584 ukisafiri kwa gari kwa kasi ya wastani wa kilometa 112 kwa saa (maili 70/h) utatumia takriban saa tano kufika.
Ikiwa dereva ataendesha gari kwa wastani wa mwendo kasi 80 kwa saa atatumia takriban saa saba kufika, tofauti ya umbali kati ya usafiri wa anga na barabara kwa mikoa hii miwili ni wastani wa kilometa 187, hii ni kwa mujibu wa mtandao wa distancecalculator.net.
Ni safari waliyokuwa wakitarajia kuianza wagonjwa 10 wenye matatizo ya moyo waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo Dodoma kuelekea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.
JKCI ndiyo taasisi pekee ya umma nchini inayotoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa njia ya upasuaji mkubwa (kufungua kifua) na upasuaji mdogo (tundu dogo) kwa kutumia mtambo wa kisasa wa Cath Lab.
Kwa kutumia mtambo huo mabingwa wa moyo wana uwezo wa kuchunguza na kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba kwa kutumia njia ya upasuaji mdogo kupitia tundu dogo.
Njia hiyo ni ya kibingwa zaidi na mgonjwa huweza kuruhusiwa mapema kuliko ile ya upasuaji mkubwa (kufungua kifua), ambapo hulazimika kukaa wodini kwa muda mrefu madaktari wakifuatilia hali yake.
Ili kuongeza nguvu ya uchunguzi na matibabu dhidi ya magonjwa hayo, serikali imechukua hatua ya kufunga mtambo wa aina hiyo BMH, hatua hiyo inafanya ongezeko la mtambo wa pili kwa hospitali ya umma.
Kwa upande wa hospitali binafsi ni Agakhan pekee iliyopo Dar es Salaam ambayo imefanikiwa kufunga mtambo wa aina hiyo, hivyo sasa kuna jumla ya mitambo mitatu nchini inayotoa huduma hiyo.
“Hatua ya Serikali kufunga mtambo huu hapa BMH imekuwa neema kwetu, nimefurahi huduma hii kusogezwa hapa watu wa mikoani tunapata shida.
“Leo hii ungekuta wote tungelazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata huduma, ingekuwa kazi kubwa, tungerundikana kule, sasa tunaipata hapa ni jambo la kushukuru.
“Nimebahatika kuwa mgonjwa wa kwanza kufanyiwa upasuaji, nimefurahi mno, kwangu hii naona ni neema kwa sababu naamini Mwenyezi Mungu anakwenda kunifungua,”anasema Lilian Kinyemi katika mahojiano maalumu na MTANZANIA.
Lilian amefika hapa Dodoma akitokea Mkoani Simiyu Wilayani Maswa ambako alipatiwa rufaa akapatiwe matibabu ya kibingwa zaidi.
Tatizo lake
Anasema akiwa mkoani Simiyu ambako ndiko anakofanya kazi katika ofisi moja ya Serikali, Novemba 5, mwaka jana alianza kuugua.
“Nikaenda hospitali ya wilaya, wakanichunguza, wakanipatia dawa kutibu tatizo walilokuwa wamebaini, wakanitaka nipate pia muda wa kupumzika,”anasema.
Anasema hata hivyo wiki mbili baada ya kuanza matibabu hayo hali yake iliendelea kubadilika, ikawa mbaya hivyo akalazimika kurudi tena hospitalini hapo.
“Wakaniambia ni vema nichunguzwe afya ya moyo wangu lakini pale walidai hawana kipimo cha Echo ambacho kinatumika kuchunguza, wakataka kunipatia rufaa kwenda Hospitali ya Bugando, niliwaomba wanihamishie huku BMH, wakanikubalia.
“Desemba 9, mwaka jana nikafika hapa BMH na kuanza huduma kwa Dk. Meda, aliniandikia vipimo lakini kwa kuwa nilifika nimechelewa na ilikuwa ijumaa, alinitaka nirudi Jumatatu kwani vipimo vyote vitakuwa vimetoka.
“Nikarudi nyumbani nilipofikia, jumapili hali yangu ilibadilika ikawa mbaya mno, kifua kilikuwa kinabana, sikuweza kuhema vizuri, nikarudishwa hapa hospitalini.
“Nikatibiwa na kupata nafuu, ikabidi nilazwe ili wafuatilie kwa ukaribu hali yangu, ilipotengemaa nikapewa ruhusa kurejea nyumbani, nilipofikia,” anasema.
Lilian anasema aliendelea kuhudhuria kliniki, katika kipindi hicho madaktari walibaini mishipa yake ya damu kwenye moyo ilikuwa imeziba na haipitishi damu inavyopaswa.
“Kila walipofanya uchunguzi waliona mishipa ilikuwa inafanya kazi ‘abnormal’, nikaendelea kutumia dawa nilizoandikiwa, walipoona maendeleo yangu ni mazuri, Desemba 23, mwaka jana nikaruhusiwa kurejea nyumbani Maswa,”anasema.
Anasema siku mbili zilizofuata hali yake ilibadilika tena na kuwa mbaya kiasi kwamba akawa anapoteza fahamu kila wakati.
“Nilikuwa nazimia, nikalazwa hospitalini, wakaniwekea mashine ya hewa ya oksijeni ili niweze kupumua, Januari 18, mwaka huu ilibidi nirudishwe tena huku BMH,” anasimulia.
Anasema tangu siku hiyo hajarejea nyumbani akipatiwa huduma hospitalini hapo na Februari 11, mwaka huu akapata bahati ya kuzibuliwa mishipa yake kwa mtambo huo wa kisasa.
“Kwa kweli maumivu yalikuwa makali mno, ilifika mahali nikawa siwezi kulala upande wa ubavu wa kulia wala kushoto, nililazimika kila siku kulala chali.
“Maumivu yale yalianza taratibu mithili ya kitu kama shilingi imetumbukia kwenye maji, yanapoanza kunakuwa kama kuna mishale inachoma choma kwa kusambaa, awali nilihisi ni kichomi.
“Yalikuwa yanakuja na kutulia, kuna wakati yalikuja ghafla kiasi kwamba hata kama nilikuwa natembea barabarani nililazimika kukaa chini, pembeni kwa muda…ilifika wakati sikuwa naweza kwenda popote peke yangu, lazima niambatane na mtu,”anasema.
Nuru mpya
Hatimaye saa ya Lilian kufanyiwa upasuaji huo wa kihistoria ikafika, yapata saa 4:20 muuguzi alimfuata tulipokuwa tumeketi kwa mahojiano na kuingia naye ndani ya chumba cha Cath Lab.
MTANZANIA lilipata nafasi ya pekee kuingia pamoja naye ndani ya chumba hicho, lilishuhudia utayari na ari waliyokuwa nayo jopo la wataalamu bingwa wa upasuaji moyo wa JKCI na wenzao wa BMH kumfanyia upasuaji huo.
Ndani ya chumba hicho, jopo la mabingwa sita linaongozwa na Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo wa JKCI, Peter Kisenge.
Baada ya sala kwa Mwenyezi Mungu kazi inaanza mara moja yapata saa 4:30 hivi, ushirikiano ni wa kiwango cha juu ndani ya chumba hiki, Lilian amechomwa sindano ya kuzuia maumivu eneo ambalo madaktari wanalitumia kufanya upasuaji huo.
Wametoboa tundu dogo kwenye paja lake la kulia, wanaingiza kifaa maalumu na kuanza kuuchunguza moyo wake kupitia ‘screen’ maalumu zilizopo mbele ya mabingwa hao.
Wakati yote yakiendelea Lilian anashuhudia kila kinachofanyika, hajachomwa nusu kaputi, madaktari wanazungumza naye wakimuuliza mambo mawili, matatu anawajibu ipasavyo.
Jopo jingine la mabingwa lipo katika chumba maalumu (control room) ambako kuna mitambo wanayotumia kuwasiliana na wenzao waliopo ndani ya chumba cha Cath Lab, wanao uwezo wa kuona kila kinachoendelea kupitia kioo kikubwa kilichopo mbele yao.
Baada ya nusu saa madaktari wakipiga makofi wakishangilia, “Mwenyezi Mungu ni mwema, hatimaye tumefanikiwa…mama kila kitu kimekwenda sawa sawa, sasa mishipa yako inafanya kazi vizuri,” anasema Dk. Kissenge.
Hapo nashuhudia tabasamu pana likichomoza katika uso wa Lilian, “Namshukuru Mungu, asanteni sana madaktari wangu,”anasema.
Kila mmoja ndani ya chumba hiki anaonekana mwenye furaha, Lilian anaridhia kupiga picha ya ukumbusho na madaktari wote waliomuhudumia.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi anasema serikali imefunga mtambo huo BMH kwa wakati mwafaka kwani kuna idadi kubwa ya wagonjwa wanahitaji huduma ya aina hiyo.
“BMH inakuwa hospitali ya pili ya umma kufungwa mtambo huo, wa kwanza upo JKCI, mtambo mmoja wa aina hii unagharimu wastani wa Sh bilioni 5. Mwaka jana pekee pale JKCI kwa kutumia mtambo huu tuliwafanyia upasuaji wagonjwa zaidi ya 1,000.
“Kwa kutumia mtambo huu tuna uwezo wa kuchunguza mishipa ya damu iliyoziba na kuizibua kwa njia ya tundu dogo, huduma hii imekuja kwa wakati mwafaka, itasaidia kuokoa maisha ya wengi.
“Kwa sababu, kwa kawaida mtu akipata mshtuko wa moyo anatakiwa kupata huduma si zaidi ya saa moja na nusu, zaidi ya hapo athari huwa kubwa, kwani mtu asipopata huduma haraka anaweza hata kupoteza maisha, hivyo tuna furaha kubwa.
“Huu ni mwanzo wa safari ya kusogeza huduma hii karibu zaidi na wananchi, zitakapoimarika hapa tunatarajia zitasogezwa pia kwenye maeneo mengine nchini ikiwamo Mwanza.
“Ni kama mbio za marathon si kama za mita 100, tumeanza rasmi, tutajipanga vizuri kuhakikisha wataalamu wenzetu wanapata uzoefu kama tulionao JKCI, siku moja tutafikia lengo,”anabainisha.
Profesa Janabi anasema magonjwa ya moyo yanawakabili wengi akitolea mfano kwamba katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa rasmi JKCI wamehudumia wagonjwa zaidi ya 200,000.
“Kwa siku tunawazibua mishipa ya damu wagonjwa wanane hadi 10 kwa njia hii ya Cath Lab na kwa njia ya upasuaji mkubwa tunawazibua wagonjwa wawili hadi watatu, kila siku,”anabainisha.
Hali ilivyo BMH
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo BMH, Willfredius Rutahoile anasema kila mwezi huwa wanapokea wagonjwa wapatao 300 katika kliniki ya moyo.
“Hadi sasa kuna wagonjwa zaidi ya 60 ambao wanasubiri huduma hii, kati ya hao tumewachagua 20 ambao tumeanza nao kisha tutapanga tena ratiba kwa ajili ya kuwafanyia wale wengine waliobaki,”anasema.
Mkurugenzi wa BMH na Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk. Alphonse Chandika katika kipindi cha Septemba hadi Desemba, 2018 waliona jumla ya wagonjwa 942 katika kliniki ya moyo.
“Kati ya wagonjwa hao 501 walikuwa wanaume na 441 wanawake, utaona jinsi tatizo hili lilivyo kubwa na linahitaji nguvu ya kitaifa kulikabili, takwimu zinaonesha duniani kila mwaka watu wapatao milioni 17.5 hufariki dunia kwa magonjwa ya moyo.
“Hivyo kufungwa kwa mtambo huu ni hatua kubwa mno kwa hospitali hii, tunawashukuru JKCI kwa kukubali wito wetu, tunajivunia wataalamu wa Tanzania tumezindua huduma hii sisi wenyewe na hatutasimama, itakuwa endelevu.
“Watanzania waelewe kwamba serikali imedhamiria wanakuwa na afya njema na matibabu yote ya kibingwa yanapatikana nchini,”anasema.
Upekee wa mtambo
Dk. Kissenge anasema ni wa kisasa zaidi na wa kipekee kwani si tu una uwezo wa kuchunguza na kuzibua mishipa ya damu iliyoziba kwenye moyo bali hata kichwani na miguuni.
“Ni uwekezaji mkubwa ambao Serikali imeufanya, tunaishukuru, kwa sababu ilibidi wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali nchini wasafariri kuja Dar es Salaam.
“Kwa hiyo huduma imesogezwa karibu zaidi kwa wananchi hapa Dodoma na walio maeneo ya jirani, JKCI tutaendelea kushirikiana na BMH kutoa huduma hapa, tunawahakikishia watanzania kupata huduma nzuri,”anasema.
Kauli ya Wizara
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kuimarishwa kwa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo nchini kumesaidia kupunguza asilimia 95 ya wagonjwa waliokuwa wanapewa rufaa kwenda nje ya nchi kufuata matibabu.
Mwongozo migahawani
Ummy anasema pamoja na uimarishwaji wa huduma za matibabu sasa serikali inajikita katika kuhakikisha jamii inapata elimu ya jinsi ya kujikinga kupata magonjwa hayo.
Anasema ulaji usiofaa bado ni changamoto katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza hasa moyo, saratani na figo.
“Matumizi ya vyakula vilivyowekwa chumvi nyingi, mafuta mengi na sukari nyingi ni miongoni mwa visababishi vinavyotajwa kuchangia mtu kupata magonjwa hayo.
“Tunafikiria kuandaa miongozo mbalimbali itakayoelekeza kiwango cha chumvi, sukari na mafuta kinachopaswa kutumika kwenye vyakula hasa vya migahawani ili kuongeza nguvu ya kuwakinga wananchi.
“Nilikuwa nchini India nimeona wenzetu wana miongozo, tukaona ni jambo zuri,” anasema