27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Msichana anayehitaji malezi anapolazimika kulea

Christian Bwaya

PAMOJA na faida zake, maendeleo yanaweza kubadili kwa kiasi kikubwa mfumo wa malezi uliozoeleka. Kwanza kabisa, majukumu ya kijinsia yaliyozoeleka katika jamii yanabadilika. Mama aliyezoeleka kuwa mlezi anapoingia kwenye soko la ajira, anaacha nyumbani swali gumu: Nani atabaki na mtoto yeye akiwa kazini?

Swali hili ni gumu kwa sababu hata ule utamaduni wa familia tandao nao umeanza kupotea. Shauri ya maendeleo, uwezekano wa ndugu kama shangazi, mama mdogo, wifi, shemeji, binadamu kukaa pamoja unakuwa mdogo na hivyo ule msaada uliozoeleka unakosekana. Matokeo yake inabidi sasa wazazi ambao kwa kawaida wanahitaji kuendelea na shughuli za uzalishaji watafute malezi mbadala. Mojawapo wa mbadala huo ni binti wa kazi maarufu ‘house girls’.

House girl, kwa kawaida, ni watoto au vijana wadogo waliokulia katika mazingira ya kawaida, mara nyingi kijijini tena bila elimu kubwa, wanaoajiriwa na wazazi kwa lengo la kuwasaidia kumtazama mtoto wakati wa kazi. Sambamba na malezi, wasichana hawa hufanya kazi za ndani.

Walezi hawa hupatikana kwa utaratibu usio rasmi unaotegemea mfumo wa kufahamiana na ndugu, jamaa na marafiki wanaoweza kuwaunganisha wazazi wenye uhitaji na msichana anayetafuta kazi. Hakuna utaratibu rasmi unaowawezesha waajiri wenye uhitaji kuwa na uhakika na historia yake, ujuzi wake pamoja na tabia zake kwa ujumla.

Hata hivyo, hutokea wakati mwingine wakapatikana kupitia kwa watu wanaofahamika. Ingawa utaratibu huu wengine huuchukulia kama namna nyingine ya usafirishaji wa binadamu, lakini umekuwa ukiwasaidia wazazi kuwa na uhakika na wapi hasa watoto hawa wanatoka.

Mara nyingi, mabinti hawa huajiriwa bila mikataba inayoeleweka na hulipwa kiasi kidogo cha fedha. Hata hivyo, nje na malipo ya fedha taslimu, wazazi wengi huwapa marupurupu kama chakula, matibabu na huduma nyingine za msingi.

Ratiba zao za siku hujaa shughuli nyingi zisizolingana na kipato chao. Wengi wao huwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kulala. Waajiri wao huwa na matumaini makubwa kupindukia.

Pamoja na kazi kubwa wanayofanya, yamekuwapo matukio ya wasichana hawa kuonewa na waajiri wao kwa namna mbalimbali. Wapo wanaotendewa kama watumwa wasiostahili heshima kama binadamu wengine. Wengine hunyimwa haki zao za msingi.

Katika mazingira haya, wasichana hawa, wakati mwingine hujenga tabia zisizofaa ambazo huzorotesha uhusiano na waajiri wao.

Hali ya kutokuelewana kati ya mwajiri na mtoto huyu wa kazi husababisha hasira, uchungu na visasi ambavyo mara nyingi huishia kwa mtoto asiye na hatia. Ikumbukwe kuwa wasichana hawa ambao mara nyingi ni watoto, huwa hawana uzoefu na malezi.

Utendaji wa wengi wao hutegemea maelekezo ya kila mara kutoka kwa waajiri wao ambao wakati mwingine ni watu wenye uwezo mdogo kiuchumi lakini wenye matarajio makubwa.

Tunaposikia matukio ya akina dada hawa kuwafundisha watoto tabia zisizofaa, kuwaonea watoto na kuwatendea vitendo visivyofaa, tunaumia kwa sababu tunafahamu waathirika wakuu ni watoto wasio na hatia wanaolelewa na wasichana hawa ambao wakati mwingine huyafanya yote wayafanyayo kulipa kisasi kwa waajiri wasiojali haki zao.

Katika makala ijayo tutatoa mapendekezo matano ya namna tunavyoweza kupunguza changamoto hizi na hivyo kumsaidia mzazi kuwa na amani anapoendelea na shughuli zake za uzalishaji kazini.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles