23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Msimamizi wa barabara anusurika kusweka ndani

Na Allan Vicent, Tabora  

Msimamizi wa kampuni ya Battalion Construction Co.Ltd ya mkoani Tabora inayotekeleza mradi wa barabara ya lami wilayani Igunga, Nicholaus Kandidas amenusurika kuswekwa mahabusu kwa kushindwa kutoa maelezo ya kina ya sababu za kukwamisha mradi.

Tukio hilo limetokea juzi baada ya Mbunge wa Jimbo la Igunga Mjini, Nicholous Ngassa kutembelea barabara inayojengwa na kampuni hiyo kwa kiwango cha lami na kukuta hakuna kazi yoyote inayoendelea katika barabara hiyo yenye urefu wa km 1.0 huku mitambo ya kampuni hiyo ikiwa imeegeshwa pembeni. 

Mbunge alitaka kujua ni kwanini ujenzi umesimama na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi ikiwemo maji kuingia katika nyumba zao mvua inaponyesha kutokana  na mkandarasi huyo kutoweka njia ya kuchepushia maji.

Akibu swali hilo Msimamizi alidai kuwa wamesimama kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, majibu ambayo hayakumfurahisha mbunge hasa kutokana na ukweli kuwa hakukuwa na mvua yoyote na jua linaendelea kuwaka.

‘We Msimamizi usinichafue, naweza kukuweka ndani sasa hivi, haiwezekani usingizie mvua wakati hainyeshi na jua linaendelea kuwaka na pia wakandarasi wenzio hapahapa Igunga wanaendelea na ujenzi, huu ni uzembe,’ alisema Ngassa.

Ngassa alibainisha kuwa kampuni hiyo ilisaini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ya kutoka Mtaa wa Posta hadi eneo la benki ya CRDB yenye urefu wa kilomita 1.0 kwa gharama ya Sh milioni 500.

Aliongeza kuwa baada ya kukagua barabara hiyo amebaini kujengwa chini ya kiwango jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho kwani hayuko tayari kuona fedha ya walipa kodi ikipotea.

 Alitaja mapungufu yaliyopo kuwa ni kutokuwepo mhandisi mwenye sifa katika kampuni hiyo, kutochimba mifereji wala kutoa tope na vifusi na kasi ndogo ya utekelezaji, kwani hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 5.

 Ngassa alibainisha kuwa uwezo wa mkandarasi huyo ni mdogo hivyo kutokana na hali hiyo amemwandikia barua Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora ili kumchukulia hatua zaidi.

Aidha aliongeza kuwa amemwandikia barua Mkuu wa wilaya hiyo Sauda Mtondoo, Mkuu wa Mkoa Balozi Dk. Batilda Buriani na pia amemwagiza Kamanda wa  TAKUKURU wilaya humo Francis Zuakuu kuchunguza mradi huo.

Msimamizi wa kampuni hiyo Nicholaus Kandidas alikiri kuwepo kwa mapungufu hayo yaliyobainishwa na mbunge huku akiahidi kuyafanyia kazi kwa kurudia sehemu zote zenye mapungufu.

Baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo, Rose Josephat, mfanyabiashara na fundi pikipiki, Emmanuel Edson walilamikia uzembe wa mkandarasi huyo ambao umekuwa ukisababisha maji kuingia katika nyumba zao pindi mvua inaponyesha.

Walibainisha kuwa kama mkandarasi huyo ataachwa aendelee na mradi huo, barabara hiyo haitadumu kwa kuwa ipo chini ya kiwango.

Meneja wa TARURA wilaya humo Mhandisi Sadick Karume alisema mkandarasi huyo alisaini mkataba huo Oktoba 1, 2021 ambapo alitakiwa kumaliza kazi hiyo Aprili 1, 2022. 

Alibainisha kuwa tayari amemwelekeza kuongeza kasi ili kumaliza kwa muda uliopangwa na kwa viwango vinavyotakiwa huku akithibitisha kuwa amemwagiza kuyafanyia kazi mapungufu yaliyopo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles