26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

MSHINDI WA KWANZA: MAOMBI YALIKUWA SILAHA YANGU

Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

MWANAFUNZI aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana, Alfred Shauri, amesema siri ya mafanikio yake ni maombi na juhudi za kusoma sana.

Shauri ambaye amemaliza katika Shule ya Feza Boys, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na MTANZANIA baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo ya kidato cha nne.

“Nilimwomba Mungu nifanye vizuri na kufanya vizuri ilikuwa moja ya ndoto zangu. Zaidi kilichosababisha nifanye vizuri ni kujiamini, kujituma na kumwomba Mungu,” alisema

Shauri alitoa ushauri kwa wanafunzi wenzake ambao bado wanaendelea na masomo wahakikishe wanajituma na kumwomba Mungu wakati wote.

“Kujituma na kumwomba Mungu vingine vyote vilivyobaki vinakuja kama ziada,” alisema Shauri.

Mama Alfred naye anena

Naye mama mzazi wa mwanafunzi huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Adela Shauri alisema anamshukuru Mungu pamoja na walimu waliomfundisha mtoto wake.

Akizungumzia siri ya maisha ya mtoto wake, alisema ni mtoto anayempenda Mungu, mwenye upendo na huruma huku akipenda kusaidia wenye shida.

“Leo kanitoa kimasomaso…namshukuru Mungu kwa ajili ya mtoto wangu. Mungu ni mwema, Alfred anampenda sana Mungu, hata leo asubuhi (jana) kaamka kwenda kanisani. Ninawashauri wazazi wenzangu wamtangulize Mungu kwani bila yeye hatuwezi kulea watoto,” alisema Adela ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mlimani.

Alisema wakati wote alikuwa akimuhimiza mtoto wake kusoma tangu akiwa shule ya msingi lakini alipofika darasa la sita alikuwa akijitambua.

“Watoto wangu tangu wakiwa wadogo kulikuwa na time table (ratiba) pale nyumbani jioni wakitoka shule wanakula na kuoga halafu wanaingia darasani palepale nyumbani nikiwapa kazi, halafu nazisahihisha na kama wamekosea wanafanya correction (masahihisho)  lakini walipofika sekondari ndiyo wakawa na timetable (ratiba)  zao wenyewe,” alisema.

Alisema Alfred alipohitimu darasa la saba alipata alama A masomo yote na kupangiwa kwenda Shule ya Sekondari Ilboru iliyopo mkoani Arusha lakini wakampeleka Feza Boys.

“Namshukuru Mungu hata alipokwenda Feza Boys pamoja na kwamba ada ni kubwa lakini alipata punguzo la ada la asilimia 30 kwa sababu alikuwa anafanya vizuri katika masomo yake,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles