Msimamizi mirathi ya marehemu Balali kizimbani kwa utakatishaji fedha

0
778

Kulwa Mzee -Dar es salaam

MSIMAMIZI wa mirathi ya marehemu Daudi Balali, Elizabeth Balali (54) amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ulaghai na kutakatisha fedha.

 Mshtakiwa huyo mkazi wa Boko Magengeni, Dar es Salaam alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka ya kujipatia Sh milioni 25 kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina kwamba kati ya Oktoba 19 na Desemba 21, 2017 Dar es Salaam, mtuhumiwa alijipatia Sh milioni 25 kutoka kwa Dk. Roderick Kisenge kwa ulaghai.

Mshtakiwa anadaiwa kujifanya anamuuzia eneo la mita za mraba 900 ambalo halijapimwa lililopo eneo la Boko Dovya, Kinondoni wakati akijua eneo hilo si lake.

Wankyo alidai katika kipindi hicho, mshtakiwa huyo alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Dk. Kisenge kupitia akaunti yake iliyopo katika Benki ya CRDB wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashtaka, Elizabeth hakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza makosa ya uhujumu uchumi.

Hakimu Mhina alimfahamisha mshtakiwa huyo kuwa licha mahakama kutokuwa na uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo, pia shtaka la utakatishaji wa fedha halina dhamana.

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika, kesi imeahirishwa hadi Oktoba 24, kwa kutajwa na mshtakiwa alipelekwa rumande.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here