Na SARAPHINA SENARA (UoI) – DAR ES SALAAM
MTAALAMU wa masuala ya saikolijia kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Baraka Mushobozi, ameeleza madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya, akisema kuwa ni pamoja na kupoteza kumbukumbu na kusababisha matatizo ya moyo.
Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu alisema matumizi ya madawa yanaweza kuwa ya muda mrefu ama mfupi kutokana na muda ambao mtu ameanza matumizi hayo.
“Adhari mojawapo anayoweza kuipata mtu ni kufeli kwa figo na hii ni ya muda mrefu ambayo inaweza kutokea kwa yule anayetumia unga na inaweza kuleta madhara baada ya matumizi ya muda mrefu kwa mhusika.
“Mtu anaweza kupata hata vidonda vya tumbo kuharibika kwa seli za ubongo na wakati mwingine anaweza kupata saratani, haya yote tunasema ni matumizi ya muda mrefu ambayo anaweza kukutana nayo mtu mwenye matumizi ya madawa ya kulevya,”alisema Mushobozi.
Hata hivyo alibainisha madhara ya muda mfupi ambayo anaweza kupata mtu anayetumia madawa ya kulevya kama vile,kupata maumivu makali ya kichwa ,joto kupanda na wakati mwingine kupata hisia ambazo sio nzuri kwake.
“Mtu anapoanza matumizi ya madawa anaweza kukutana na madhara ya muda mfupi kwa sababu unapoanza kutumia inakutaka kila wakati uhakikishe unaendelea kupata na pale mtu anapokosa ndio huanza kukutana na changamoto tulizosema.
“Hata kama mtu alianza kutumia madawa kwa kujaribu tu baada ya masaa sita atakuwa anataka tena kuendelea kutumia na hii ndio hufanya watu wengi kuendelea kutumia madawa kwasababu tu waliamua kujaribu”alisema.
Adhari nyingine ni kuwa na migogoro ya mara kwa mara katika eneo analoishi wakati mwingine kazini au hata katika familia huku wakiwa watu wanaovunja sheria zaidi na hii inatokea zaidi kwa wale wa Uraibu.
Aidha alisema ziko sababu nyingi zinazopelekea mtu kuanza matumizi ya madawa ya kulevya japokuwa kwa upande wa vijana wamekua na mazoea ya kujaribu sana ukilinganisha na makundi mengine hivyo kupelekea kuendelea kutumia na wengine kushindwa kabisa kuacha.
“Vijana wamekua wakijaribu na baada ya kujaribu wanajikuta kuendelea na matumizi ya madawa na hii inatokana na sababu ambayo kitaalamu tunaita (Experimental) yani kujaribu na imekua sababu kubwa inayopelekea vijana kuanza matumizi ya madawa ” alisema Mushobozi.
Alisema ushawishi pia unaweza kuchangia kwa namna moja ama nyingine watu kutumia madawa kama tu watakua na watu ambao wanajaribu kuwashawishi kuanza kutumia na wakati mwingine ikichochewa na kundi rika kwa namna Fulani.
Aliongezea kwamba wengine wamejikuta wakitumia madawa kwasababu ya vina saba vyao ambavyo vipo ndani ya damu zao kwa mfano matumizi ya vinywaji vikali pia yanaweza kutokana na vina saba huku akidai kuwa hata tabia ya mama kutumia madawa wakati wa kipindi cha ujauzito kinaweza kupelekea matumizi baada ya muda Fulani kwani mtu huyo alishazoea matumizi hayo tangu akiwa tumboni.
“Wapo watu wanaotumia madawa kwasababu tu walitakiwa kufanya hivyo hasa pale ambapo mtu anakosa usingizi inamlazimu kuanza kutumia madawa ili apate usingizi na hii pia ni sababu ya mtu kuanza kutumia madawa,”alisema Mushobozi.
Aliongeza kuwa wengine wamekua wakitumia madawa ya kulevya kwasababu tu ya kujifurahisha hivyo hakuna sababu yoyote iliyowapelekea wao kuanza kutumia.
“Elimu ya saikolojia inahitajika sana ilikuweza kusaidia watu wengi kuondokana na hii hali na kabla hatujakutana na mtu ambae ameshaathirika na matumizi ya madawa tunahusisha saikolojia,hospitali tukimaanisha matibabu pamoja na watu wanaomzunguka.
“Haya yote yanaweza kumsaidia mtu huyo na kabla ya kumsaidia ni muhimu tukatazama kwanza mambo hayo ili kuweza kusaidia lakini pia ikiwa na imani maana ni vizuri pia kujua kuhusu mambo ya kiimani zaidi,”alisema Mushobozi.
Familia imekua na mchango mkubwa katika malezi hivyo ni vyema wazazi au hata walezi kuzingatia malezi ya watoto wao na mienendo katika maisha ya watoto wao.
Alisema watu wanapaswa kukubaliana na ukweli unaowakabili maana kukimbilia kutumia madawa huongeza matatizo zaidi badala ya kumaliza tatizo na kama ni kuwa na msongo wa mawazo basi hauwezi kumalizwa na madawa.