NAIROBI,KENYA
MSOMI na mwanasiasa wa Kenya Dk. Reuben Savai, 70, ambaye jaribio lake la kuwania kiti cha urais mwaka 1997 na 2002 lilitibuka, amefariki.
Mwanawe wa kiume, Daniel Lihanda amenukuliwa na Gazeti la Daily Nation nchini Kenya, akithibitisha kifo chake kilichotokea Jumapili.
Licha ya kuwa na shahada sita na cheti cha diploma, mwanasiasa huyo mtata hakuwahi kupata kazi nchini Kenya.
Juhudi za Dk Savai ambaye ni kiongozi wa chama cha Kenya Republican Reformation Party kupata kazi Kenya ziligonga mwamba licha ya kusomea shahada sita nchini Ugiriki na diploma kutoka Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
Baadhi ya vitu alivyosomea ni pamoja na Diploma ya Thiolojia, Shahada moja ya sheria, shahada mbili za elimu na nyingine moja ya Sayansi.
Familia yake inasema alizuiliwa kufanya kazi ya sheria nchini Kenya kwa sababu hakufuzu katika chuo cha mafunzo ya sheria nchini humo.
Dk. Savai, ambaye alitaka kuwampinga marais wastaafu wa Kenya Daniel arap Moi na Mwai Kibaki, alizuiliwa kuwania kiti cha urais kwa kukosa stakabadhi zilizohitajika kuidhinishwa kushiriki chaguzi hizo.
Miaka ya 1990 iliporejelea siasa ya vyama vingi alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha Forum of Restoration and Democracy (Ford), Kenya.
Mwaka 1997, Dk. Savai aliwania kiti cha ubunge cha Lang’ata lakini alishindwa na Raila Odinga, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa chama cha National Development Party (NDP).
Eneo la Lang’ata liligawanywa mara mbili- Lang’ata na Kibra – baada ya kufanyika uhakiki wa mipaka kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2013.
Lihanda aliliambia gazeti la Nation kuwa baba yake alipakutwa amefariki nyumbani kwao katika kile kinachoshukiwa kuwa kupooza.
Lihanda anasema baba yake hakuwahi kuajiriwa nchini Kenya licha ya kisomo kikubwa alichokuwa nacho na kujihusisha kwake katika siasa za nchi hiyo.
“Alisomea Ulaya na kupata shahada sita na cheti cha Diploma. Aliporudi Kenya hakuwahi kupata kazi akaamua kujitosa katika siasa,” alisema Lihanda.
Aliongeza kuwa baba yake alikuwa akisumbuliwa na tattizo la shinikizo la damu licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Familia ya mwanasiasa huyo sasa inatoa wito kwa wahisani kuisaidia kuchangisha dola 1,274 kugharamia mazishi yake.
Mwili wake umepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti mjini Kaimosi Magharibi mwa Kenya