Na Mwandishi Wetu
-DAR E SA SALAAM
SHIRIKA la Umeme la Ugavi wa Umeme Tanzania, (TANESCO), limesema lipo mbioni kukamilisha mtambo wa Kinyezi II ambako awamu ya kwanza ya megawati 30 itakamilika Desemba mwaka huu na kuingizwa kwenye gridi ya taifa.
Kukamilika kwa mtambo huo wa ufuaji umeme kwa kutumia gesi kutasaidia taifa kuwa na umeme wa uhakika na kuelekea kwenye uchumi wa Tanzania ya viwanda.
Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco Dk, Tito Mwinuka, alikuwa akizungumza Dar es Salaam juzi katika ziara kutembelea mradi wa umeme wa gesi wa Kinyerezi II ambao unatarajiwa kutoa megawati 240 za umeme.
Alisema hatua ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo ni sehemu ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
“Tumeona ni vema katika ziara hii tujumuike nanyi wanahabari muweze kuona mafanikio ya mradi huu ambao ulizinduliwa na Rais Dk. John Magufuli Machi mwaka huu.
“Hadi sasa kazi inakwenda vizuri na mradi huu utakuwa na mitambo minne ambayo kila mmoja utakuwa na uwezo kuzalisha umeme.
“Kwa awamu ya kwanza tutakamilisha Desemba mwaka huu ambako tutawasha mtambo na kuingiza umeme kwenye gridi ya taifa huku kazi zingine zikiwa zinaendelea hadi mtambo wote utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 240,” alisema Dk. Mwinuka.
Aliwahakikishia Watanzania mradi huo utakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.
“Niwahakikishie watanzania kuwa ifikapo Agosti mwakani (2018), mradi wa umeme Kinyerezi II utakamilika na hivyo tutaongeza megawati 240 kwenye gridi ya taifa,” alisema Dk. Mwinuka.
Kaimu Mkurugenzi huyo alifuatana na timu ya wakurugenzi akiwamo Abdallah Ikwasa (mhandisi anayeshughulikia uzalishaji), Khalidi James (mhandisi anayeshughulikia uwekezaji na miradi) na Kahitwa Bishaija (mhandisi anayeshughulikia usambazaji).
Dk. Mwinuka alisema Watanzania wanahitaji umeme wa uhakika na Serikali kupitia TANESCO imejipanga kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana kwa watanzania na hivyo kuchangia pato la taifa.
“Kama mjuavyo serikali imefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha shirika linatekeleza miradi hii na tayari Sh bilioni 110 zimetolewa na serikali katika kutekeleza mradi huu wa Kinyerezi II,” alifafanua.
Awali, Meneja wa Mradi wa Kinyezi II, Stephens Manda, alisema umeme utaanza kuingizwa kwenye gridi ya taifa kila mwezi kuanzia Desemba mwaka huu ambako megawati 30 zitaingizwa .
“Tuna mashine nane ambazo zitafua umeme huo kwa hiyo kuanzia Desemba Mosi mwaka huu tutaingiza megawati 30 kwenye gridi ya taifa na tutafanya hivyo kila baada ya mwezi mmoja kwani tunaelewa kuwa serikali ambayo imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda.
“Tunaona umeme umekuwa ni mahitaji makubwa na muhimu hivyo kila tutakapokamilisha mtambo mmoja tunaingiza umeme kwenye gridi ya taifa, hatutasubiri kuwasha mitambo yote minane,” alisema Manda.