25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, February 13, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Msimu wa 23 wa Kilimanjaro Marathon wazinduliwa kwa shangwe Moshi

Na Safina Sarwatt, Mtanzania Digital

Msimu wa 23 wa mbio maarufu za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2025 umezinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Salinero, Moshi. Hafla hiyo, iliyojumuisha wadau mbalimbali wa michezo, ilitangaza maandalizi ya mbio hizo ambazo zinatarajiwa kufanyika Februari 23, 2025.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Katibu Tawala wa Mkoa, Kiseo Yusuf Nzowa, aliwapongeza wadhamini na waandaaji kwa juhudi zao endelevu za kuimarisha tukio hilo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.

“Mbio hizi zimekuwa maarufu barani Afrika, zikiwa na washiriki zaidi ya watu 12,000 kutoka takriban nchi 56. Hii ni fursa kubwa kwetu sio tu katika sekta ya michezo, bali pia utalii na biashara. Ni lazima wadau waendelee kushirikiana ili kuhakikisha tunaboresha zaidi tukio hili,” alisema Nzowa.

Faida za kiuchumi na kijamii

Nzowa alieleza kuwa mbio hizo zimeongeza mzunguko wa fedha ndani ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro, zikiimarisha biashara ndogo na kubwa. Alitoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa huduma bora ili kulinda heshima ya Mkoa katika nyanja za kibiashara na kimataifa.

“Ni dhahiri kuwa mbio hizi zimeleta mabadiliko makubwa kwa jamii. Kwa mfano, tukio hili limekuwa kichocheo kikubwa cha shughuli za kitalii, huku likiimarisha biashara za malazi, usafiri, na vyakula,” aliongeza Nzowa.

Wadhamini na zawadi za washindi

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Khensani Mkhombo, alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa sehemu ya tukio hili kwa miaka 23 kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager. Alitangaza kuwa jumla ya shilingi milioni 30 zimetengwa kwa zawadi za washindi wa mbio za kilomita 42, ambapo washindi wa kwanza wa mbio hizo kwa wanaume na wanawake kila mmoja atapokea shilingi milioni 5.5.

“Mbali na zawadi kwa washindi, pia tunatarajia kuchangia asilimia 5 ya malipo yote ya kiingilio kwa Shirika la Tumaini la Maisha (TLM), kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani katika hospitali ya KCMC,” amesema Mkhombo.

Afisa Mkuu wa Biashara wa YAS, Isack Nchunda, alisema kuwa Yas Half Marathon, inayoshirikisha washiriki takriban 6,500, itaendelea kuboresha uzoefu wa washiriki mwaka huu. Aliongeza kuwa mbio hizo zinasaidia si tu kukuza michezo, bali pia kuimarisha mshikamano wa jamii na sekta ya utalii.

Mipango na maendeleo ya msimu wa 2025

Kwa mujibu wa waandaaji, mbio za mwaka huu zitajumuisha matamasha ya siku tatu kuanzia Ijumaa hadi Jumapili, yakilenga kuongeza mzunguko wa biashara mjini Moshi. Mbio hizo zitaanzia na kumalizikia katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Waandaaji walieleza kuwa zawadi zitakazotolewa kwa jumla ni shilingi milioni 53 kwa washindi wa vitengo vyote, zikiwemo mbio za kilomita 42 na 21.

Maandalizi ya kipekee

Kamati ya maandalizi imeeleza kuwa ushirikiano wa wadhamini wakuu kama Kilimanjaro Premium Lager, Yas, CRDB Bank, na Simba Cement umewezesha ufanisi mkubwa wa tukio hilo. Washiriki na mashabiki wanatarajiwa kushuhudia tukio lenye viwango vya kimataifa, huku maabara maalum za uchunguzi wa muda na vifaa vya usalama vikiongezwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
594,000SubscribersSubscribe

Latest Articles