22.1 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Msiende kuwa na ‘balehe’ ya madaraka- Mtaka

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewaapisha Wakuu wapya wa Wilaya za mkoa huo huku akiwataka kutokuwa na ‘balehe’ ya madaraka.

Wakuu wapya wa wilaya walioapishwa leo Jumanne 22, 2021 ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa, Remidius Mwema na Mkuu wa wilaya ya Kondoa Khamisi Ramadhan Mkanachi .

Juni 19, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa wakuu wapya wa  wilaya ambapo kwa mkoa wa Dodoma alifanya mabadiliko kwa kuwabadilisha vituo vya kazi, Mkuu wa wilaya wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri ambaye amehamia Dodoma Mjini, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Josephat Maganga amabye yeye aliteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa huku, Simon Chacha akibaki Chemba na Mwanaidi Mkunda nae akibaki Bahi.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha, Mtaka amewataka wakuu hao wa wilaya kutokuwa na balehe ya madaraka kwani ni mbaya na itawafanya wasifanikiwe katika mipango yao.

“Unaweza ukafanya vituko hata familia yako ikaona aibu kusema huyu ni ndugu yetu, katika yote hayo epuka sana balehe ya madaraka hizi staili za ukuaji wa binadamu kwenye madaraka zipo epuka sana balehe ya madaraka,”amesema.

Vilevile, Mtaka amewataka wakuu hao kuwa makini na aina ya marafiki ambao watawapata kwani wengi ni feki na wanawafuata sababu ya vyeo vyao.

“Moja ya faida mtakayoipata nyinyi ambaye ni wateuliwa ni kupata watu feki unafanya ujinga anasema jembe letu hakuna kama wewe na uzuri wa madaraka unapata marafiki feki. Jitahidi umenteni uhalisia mimi namba yangu ya simu ndio nilitumia tangu naanza kumiliki simu. Kwa hiyo nimementaini simu yangu moja kwa sababu nimeona viongozi wengi akiombwa simu anasema anaomba inayopatikana.

“Sisi marafiki wa majina tunakwambia ukweli ila marafiki wa vyeo vyetu hawezi kutuambia ukweli. Nimentaini marafiki zangu wale wa cheo nimeaacha Simiyu na wale wa jina bado nipo nao mpaka leo meseji yangu hapa ni kwamba acheni na epukeni balehe ya madaraka,” amesema Mtaka.

Pia amewataka wakuu hao kumpa fahari aliyewateua (Rais Samia) kwa kuchapa kazi ambazo zitaoneka kwa wengi kama ilivyokuwa yeye wakati akiwa mkuu wa mkoa wa Simiyu.

Aidha, amesema wakuu wa mikoa sio wasaidizi wake kwani wao wanawajibika moja kwa moja kwa Rais hivyo kila mmoja atimize wajibu wake kumsaidia Rais.

Pia, Mtaka amewataka kusimamia elimu kwani kwa sasa hali hairidhishi katika maeneo mengi ya mkoa wa Dodoma.

“Nendeni mkasimamie elimu pale Mpwapwa Kata 11 hazina shule, mimi kipaumbele changu ni elimu na hapa kwenye elimu kuna shida lakini pia nendeni mkayaweke vizuri mahusiano, ukiitwa nenda ili ukiita na wao waje hasa kwa viongozi wa dini,”amesema Mtaka.

Kwa upande wake, Mkuu mpya wa Wilaya ya Kongwa, Mwema amemshukuru rais kwa kumteua kama kijana kushika wadhfa huo ambapo amesema atalipa fadhila kwa kufanya kazi kwa bidii ili maono na matarajio aliyoahidi rais yatimie.

“Ninaahidi ushirikiano nashukuru kwa viongozi wenzangu ninahitaji sana ushirikiano na mimi nitatoa ushirikiano kazi yangu kwenda kutekeleza imani ambayo Rais ameionesha kwangu kama kijana kazi yangu kuhakikisha yale aliyoaahidi, matarajio na mategemeo kwenda kuyatekeleza katika wilaya ya Kongwa,”amesema.

Nae, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mkadachi amesema ameteuliwa kuwa mtumishi na sio mtawala hivyo anaenda kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na maelekezo ambayo yametolewa na Mtaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles