25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Msiba wa mhariri wagonganisha vichwa vigogo

Na Tunu Nassor -Dar es salaam

MSIBA wa Mhariri wa Gazeti la Jamhuri, marehemu Godfrey Dilunga, jana umegonganisha vichwa vigogo ambao kila mmoja wao alijivutia namna alivyofanya naye kazi.

Dilunga aliagwa viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam jana na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali.

POLEPOLE

Kigogo wa kwanza kueleza namna alivyofanya naye kazi na kumwelezea kwa kina, alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole.

Alisema Dilunga alikuwa miongoni mwa waandishi ambao CCM inawaheshimu kutokana na uwezo wake mkubwa.

Polepole alisema Dilunga ndiye mwandishi wa habari pekee  aliyepata fursa mwaka 2015 kufanya mahojiano na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho, Rais Dk. John Magufuli.

“Huyu ndiye mwandishi pekee ambaye alipata fursa ya kufanya mahojiano na mgombe wa CCM mwaka 2015 (Rais Magufuli). Hii ilikuwa heshima kubwa, alifanya kazi nzuri mno hakika,” alisema.

Polepole alisema chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wake, huku Rais na viongozi wengine wakitoa pole.

“Chama kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo hiki, rais na viongozi wengine wanatoa pole kwa familia na tasnia ya habari.

“Rais Magufuli anawapa pole wote pamoja na viongozi wa juu wa chama kutokana na msiba huu mkubwa.

“Sifa zote zilizoelezwa hapa ni za kweli, hakika alikuwa mwadilifu na mzalendo kwelikweli kwa nchi yake,” alisema Polepole.

Alisema alichojifunza kutoka kwa Dilunga ni ustahimilivu aliokuwa nao kwa kuwa hakuwahi kutumia kalamu yake kumchafua mtu.

“Hata mimi tulipoambiwa tuwaambie majirani zetu kuwa tunawapenda, nilimwambia Zitto nampenda.

“Niwaombe waandishi myaendeleze yote mema aliyokuwa akiyatenda Dilunga, hasa kuwatendea haki wengine,” alisema Polepole.

Alisema Dilunga alikuwa mpenzi wa CCM, licha ya kuwahi kufanya kazi pia na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kauli hiyo ilisababisha watu kucheka, kwani ilianza kama kuleta minong’ono miongoni mwa waombolezaji ambao wengi walisikika wakisema mwakilishi wa Chadema akipewa nafasi atajibu hoja hiyo.

CHADEMA

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alipopewa nafasi ya kutoa salamu za rambirambi, hakusita kumjibu Polepole na kusababisha waombolezaji kuangua vicheko.

Akimzungumzia Dilunga, Mwalimu alisema alikuwa katika timu ya waandishi 12 waliozunguka wakati wa kampeni ya Uchaguzi Mkuu kwa mwaka 2005.

“Tumemtengeneza sisi wakati wa kampeni za mwaka 2015, nasema bado tuna vijana wengi, nimemsikia Polepole akisema alikuwa kwao, alikuja huko akitokea kwetu,” alisema Mwalimu.

Alisema pamoja na madai kwamba Dilunga alikuwa mwandishi wa kwanza nchini kupanda helkopta ya Chadema, yeye ndiye wa kwanza, wakati ametua mjini Bukoba alishuka na kwenda kumsimulia Dilunga namna alivyokuwa na hofu.

“Niliposhuka kwenye helkopta kwa mara ya kwanza pale Bukoba, nilikwenda kumsimulia namna nilivyokuwa na woga na uzanzibari wangu.

 “Lakini pamoja na yote hayo, nasisitiza tunatakiwa kuheshimu uhuru wa habari kwa ustawi wa nchi,” alisema Mwalimu.

Kuhusu wanasiasa wanaposhikana mikono, Mwalimu alisema inapaswa kutoka ndani ya nafsi zao kweli kweli na isiwe unafiki.

“Tukio lililofanyika hapa la kupeana mikono na kumwambia jirani yako nakupenda, ni ujumbe mzito ambao sote tunatakiwa kuuzingatia, usiwe wa unafiki,” alisema Mwalimu.

ZITTO

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, aliwataka waandishi kujenga ushirikiano kwa kuwasaidia wenye shida kabla ya madhara makubwa hayajatokea.

“Nawaomba waandishi kujenga utamaduni wa kuthamini wenzetu wanapokuwa wanakabiliwa na shida mbalimbali,” alisema Zitto.

Alisema waandishi ni wengi, lakini wa aina ya marehemu Dilunga ni wachache kwa kuwa alikuwa akiandika kulingana na taaluma yake.

“Alikuwa akiandika kwa weledi, tunapaswa kutengeneza wahariri wengine wenye weledi kama Dilunga.

“Nalishauri Jukwaa la Wahariri tengenezeni kina Dilunga wa aina hii wengi, ni hazina kubwa katika tasnia ya habari.

“Dilunga alikuwa na msimamo wake mkibishana kwa hoja, mwisho wa siku anakwenda, akiandika maoni anakunyuka kwa hoja bila kukuonea,” alisema.

SUNGURA

Mkurugenzi wa Uhuru Media Group, Ernest Sungura, ambaye aliwasilisha salamu za Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, alisema tasnia ya habari imepata msiba mzito.

Akimnukuu Dk. Bashiru, alisema atamkumbuka Dilunga tangu kuanzishwa kwa Kigoda cha Mwalimu, Kavazi la Mwalimu na mchakato wa Katiba mpya.

“Alifanya naye mahojiano ya kina kwa saa mbili na kuandika makala nzuri iliyosheheni ukweli,” alisema Sungura.

Alisema Dk. Bashiru ataendelea kumuenzi Dilunga kupitia kazi zake alizowahi kufanya naye na kuziripoti kwa weledi.

TEF  

Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena, alisema jukwaa hilo limempoteza mwanachama wake aliyejiunga tangu mwaka 2010.

Alisema Dilunga atakumbukwa na waandishi wenzake na jamii kwa ujumla kutokana na uhodari wake wa kutafuta habari.

“Niliposikia amelazwa, nilienda kumwona, akamwambia mkewe huu ni ugeni mkubwa na kuniambia ‘katibu umeona nilivyotikiswa’, nami nikamtia moyo kuwa atapona,” alisema Meena.

MEMBE

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alitaka vyombo vya habari kuwa na uhuru wa kutosha.

Alisema ustawi wa uhuru wa vyombo vya habari ndiyo ustawi wa nchi ili istawi, hakuna budi kuhakikisha kunakuwapo na uhuru wa vyombo vya habari.

Membe alisema uhuru huo ni sawa na mbolea katika ustawi wa taifa, kinyume chake nchi hudumaa.

“Kifo hiki kitukumbushe kitu kimoja, kitukumbushe uhuru wa vyombo vya habari ni sawa na mbolea inayowekwa kwenye mche ili uchipue vizuri na kuzaa matunda,” alisema Membe.

Alisema ni jukumu la kila mtu kuhakikisha kunakuwa na uhuru wa vyombo vya habari.

Membe alisema vyombo hivyo ndivyo vinavyotoa afya kwa Serikali kutokana na kuibua mambo mbalimbali yaliyojificha katika jamii na ikitokea vimedumaa huzorotesha maendeleo ya nchi.

“Naomba waandishi tuwe huru kuzungumza ukweli na kuibua mazito yaliyojificha ili nchi hii iweze kusonga mbele,” alisema Membe.

Kuhusu marehemu Dilunga, Membe alisema nchi imempoteza shujaa kwa kuwa alikuwa ni mwenye kujitoa na kuheshimu kazi yake.

“Alikuwa huru na mzalendo aliyeandika kile alichokiamini kwa maendeleo ya nchi yake, hivyo namwita shujaa,” alisema Membe.

MWAKYEMBE

Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema amepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa.

 “Nilikuwa kwenye ufunguzi wa mafunzo ya waandishi wa habari, nikatizama sikumwona Dilunga, nikamwambia msaidizi wangu ampigie, nikaambiwa anaumwa yupo wodini,” alisema Mwakyembe.

Alisema Dilunga amefariki akiwa na umri mdogo wa miaka 43, akiwa bado jamii na nchi ikimhitaji zaidi.

TAMWA

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Wanawake (Tamwa), Joyce Shebe, alisema Dilunga alikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Tulikuwa tunapambana na mtoto wa kike pekee, sasa hadi watoto wa kiume nao wananyanyaswa kwa kulawitiwa jambo linalomhitaji Dilunga kuandika, hatuko naye sasa,” alisema Joyce.

MISA TAN

 Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari vya Kusini mwa Afrika (MisaTan), James Marenga, alisema Dilunga alikuwa anaandika kwa uchunguzi wa ndani wa habari hasa katika makala.

“Niwaombe wahariri kuzikusanya makala alizokuwa akiandika, hasa za kuigusa jamii ili wengine waweze kujifunza kupitia makala hizo,” alisema Marenga.

WAANDISHI HABARI ZA BUNGE

Kwa niaba ya waandishi wa habari za Bunge, mmoja wa wandishi hao, Hamis Mkotya, alisema Dilunga alikuwa ni mwandishi anayezingatia kanuni za uandishi wa Bunge.

Alisema habari za Bunge zimetengenezewa kanuni maalumu namba 140 na Dilunga alikuwa akitembea nazo.

“Hajawahi kulalamikiwa katika habari zake kuwa ameigombanisha Serikali na wananchi wake, hii ni sifa aliyokuwa nayo,” alisema Mkotya.

WASIFU WA MAREHEMU

Akizungumzia wasifu wa marehemu, Mhariri Mkuu wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balille, alisema Dilunga alijiunga na kampuni yao Januari, mwaka huu akitokea gazeti la Raia Mwema.

Alisema awali alikuwa akifanya kazi Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na alikuwa akifanya kazi na vyama vyote vya siasa.

Mwili wa marehemu Dilunga ulisafirishwa jana kwenda mkoani Morogoro kwa mazishi ambayo yanatarajia kufanyika leo eneo la Bigwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles