27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Mshtuko wa figo hatari

*Utafiti wabaini asilimia 50 ya watoto wapoteza uhai

TUNU NASSOR Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa na jopo la madaktari bingwa wa figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umebaini asilimia 30 ya watoto wachanga 380 waliokuwa wamelazwa walipata ugonjwa wa mshtuko wa figo.

Akizungumza na MTANZANIA hospitalini hapo jana, daktari bingwa wa magonjwa ya figo kwa watoto, Dk. Francis Furia, alisema utafiti huo ulifanyika kati ya mwaka juzi na mwaka jana.

Alisema kati ya watoto waliogundulika kuwa na mshtuko wa figo, asilimia 50 walifariki dunia.

“Kwa sasa kliniki ya figo kwa watoto inayofanyika mara moja kwa wiki, tunawahudumia wagonjwa kati ya 16 hadi 20,” alisema Dk. Furia.

Alisema sababu za kupata magonjwa ya figo kwa watoto ni pamoja na kuugua malaria, dengue, homa ya ini, kuhara, kipindupindu, kupata maambukizi ya bakteria na tatizo la kupumua.

Aliongeza kuwa baadhi ya dawa zinazotumika kutibu magonjwa mbalimbali zimekuwa zikisababisha kupata ugonjwa huo.

“Dawa kama ‘Gentamicin’, ‘Diclofenac’ na ‘Movera’ zimekuwa zikichangia kuongezeka kwa ugonjwa wa figo kwa watoto,” alisema Dk. Furia.

Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni upungufu wa damu, kuvimba uso na tumbo, kiungulia, shinikizo la juu la damu na kushindwa kutoa haja ndogo.

“Niwashauri wazazi wanapoona dalili hizo kwa mtoto wawahi hospitali kupata matibabu ili kuepuka ugonjwa huo kuwa sugu,” alisema Dk. Furia.

Aliongeza watoto wanapougua magonjwa yanayoweza kusababisha ugonjwa wa figo, wawahi hospitali kupata matibabu sahihi na kwa wakati.

“Wazazi waache tabia ya kuwapa watoto dawa za miti shamba ambazo hazijafanyiwa utafiti, kwani zinaweza kuhatarisha afya ya mtoto na kumsababishia ugonjwa wa figo,” alisema Dk. Furia.

Aliwataka wazazi kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya katika malezi ya watoto, ikiwa ni pamoja na kuwapa dawa bila maelekezo ya daktari.

“Niwaombe wazazi kutokuwapa watoto dawa ambazo hawazijui kwani inaweza kuhatarisha figo,” alisema Dk. Furia.

Mmoja wa wazazi waliowaleta watoto katika kliniki hiyo, Sara Mjema, aliiomba Serikali kupeleka huduma ya madaktari bingwa katika maeneo ya pembezoni.

“Wananchi wengi hawana elimu ya ugonjwa huu, hivyo naishauri Serikali kuwekeza nguvu katika utoaji wa elimu, hasa maeneo ya vijijini ili waweze kuepuka ugonjwa wa figo,” alisema Sara.

Aliongeza kuwa ni vyema kutumia vyakula vya asili katika milo yao kwani katika vitabu vya Mungu inahimizwa hivyo.

DALILI NA UTAMBUZI WAKE

Kwa mujibu wa mtandao wa Kidney Education, inaelezwa kuwa ugonjwa sugu wa figo, ni kwamba figo hushindwa kufanya kazi polepole, kwa miezi hata miaka, kwa hiyo mwili huzoea hatari za hali hii.

Pia, figo huwa na uwezo mkubwa wa kujisaidia katika shida ya kazi zake kwa sababu watu walio na ugonjwa huu usiopona, huwa hawana dalili zozote hadi wakati figo zimeharibika sana.

Figo huwa na kazi nyingi sana kama kutoa uchafu na maji kwenye mwili, kuzuia shinikizo la damu, kusawazisha kemikali mwilini, uzalishaji wa chembechembe za damu nyekundu mwilini na kadhalika.

Hivyo kutegemea matatizo yaliyoko kwenye figo, dalili huwa tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine.

DALILI ZA UGONJWA SUGU WA FIGO

Inaelezwa kuwa dalili hutofautiana kulingana na kiwango cha ugonjwa.

Ili kuelewa vyema na kukabiliana na hali hii vizuri, ugonjwa wa figo umegawanywa katika viwango vitano kulingana na kiasi cha utoaji uchafu kwenye figo (Glomerular Filtration Rate- GFR), ambacho ndio kiwango cha kuonyesha jinsi figo zinavyochuja uchafu kutoka kwenye damu. GFR uhesabiwa kulingana na kiasi cha ‘creatinini’ katika kipimo cha damu.

Kipimo cha GFR ni sahihi cha kuonyesha utendaji wa figo; Utendaji mzuri wa figo ni wakati GFR ni zaidi ya mililita tisini kwa kila dakika (90 ml/min).

HATUA YA KWANZA YA UGONJWA WA FIGO

Inaelezwa kwamba kazi ya figo ikiwa asilimia 90-100, hiyo ni hatua ya mapema ya ugonjwa huu na figo huwa hazijadhurika. Umajimaji (serum creatinini) kwenye damu huwa uko katika kiwango cha kawaida.

Katika hatua hii ya kwanza ya CKD, tatizo linaweza tu kujulikana mtu anapofanyiwa uchunguzi wa kimatibabu au anapopimwa kwa ugonjwa mwingine.

Ishara za hali hii zinaweza kukosekana. Kwa mfano, kuwepo kwa protini kwenye mkojo, sura ya figo kuonekana zimebadilika kwenye picha za X-ray, ultrasound, MRI au CT ma historia ya familia yenye ugonjwa wa uvimbe wa figo (polycystic kidney).

HATUA YA PILI YA UGONJWA WA FIGO

Hatua hiyo huifanya figo isidhurike kidogo, ambapo wagonjwa wanaweza kuwa hawana dalili, lakini ishara zinaweza kuwa ni kukojoa mara nyingi, hasa usiku, shinikizo la damu kuwa juu, mkojo usio wa kawaida na creatinini kwenye damu inaweza kuwa juu (au hata kawaida).

ISHARA KUU ZA UGONJWA WA FIGO

Kwa mujibu wa mtandao wa Kidney Education, dalili za ugonjwa figo ni pamoja na kukosa hamu ya chakula, kichefuchefu na kutapika.

Nyingine ni kuwa dhaifu, mwili kuchoka na kupungua uzito, kuimba miguu, mikono au na usoni karibu na macho pamoja na  shinikizo la damu lisilozuilika, hasa kwa umri mdogo.

Kukosa nguvu kunakosababishwa na upungufu wa damu mwilini (anaemia), hali inayosababishwa na figo kutotengeneza homoni ya erithropoyetini inayosaidia kutengeneza chembechembe za damu.

Kushindwa kulala, kizunguzungu na kushindwa kuwa makini, kujikuna, mkakamao wa misuli, kuhisi uchovu kwenye miguu na kushindwa kufikiria kitu kwa makini.

Maumivu mgongoni hasa chini ya mbavu pamoja na kuhisi kutaka kukojoa mara kwa mara, hasa wakati wa usiku (nocturia).

Maumivu, urahisi wa kuvunjikavunjika mifupa kwa watu wazima na watoto kutokukua kwa sababu ya upungufu wa vitamini D inayotengenezwa na figo.

Kukosa hamu ya kufanya mapenzi kwa wanaume na kukosa hedhi kwa mwanamke  na pia ugonjwa wa figo huhusishwa na ongezeko la vifo vinavyotokana na ugonjwa wa moyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles