29.3 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Msikubali kurubuniwa na wasiotutakia mema-Majaliwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania hususani vijana wasikubali kurubuniwa na makundi ya watu wasio na mapenzi mema na nchi yetu ambao watataka kuwatumia kwa maslahi yao binafsi na hatimaye kuhatarisha usalama na amani ya nchi yao.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana Alhamisi, Desemba 10, wakati akifungua mkutano Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma. Amewasisitiza Watanzania wawe wazalendo kwa nchi yao.

“Uzalendo ndio utalifanya Taifa liendelee kujitegemea, hivyo ni muhimu suala hilo likapewa kipaumbele. Tusimkubali kushawishiwa na Mtanzania yeyote anayetumiwa na watu wenye lengo la kutaka kuja kututawala, tusikubali lazima tuendelee kuwa  huru na tulinde rasilimali kwa manufaa ya wote.”

Waziri Mkuu amesema uzalendo ni muhimu sana katika kujenga umoja wa kitaifa na Vijana ni zaidi ya asilimia 60 ya wananchi wa Tanzania, hivyo wakipata misingi mizuri ya uzalendo tutajenga Taifa imara, lenye mshikamano, nguvu na kuendelea kudumisha Amani nchini.

Amesema Serikali kwa kutambua hilo, kupitia Ilani ya CCM 2020-2025, imeweka msisitizo wa kuhamasisha na kuelimisha wananchi juu ya masuala ya uzalendo wa Kitaifa. “Suala la uzalendo ni muhimu sana kwa mustakabali na maendeleo ya Taifa lolote.”

Waziri Mkuu amesemaamefurahi kuona skauti wenye umri mdogo katika mkutano huo na kwamba wanachama wa chama cha skauti huanzia umri wa miaka mitano na kuendelea, ni dhahiri kuwa malezi na makuzi ya uzalendo kuanzia utotoni yatawezesha ujenzi wa Taifa imara lenye wananchi wenye kuipenda nchi yao, kuilinda na kuithamini.

“Hawa ndio viongozi bora wa baadaye ambao watailinda ipasavyo na kamwe hawatakubali kuwa vibaraka wa mataifa ya ughaibuni. Hivyo natoa wito kwa chama cha skauti kuweka mkakati wa kuhakikisha mnawafikia vijana wa rika mbalimbali katika kutoa elimu ya uzalendo.

Waziri Mkuu amesema vitendo vya uvunjifu wa amani na uharibifu wa miundombinu ni ukosefu wa uzalendo na kutothamini kodi za zinazolipwa na wananchi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. “Vijana wakilelewa katika misingi ya uzalendo watakuwa walinzi bora wa Taifa letu.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema mlezi wa Skauti Taifa ni Rais Dkt. John Pombe Magufuli na wakuu wa mikoa wote ni walezi wa skauti wa mikoa kwa nafasi zao, hivyo amewataka wakuu wa mikoa wasiolea Skauti katika maeneo yao wajitathmini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu hao wa mikoa wahakikishe wanampelekea taarifa ya idadi ya Skauti walioko kwenye mikoa yao na kwamba Serikali inahitaji kuona Skauri ikiendelezwa.

Pia, Waziri Mkuu amewataka vijana wa Skauti wazingatie maadili na wawe chachu kwa wengine kuwa na mwenendo mwema. “Wakati wote skauti wasijihusishe na vitendo viovu vya uvunjifu wa amani bali wawe kielelezo cha ushupavu, uchapakazi, uadilifu, nidhamu na uzalendo. Kwa nafasi zao wawe wepesi kutoa taarifa pale ambapo wamebaini kuwepo kwa vitendo viovu.”

Nitoe maagizo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi na Vijana ahakikishe kwamba masuala ya Skauti yanaingizwa kwenye programu zote za mafunzo kwa vijana. Aidha, mada ya uzalendo ijumuishwe kila yanapotolewa mafunzo mbalimbali kwa vijana mfano mafunzo ya ujasiriamali, urasimishaji wa biashara na upatikanaji wa mitaji.”

Waziri Mkuu ameitaka Ofisi Rais-TAMISEMI ichukue wajibu wa kuratibu shughuli za Skauti na kusisitiza ushiriki wa vijana wengi walioko shuleni na pia kuhakikishe skauti inawekewa msititizo kwenye utekelezaji wa mitaala kuanzia shule ya msingi ili kujenga Taifa imara.

Awali, Skauti Mkuu Chama cha Skauti Tanzania, Mwantumu Mahiza aliiomba Serikali iwapatie eneo jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga Kambi Kuu ya Kimataifa ambayo itakuwa na Chuo cha Ufundi, nyumba ya kulea vijana walioathirika na dawa za kulevya, kituo cha michezo, karakana, hoteli ya mafunzo, maeneo ya utalii na utamaduni, bustani za michezo na mashamba darasa.

Waziri Mkuu alisema Serikali iko tayari kuwaunga mkono ili wafanikishe maono yao na hivyo aliielekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mlezi wa Skauti katika Mkoa kushirikiana na Chama cha Skauti ili kuhakikisha hicho kinamilikishwa eneo na kuanza kutekeleza mipango iliyotajwa na kuweza kujitegemea kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles