*Mkoa kushomesha wanafunzi 43 waliopata daraja la kwanza kidato cha Nne
Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Serikali ya Mkoa wa Dodoma imesema itawasomesha jumla ya wanafunzi 43 kutoka shule saba za serikali waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana na kupata ufaulu wa daraja la kwanza la alama saba kwa Wavulana na wasichana alama saba hadi tisa kwa masomo ya kidato cha tano na sita.
Kati ya wanafunzi 43 watakaosomeshwa wavulana ni nane na wasichana ni 35 toka shule za Godegode Mtera Dam, Mlowa Barabarani, Lukundo, Dodoma Sekondari, Msalato Girls na Mpwapwa Sekondari.
Akizungumza jana jijini hapa, katika hafla ya utoaji tuzo kwa Walimu na Wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa kidato cha nne na darasa la saba mwaka 2021, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka, amesema watagharamia ada kwa wanafunzi hao pamoja na kuwanunulia vifaa vya shule.
Vifaa hivyo vinahusisha madaftari lengo likiwa kuongeza motisha kwa wanafunzi na wazazi ili waendelee kufanya vizuri katika masomo yao.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Elimu, Walimu Wakuu, walimu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma.
Mtaka amesema kipaumbele chake ni elimu, hivyo atahakikisha anapambana kwa kushirikiana na walimu kuongeza ufaulu wa mkoa huo katika mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne.
“Kazi ya serikali ya mkoa wa Dodoma kwa wanafunzi hawa ni kuwezesha na kuhakikisha ada na vifaa vinapatokana, wajibu wa mzazi utabaki katika suala la sare za shule, mzazi mtoto wako akipangiwa shule njoo na barua yake tuletee sisi tunampatia vifaa na pamoja na kulipa ada.Na leo tunawapatia madaftari 9 kila mmoja,” amesema Mtaka.
Pia mtaka amenunua alama “A” kwa Sh 5,000 kwa walimu waliowasaidia wanafunzi kupata alama hiyo huku akidai kwa mwaka 2022 atanunua kwa Sh 10,000 lengo likiwa ni kuzidi kuongeza motisha kwa walimu.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Afisa Elimu kuwaandikia barua wakuu wa shule ili ziende kwenye matangazo ya bodi za Vijiji siku ya kufunnga shule wazazi waende kwenye kikao cha shule lengo kuhakikisha wanafunzi wanafaulu.
Pia, walimu wametakiwa kuwa wabunifu katika ufundishaji wao ikiwemo kuwasidia wanafunzi waweze kufaulu mitihani yao huku akifurahishwa na ubunifu ulioonyeshwa na baadhi ya walimu akiwemo mwalimu wa shule ya sekondari Godegode ambaye alionyesha ubunifu katika ufundishaji wa masomo ya sayansi licha ya kutokuwa na vifaa vya kufanyia mazoezi kwa vitendo.
Vilevile, amezitaka kamati za kitaaluma zikae na kuona namna yakuwa na mitihani ya mara kwa mara ili kupata namna nzuri ya maandalizi ya mitihani ya sekondari hasa kwa kutembelea shule ya sekondari Bunge kwani inawafunzi wanaotoka katika shule bora.
“Ufaulu wa mtoto ni faida kwa taifa hivyo maandalizi yanaanza na mzazi mwenyewe hivyo mzazi ana wajibu kuchangia, ikifika mahala wazazi wakaonanumuhimu wa elimu wataweza kusaidia taifa,” amesema.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk.Fatma Mganga amesema kuwa tuzo hizo zitatoa hamasa kwa Walimu na wanafunzi katika ufundishaji na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza katika kuwekeza kwenye suala la elimu.