25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MSHTUKO ZAIDI AJALI YA WANAFUNZI

Na WAANDISHI WETU

-ARUSHA

NI mshituko zaidi. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya ajali ya basi kusababisha vifo vya wanafunzi 33 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya mjini Arusha. Ajali hiyo iliyotokea juzi saa 3 asubuhi.

Mbali na wanafunzi hao 33, walimu wawili na dereva   wa basi   ya Mitsubishi Rossa namba T. 871 BYS, walifariki dunia   baada ya gari hilo kutumbukia kwenye korongo eneo la Marera, Rothia wilayani Karatu.

Ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi  na walimu wao walipokuwa wakienda  wilayani Karatu kufanya mtihani wa ujirani mwema (joint examinations) na wanafunzi wenzao wa Shule ya Tumaini Junior School.

Katika matokeo ya mwaka jana ya darasa la saba, shule hiyo ya Lucky Vincent ilishika nafasi ya pili kwa mkoa.

MTANZANIA ilizungumza na wazazi, walezi waliopoteza watoto wao.

 Mosses Kivuyo,   ni baba wa Irene ambaye ni miongoni mwa wanafunzi 33 waliofariki dunia  katika ajali hiyo, alisema  alifanikiwa kulifikia gari la wagonjwa (Ambulance) na kushuhudia mtoto wake Irene akikata roho.

Alisema mtoto wake akiwa na majeraha makubwa yaliyoambatana na maumivu makali, alitoa namba ya simu akiomba apigiwe simu kujulishwa kwamba motto wake alikuwa amepata ajali akiwa katika safari ya  masomo.

“Niliposikia taarifa nilienda shuleni nikitokea nyumbani Kwa Mrombo… nikaamua kwenda eneo la tukio lakini baadaye nilipigiwa simu kwamba hali ya mwanangu   si nzuri, yuko katika Hospitali ya Lutheran Karatu.

“Na mtoto ndiye alitoa namba ili nijulishwe kuwa anafanyiwa upasuaji kwa sababu  alikuwa ameumia kichwa na mdomo.

 “Nilifika hospitalini nikakuta mtoto anapandishwa katika ambulance ili apelekwe Arusha lakini kabla gari halijaondoka, mtoto alikata roho nikimuona… hakuweza kuzungumza chochote ingawa ndiye alitoa namba yangu ya  simu,” alisema Kivuyo kwa masikitiko makubwa.

Alisema binti yake Irene alikuwa wa kwanza kuzaliwa katika watoto wake watatu na alikuwa akilala bwenini shuleni hapo.

 

BABA WA NTEGEAJE

Naye Augustine Amos ambaye ni baba mzazi wa mwanafunzi Ntegeaje Amos, alisema amepoteza mtoto wake ambaye alikuwa mtulivu na aliyependa kusoma.

“Alikuwa kijana mtulivu, nilimtegemea nyumbani… ndoto zake zilikiwa kusoma kwa bidii ili awe daktari. Kwa  bahati mbaya zimezimika gafla akiwa safarini kuzipigania ndoto zake,” alisema Augutine.

Akielezea zaidi, Augustine anayefanya kazi Benki ya TPB mkoani Manyara, alisema alizungumza na mtoto wake Alhamisi  iliyopita.

“Mama yake alimuandaa Jumamosi kwa safari ya masomo na alimsindikiza mpaka shuleni saa 11 alfajiri. Lakini ndiyo hivyo tena yaliyotokea,” alisema Augustine.

 

Baba wa Praise Mwaliambi

Baba Mzazi wa mwanafunzi Praise (14), Rolland Mwaliambi, akielezea alivyopokea taarifa za kifo cha mtoto wake, alisema  taarifa za kifo cha mwanae alizipata akiwa Dar es Salaam kwa shughuli za  kazi.

Alisema akiwa katika kikao baada ya kupigiwa simu kutoka nyumbani na alifuatilia taarifa hizo na akajiridhisha mwanaye alikuwa amefariki dunia.

“Bahati nzuri wafanyakazi wenzagu walifanya utaratibu nikaondoka na ndege ya Coastal, hivyo nikawahi kufika mapema Arusha kuungana na familia.

“Hali ilikuwa mbaya, mke wangu hakuweza kulipokea kwa urahisi jambo hili ilikuwa ngumu kwake, taratibu tunajaribu kurudi kwenye hali ya kawaida, mwanangu alikuwa darasa la saba akielekea Karatu kufanya mitihani.

Akimuelezea mtoto wake huyo, Mwaliambi alisema tayari alikwisha kuanza kujitambua na kujua anatakiwa kufanya nini anapokuwa shuleni na hasa katika masomo yake.

“Praise alijitambua mapema kwamba anahitaji kusoma na kufaulu.  Alikuwa na malengo ya kufika Chuo Kikuu. Lakini alipendelea kusoma na kuwa Padri, hii ni kwa sababu alilelewa maisha ya kanisani na alienda kutumikia kanisani Parokia ya Utatu Mtakatifu.

“Na wakati nikipata taarifa za kifo chake tayari tulishachukua fomu za kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza Seminari ya Maua…  Juni mwaka huu alikuwa anaenda kufanya mitihani wya majaribio.

“Lilikuwa hitaji lake kubwa kusoma seminari, ndoto zimeishia hapo hata jana wakati akapoteza maisha.  Kaka yake alikuwa hapa Arusha kuleta fomu   zijazwe na walimu wa Lucky Vincent,” alisema mzazi huyo.

 

Mama wa Doreen Aloyce

  Neema Mshana, mama wa mwanafunzi Doreen Aloyce, anayeendelea kupatiwa matibabu  katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU)  kutokana kuvunjika paja, mkono na shingo, alisema anaendelea kumuombea mtoto wake apone haraka.

“Mwanangu yupo ICU, naamini Mungu atampigania apone haraka,” alisema Mshana.

 

MEYA WA JIJI

Akizungumza   shuleni hapo jana Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro (Chadema),  alisema  huzuni kubwa imeendelea kutanda kwa wazazi, walezi na wananchi hasa ikichukuliwa ni tukio lililoshtua watu wengine.

“Huu ni mshtuko mkubwa kwa wananchi, kwa sasa waombelezaji wote tumekutana shuleni hapa kwa ajili ya kufahamishana taratibu za kuaga miili kesho (leo).

“Na baada ya taratibu hizo, kesho kila familia itaangalia namna ya kuendelea na utaratibu wake kuwasitiri wapendwa wetu, na sisi viongozi tutahakikisha tunashiriki kwa ukamilifu,” alisema Meya.

 

SHULE YA FUNGWA

Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Longino Vincent aliwatangazia wazazi waliokusanyika shuleni  hapo jana jioni kuwa uongozi wa shule hiyo umelazimika kuifunga   kwa siku saba.

“Kuanzia kesho mpaka Jumatatu ijayo tutafunga shule, tunaomba taarifa hii mtusaidie kuisambaza, ila darasa la saba waliopo na darasa la sita tutawaomba waje uwanjani kuwaaga wenzao …ni kwa darasa la sita na saba pekee,” alisema Mwalimu Vincent.

 

Uozefu wa dereva

Akifafanua kuhusu dereva wa gari lililokuwa limebeba watoto hao,   Mwalimu huyo alisema dereva Desmass Kessy aliajiriwa shuleni hapo   miaka minne iliyopita.

“Marehemu alikuwa mzoefu wa kazi yake na alikuwa na leseni inayomruhusu kuendesha aina gari alilopata nalo ajali, lakini pia kabla hawajaondoka kuelekea Karatu magari yote matatu yalifanyiwa ukaguzi maalumu,” alisema Mwalimu Vincent.

 

LEMA MBUNGE

Mbunge wa   Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akizungumza shuleni hapo jana akiwa ametokea  Dodoma, alisema  msiba huo   unahitaji kufundisha namna ya kurekebisha baadhi ya mambo.

“Jumanne ni siku ambayo nasoma hotuba yangu kama Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani bungeni,  nitahakikisha mambo hayo nayaweka kwenye hotuba,” alisema Lema.

Mbunge huyo pia aliwaonya watu wanaotaka kuutumia msiba huo kwa lengo la  siasa,   wahakikishe wanatoa pole kwa kuwafariji wafiwa.

“Kufiwa na mtoto aliyekuwa darasa la saba akijiandaa kuanza kidato cha kwanza… kwa wazazi wake wanahitaji busara za viongozi kuliko mbwembwe za viongozi,” alisema Lema.

 

MAKAMU WA RAIS AWASILI ARUSHA

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, jana jioni aliwasili  i Arusha ambako leo ataongoza wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili   na dereva   wa shule ya Lucky Visent, waliofariki dunia ajalini.

 Ibada na dua za kuaga miili ya marehemu hao itafanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuanzia saa 2.00

asubuhi.

 

WAZIRI WA ELIMU

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Professa Joyce Ndalichako, aliwasili shuleni hapo jana jioni na kutoa pole kwa wazazi, walimu na walezi waliokuwa wamekusanyika.

  Profesa Ndalichako alisema alipokea taarifa za tukio hilo la ajali na vifo hivyo kwa masikitiko makubwa.

“Niungane na Rais Dk. John Magufuli kutoa pole   kwa familia na ndugu walimu na uongozi wa ashule…tuendelee kuvuta subira na kuwa na moyo wa utulivu utakaotuwezesha kukubali jambo hili ambalo limepoteza viongozi wetu wakiwamo madaktari na walimu.

