25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

MSIJIDANYANYE HATA ULAYA NI KAZI TU!

UKITAKA uingie kwa miguu miwili katika dimbwi la ufukara uliobobea basi kaa vijiweni, halafu yale mawazo unayoyapata pale uyafanyie kazi.

Juzi Abiria wa Mwendo kasi alikikumbuka kijiwe chake cha miaka nenda miaka rudi, kipo Mwananyamala hapahapa Bongo na katika historia kijiwe hicho kimedumu zaidi ya miaka 20.

Wanabadilishana masela tu hawa wakizeeka, au kutoweka duniani basi wanaibuka wengine, lakini cha ajabu kila anayekuja aneendelea falsafa zilezile.

'Topiki' ya juzi ndiyo iliyonistua maana ilikuwepo tangu miaka ya mwanzoni ya 1980 ambapo vijana wa Bongo enzi hizo tuliaminishwa, nasi tukajiamnisha kwamba maisha ya Ulaya ni bora kuliko hapa kwetu.

Enzi zile tuliamini kama msela, ukipata bahati ya kupata kazi melini, bila kujali kama uliingia kwa staili ya kuzamia au kufanyiwa mipango na wazee wa Bandari basi wewe utakuwa umefanikiwa kimaisha.

Kana kwamba kazi ya meli haina changamoto zaidi ya kuipata na kuanza kuishi vizuri, tena uzuri wa kazi hiyo ilipewa sifa za ziada kwa kuwa mtu akitoka mle na kuingia katika vijiwe vyake, anabadilika na kuwa siyo yeye tena.

Miongoni mwa mambo ambayo kijana alikuwa akiyapigania muda mfupi tu baada ya kupata kazi melini ni kununua mikufu na pete za dhahabu.

Kwa vile enzi hizo upatikanaji wa nguo chakavu a.k.a mitumba ulikuwa adimu basi baharia akipata na suruli mbili tatu za jinsi na raba basi ameshakuwa yeye ndiyo mtu miongoni mwa watu.

Kwa bahati mbaya zama zile zilishapita, leo hii bahari atakayejea nchini akitokea Ulaya unaweza kumtambua kwa yeye mwenyewe kujitambulisha, lakini siyo kwa mitumba yake, manukato ya pafyum yake, au hata kwa raba, maana sasa zinapatikana hata pale Manzese, tena kwa bei ya kutupa.

Hata ukiingia kwenye vibanda vya gongo siku hizi unakuja msela kapigilia raba kali, ana jinsi na akijiongeza kidogo anakuwa na cheni nzuri tu 'made in Kariakoo'.

Pale kijiweni nikazikuta tena zile falsafa za Ulaya ni bora kuliko kwetu, kwamba kule ukiamka asubuhi tu unapiga supu ya maana, ambayo haifanani na ile ya Vingunguti, eti mchana msosi wake ni balaa, yani nyama mchanganyiko, na madikodiko, sasa angalia huo wa usiku.

Masela wanakwenda mbali kweli na kuamini kwamba Ulaya, mtu anakuwa na ratiba ya kupumzika na kufanya mazoezi kisha usiku mambo yote kwenye makasino yaliyokwenda shule.

Ajabu masela hawa sikuwasikia wakiyataja masaa ya kufanya kazi, tena katika mazingira magumu kama vile kusafisha kwenye mahospitali yaliyojaa uchafu ambao wazungu hawapendi kuhangaika nayo.

Hawazungumzii shida zile za kodi za nyumba za kutisha, upweke uliokithiri kutokana na kutokuwa na tabia ya kutembeleana na kuweka vijiwe kama hapa Bongo.

Sikusikia yale manyanyaso endapo Mbongo utakuwa ukifanya kibarua chini ya usimamizi wa Mzungu.

Wala hawasemi kazi za dharau za kulisha na kusafisha nyumba za wanyama kama mbwa na farasi na kisha kuambulia visenti vinavyopatikana baada ya kukashfiwa na kubaguliwa kwa dhahiri!

Siyo kweli masela

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles