‘MSISEME NUSU KAPUTI, SEMENI TIBA YA USINGIZI’

0
1965

Na Veronica Romwald, Dar es salaam

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya ameishauri jamii kuacha kutumia neno nusu kaputi badala yake watumie tiba ya dawa za usingizi.

Akifungua mafunzo ya awamu ya tatu kwa wataalamu wa dawa za usingizi jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Machi 5, Dk. Mpoki amesema neno hilo huwaogopesha wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji.

“Sijajua kihistoria neno kaputi linapotoka lakini haraka haraka maana yake ni mtu amekufa, hivyo unaposema nusu maana yake umeua mtu nusu na nusu nyingine bado yupo hai.

“Sasa hii inawaogopesha sana wagonjwa, tungependa jamii itambue kwamba fani hii inatoa dawa ya kulaza wagonjwa au dawa ya mtu asisikie maumivu wakati akipasuliwa kwani huwa anakatwa na anahisi maumivu,” alisema.

Alisema ndiyo maana wataalam wanaotoa tiba hiyo wanatambulika kama wataalam wa tiba ya usingizi na si wataalamu wa nusu kaputi.

“Ili kuondoa ule woga kusudi mtu ajue anakwenda kule anapewa dawa ya usingizi na tunajua mtu anapolala kuna kuamka, ndiyo maana tunapenda neno hili, sisi tunatoa dawa ya usingizi na mtu anaamka baada ya upasuaji,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here