“Huu ni msiba mzito sana, tunatambua watoto hawa walikuwa ni hazina ya taifa ya kesho.  Kazi ya Mwenyezi Mungu haina makosa, Mungu atutie nguvu na faraja pekee ndiyo inayoweza kutoka kwake… serikali iko pamoja na nyie na kufanikisha mazishi ya watoto hawa na wapenzi wetu,” alisema Prof. Ndalichako

 

Mbunge Bashe

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), aliwapa pole, wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ajali hiyo iliyotokea juzi. 

“Hakika ni simanzi kubwa na huzuni sana, jambo hili limegusa sana mioyo yetu na hisia za kila mtu duniani kote… nasi kama wazazi na ndugu tunaumia na kuomboleza pamoja na wafiwa wote,”alisema Bashe.

Alisema taifa limeondokewa na hazina kubwa ya viongozi na wataalamu wa Tanzania ya kesho hivyo mioyo inaumizwa zaidi watoto wanapozimika ghafla.

“Ni maombi yangu kuwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema atawarehemu watoto wote na kuwalaza mahali pema peponi, Amen,”

Pia alimpa pole Rais John  Magufuli, Waziri wa Elimu Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa Arusha, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini  na  Mkuu wa Shule ya Lucky Vicent  na wazazi wote walioondokewa na watoto wetu wapendwa.

 

NCCR mageuzi   

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Magaeuzi, James  Mbatia,  kwa niaba ya chama chake alisema wamepokea kwa masikitiko msiba wa wanafunzi hao na anaungana na familia ya wafiwa katika kuomboleza msiba.

Katika taarifa yakei jana alieleza kwamba chama hicho kinatoa pole kwa uongozi, walimu na wanafunzi wa Shule ya  Lucky Vincent ya Arusha kutokana na msiba huo mzito uliowapoteza wanafunzi wa darasa la saba 32, walimu wao wawili (2) na dereva wa gari hilo.

“Kwa msiba huu tunaungana kwa hali zote kama watoto wa mama Tanzania, kwa sababu  ni mama Tanzania iliyopoteza viongozi na watalaamu wajao wa masuala mbalimbali,” ilieleza taarifa hiyo.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alisema kama taifa, msiba huo ni pigo kubwa na hautaweza kusahaulika kwa namna yoyote ile.

“Chama cha NCCR-Mageuzi kinawaasa Watanzania wote wanaotumia barabara  kuwa makini katika kipindi hiki cha mvua  na kuzingatia sheria na alama za barabarani,”ilisema taarifa hiyo.

 

CCM

Wakati huohuo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimepokea kwa mshtuko na huzuni ajali na vifo vya wanafunzi walimu wa shule ya msingi Lucky Vicent ya Arusha.

Taarifa ya  chama hicho iliyosainiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humprey Polepole, ilieleza kuwa  CCM inatambua  safari  hiyo ilikuwa ni sehemu ya kuimarisha  taaluma ili kutimiza ndoto zao maisha.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana pia anawapa pole wote walioguswa na msiba huo.

 

CHADEMA WANAWAKE

Baraza la Wanawake  la Chama cha Demokrasia  na Maendeleo (Chadema) limesema limepokea kwa mshtuko na uchungu  wa vifo vya wanafunzi wa shule ya Lucky Vicent .

Taarifa ya Mwenyekiti wa Baraza hilo , Halima Mdee inaeleza kuwa Bawacha imeshtushwa na tukio hilo ililolieleza kuwa ni gumu katika historia ya nchi.

“Tumeshtushwa na tukio hili gumu katika historia ya nchi yetu bali pia taifa linalia na kina mama wote waliopoteza  watoto wao katika ajali hii mbaya.

“Kwetu sisi vifo vya watoto hawa vimetupa wakati mgumu hasa tukijikumbusha msemo usemao, ‘Uchungu wa mwana aujuaye mzazi,’’ alieleza Halima.

 

MSIBA WAVUKA MIPAKA

Kutokana na msiba huo mkubwa kwa taifa, juzi, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, aliwaongoza wafuasi wa muungano wa Jubilei kuombeleza kwa dakika tatu msiba huo wa wanafunzi waliofariki mkoani Arusha.

Vilevile  Parokia ya Immaculate   mjini Moscow,  Urusi nayo iliwaombea  marehemu hao katika ibada ya Jumapili, ili Mwenyezi Mungu awape pumziko la milele na amani.

 

Habari hii imeandaliwa na ELIYA MBONEA, ABRAHAM GWANDU,   JANETH MUSHI, Arusha , na mitandao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles