26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Msongo wa mawazo, uchovu kichocheo cha ajali barabarani

*Uchunguzi wabaini madereva wengi hupata ajali kutokana na matatizo yanayowazunguka

ANDREW MSECHUDAR ES SALAAM

UCHUNGUZI umebaini kuwa madereva wengi hupata ajali kutokana na msongo wa mawazo, hasa kutokana na matatizo ya kifamilia, kipato na matatizo katika jamii zinazowazunguka.

Akizungumzia haki hiyo, Meneja wa Usalama Barabarani na Mazingira

wa Mamlama ya Usafiri wa Nchi Kavu na Baharini (Sumatra), Geoffrey Silanda anasema katika baadhi ya chunguzi za vyanzo vya ajali barabarabni wamebaini kuwa pamoja na mambo mengine, msongo wa mawazo na uchovu kwa madereva vimekuwa vikichangia ajali hizo.

Anasema kupitia uchunguzi uliofanywa na kamati maalumu ya kuchunguza ajali za barabarani iliyoundwa baada ya kutokea kwa ajli ya gari dogo aina ya Toyota Hiace na basi la New Force mkoani Morogoro, ulibaini kuwa ajali hiyo ilikuwa inaweza kuepukika kama dereva asingekuwa na msongo wa mawazo.

“Kamati hiyo iliundwa baada ya kutokea ajali ya Machi 4, 2018 majira ya saa 4:00 asubuhi, baina ya basi lenye usajili wa namba T346DLY lililokua likielekea Tunduma. Basi hili linalomilikiwa na Kampuni ya New Force liligongana na basi dogo aina ya Toyota Hiace lenye usajili namba T962BSE linalomilikiwa na Harold Sugunga lililokuwa likielekea Morogoro mjini. Ajali hii ilisababisha vifo vya watu watano na majeruhi tisa,” anasema.

Chanzo cha ajali

Silanda anasma kamati hiyo ilibaini kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa dereva wa basi dogo aina ya Toyota Hiace, ambaye alikuwa akijaribu kulipita lori lililokua mbele yake na katika mchakato wa kulipita lori hilo aligongana na basi la New Force lililokuwa likija mbele yake likitokea Morogoro kuelekea Tunduma.

“Kamati ilibaini kuwa dereva wa basi la New Force hakufanya jitihada zozote za kulizuia basi lake ili kuepusha ajali, baada ya kuona hatari kubwa iliyokuwa mbele yake baada ya maamuzi ya dereva wa Toyota Hiace kuhama kutoka kwenye njia yake kwenda upande wa magari yanayo elekea Tunduma,” anasema.

Anasema kamati hiyo iliundwa na Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra kwa mujibu wa kifungu namba 18(1) cha Sheria ya SUMATRA ya Mwaka 2001, aliunda Kamati ya kufanya uchunguzi ili kuweza kubaini chanzo cha ajali, ikipewa jukumu la kutoa ushauri kwa nia ya kuzuia ajali za namna hiyo zisitokee tena.

Silanda anasema kamati hiyo ilifanya ukaguzi katika ofisi za Kampuni ya New Force na kubaini kuwa wana mfumo mzuri wa matengenezo ya mabasi, kuona nyaraka za mikutano ya kujadili mambo mbalimbali ya nayohusu udereva na unaolenga katika kuimarisha ufahamu wa mambo ya usalama barabarani

Dereva wa Hiace

Silanda anasema wakati wa uchunguzi, kamati ili baini kuwa dereva wa Hiace (marehemu) alikuwa na ugomvi na mke wake uliosababisha wawili hao kutengana, ulioanza na kushamiri kutokana na ugomvi mkubwa baina ya mama wa marehemu (Mama Jackson) na mke wa marehemu uliosababisha Mama Jakson kulazwa hospitalini baada ya kupigwa na mke wa marehemu.

“Hali hii ilimfanya dereva (marehemu) kuwa katika katika msongo wa mawazo/sonona kwa muda wa siku tatu mfululizo. Ilikuwa siku ya Jumapili (siku ya ajali) alipoamua kwenda kuendesha gari ili aweze kupata fedha za kumpa mmiliki wa gari.

“Siku ya Jumapili huwa na wasafiri wengi wanaotoka na kuelekea katika Kjiji cha Mlali. Katika kipindi chote alichokuwa akiendesha gari Jaskson alikuwa katika hali ya msongo wa mawazo, hali hii ilithibitishwa na kondakta na mama wa marehemu aliyehojiwa na Kamati, mama yake mzazi pamoja na ndugu wa karibu na marahemu,” anasema.

Anasema katika ajali hiyo iliyotokea katika Barabara Kuu ya Morogoro na Iringa kuna eneo lenye urefu wa takribani 0.8KM ambalo linaonekana bila kizuizi chochote, ambapo barabara imenyooka na magari yanaruhusiwa kuyapita magari mengine.

Silanda anaeleza kuwapamoja na kuwepo kwa ugomvi mkubwa katika familia ya Jackson (dereva) wiki moja kabla ya ajali kutokea, lakini pia basi dogo la Hiace lilikua limebeba abiria 23 na mizigo kuzidi uwezo wake na kamati ilibaini kuwa kutokuwepo kwa alama ya kuonesha mwanzo wa kilometa 50 kwa saa na mwisho pande zote.

Ajali ya Mkuranga

Silanda anasema Machi 24, 2018 majira ya saa 2:30 usiku lori lenye usajili wa namba T223CZB na tela namba T371CDT lililokua limepakia chumvi likitokea Kilwa likielekea Mwanza, liligongana na Basi dogo aina ya Toyota Hiace lenye usajili namba T676 DGK lililokuwa likitoka Mbagala rangi tatu kuelekea Kimanzichana.

Anasema ajali hii ilisababisha vifo vya watu 26 na majeruhi wanane ambapo ilibainika kuwa chanzo cha ajali ni dereva wa lori kushindwa kulimudu gari lake lililokua katika gia kubwa na mwendokasi kwenye kona kali katika mlima.

“Kutokuwepo kwa alama za barabarani katika eneo la ajali kama unatokea Lindi (ukomo wa mwendokasi na kuwepo kwa kona kali) ni moja ya sababu zinazosababisha pia ajali hizi,” anasema.

Abasena kamati ilibaini kuwa ajali hiyo ilichangiwa pia na ubovu wa mfumo wa breki kwenye tairi za nyuma za lori hilo na wakati mwingine uchovu kwa dereva, lakini pia basi dogo la Toyota Hiace lilikua limejaza abiria kuzidi uwezo wake.

Ajali ya Igunga

Silanda anasema Aprili 4, 2018 majira ya saa 2:00 lori lenye usajili wa namba T486ARB lililokua limepakia viazi mviringo likitokea Njombe likielekea Mwanza, liligongana na Basi aina ya Scannia (City boy) lenye usajili namba T983DCE lililokuwa likitoka Karagwe kuelekea Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi 49.

Anasema ajali hiyo ilitokea baada ya lori kuhama kutoka upande wake kwa nia ya kukwepa shimo kuelekea upande mwingine ambao basi lilikua linakuja.

Anaeleza kuwa ajali hiyo ilitokea katika eneo la Makomero, katika Wilaya ya Igunga umbali wa kilomita 20 kutoka Mji wa Igunga kuelekea Singida, ambapo kamati ilibaini kuwa alama za barabarani zilikuwepo na zilikuwa zina onekana vizuri , ingawa alama hizo hazikuwa kwenye kiwango kinachotakiwa.

“Kamati imebaini kuwa basi lilikuwa na madereva wawili wakati wa kuanza safari hata hivyo dereva wa pili anaejulikana kwa jina la Deus Richard Lweikiza hakuweza kuonekana baada ya ajali. Lakini pia dereva wa basi hakupunguza mwendo pamoja na kuwa ilikuwa usiku na mvua ilikuwa ikinyesha. Dereva wa basi alikuwa amewasha taa kubwa na kuna uwezekano kuwa alisababisha dereva wa lori kutoona vizuri,” anasema.

Anaongeza kuwa taarifa zilizo patikana katika mfumo wa VTS zilionesha kuwa dereva wa basi wakati wa kupishana aliongeza mwendo kutoka kilometa 81-82 lakini pia dereva wa lori aliendesha gari bovu kwa kuwa matairi yalikuwa yamekwisha.

“Dereva wa lori hakuchukua tahadhari yoyote kupunguza mwendo kabla ya ajali au kupishana. Kuna ushahidi kuwa dereva wa basi alikuwa na uchovu kwa sababu aliendesha zaidi ya masaa kumi na mbili bila kupumzika. Hali hii ilisababisha kupunguza umakini. Dereva wa lori hakutoa taarifa kwenye kituo cha polisi kama inavyotakiwa kisheria,” anasema.

Mapendekezo

Silanda anasema kutokana na sababu zilizoainishwa na kamati hiyo, mongoni mwa mambo muhimu yanayopendekezwa ni kuimarishwa kwa utaratibu wa kuzitatua changamoto zilizopo kwa kuimarisha mafunzo kwa madereva na kutatua changamoto za alama za barabarani.

Anasema suala jingine ni kutatua changamoto za mwendokasi wa magari, kuwepo na manejimenti ya uchovu wa madereva, kutatua changamoto za matengenezo ya za magari, kuimarisha ubora wa matengenezo ya magari, matumizi sahihi ya mikanda kwenye magari, upimaji wa vileo kwa madereva, ulipwaji wa bima kwa wahanga wa ajali, pia kukabiliana na changamoto ya kupakia abiria/mizigo kuzidi uwezo wa magari

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles