23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Msele: Simwelewi Ndugai

MASELE AMTUHUMU MAZITO NDUGAIAGATHA CHARLES naRAMADHAN HASSAN-DAR/DODOMA

SIKU moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kusitisha uwakilishi wa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele, akimtuhumu kwa ukosefu wa nidhamu, mbunge huyo amesema ingawa alimsikiliza Spika lakini hakumwelewa.

Masele aliyasema hayo jana wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari kuhusu hatua yake ya kutakiwa arejee nchini kutoka Afrika Kusini anakohudhuria vikao vya Bunge hilo.

Alipoulizwa anaizungumziaje hatua hiyo ya Ndugai, Masele alijibu: “Nisingependa kuizungumzia kwa sababu nimemsikiliza lakini sikumwelewa.”

Kuhusu kauli yake kuwa wakati Ndugai anamwita arudi nchini na Waziri Mkuu alimpigia simu aendelee na kazi, je, si kwamba anachonganisha mihimili ya dola? Masele alijibu:

“Hapo ilikuwa inazungumziwa nchi ambayo inawakilishwa na Serikali, hivyo Bunge haliwezi kuingilia masuala ya Serikali.

“Ninatimiza majukumu yangu kikamilifu na kwa weledi, ni vyema taarifa zinazosemwa ninafanya mambo ya ovyo ovyo zingeelezwa kinagaubaga ni kitu gani ninafanya kuliko kusema mambo kwa mafumbo. Mimi ni mtu ambaye nina heshima zangu, nina wananchi ninaowaongoza, nina familia, ninastahili kuheshimiwa,” alisema Masele.

Alipoulizwa kilicho nyuma ya jambo hilo, Masele alisema aliunda tume ya kumchunguza Rais wa Bunge la Afrika, Roger Dang, anayetuhumiwa kwa rushwa, matumizi mabaya ya ofisi, undugu pamoja na tuhuma za ngono (kashfa ya kulazimisha wafanyakazi kwa ngono).

“Bunge limeazimia kuunda tume ya kumchunguza, ripoti ilikuwa iwekwe mezani ndani ya Bunge (Bunge la Afrika) jana (juzi) na kujadiliwa. Kwa hiyo huyo Rais kwa kuona kwamba mimi Makamu wa Rais nasimamia na kuongoza Bunge kujadili ripoti hiyo anatambua misimamo yangu, sipendi mambo ya ovyo ovyo, akaamua kumtumia Spika wetu wa nyumbani (Spika Ndugai) ili aweze kuniita haraka nyumbani ili niweze kushindwa kuwepo hapa Afrika Kusini kuongoza vikao ambavyo vingejadili ripoti ya uchunguzi, hiyo ndiyo sababu kubwa,” alisema Masele.

Alipoulizwa iwapo atarejea nyumbani nchini Tanzania, Masele alisema alikuwa njiani.

“Nitarejea nyumbani, niko njiani naelekea nyumbani na nitaripoti kwenye Kamati ya Nidhamu ya Bunge kama nilivyotakiwa na Spika,” alisema Masele.

Alipoulizwa iwapo wakati uchunguzi huo unaendelea, je, Rais wa Bunge la Afrika, Roger Dang, alikuwa amewekwa pembeni, ambapo Masele alikiri alikuwa amepumzishwa.

“Unapochunguzwa, unapofanyika uchunguzi wa kina ‘automatic’ kanuni ya mambo ya maadili ya Umoja wa Afrika inakupasa upishe uchunguzi, kwa hivyo anapopisha yeye uchunguzi, mimi Makamu wa kwanza, kanuni zinatamka ndiye nitakuwa mkuu wa shughuli zote na nitasimamia shughuli zote za uendeshaji wa shughuli za Bunge.

“Kwa hiyo hofu yake ilikuwa kwamba nikikaa mimi kwenye kiti nitahakikisha kwamba yeye anapisha uchunguzi, lakini nataka niseme kwamba Tume ya Uchunguzi imeleta ripoti na amebainika ana kesi ya kujibu kwa uchunguzi wa awali, ana kesi ya kujibu ya unyanyasaji wa kijinsia na hivyo tunalipeleka jambo hili kwa Umoja wa Afrika kuweza kufanya uchunguzi wa kina na kisha kuchukuwa uamuzi utakaokuwa unastahili,” alisema Masele.

Alipoulizwa iwapo hadi wakati huo bado ni Kaimu wa Rais wa Bunge la Afrika, alijibu ndio.

Kuhusu kutii amri ya Spika Ndugai, Masele alisema yeye ni mtiifu, hivyo atatii wito wake na anamheshimu.

Alipoulizwa iwapo kuna uungwaji mkono au wanamtenga kutokana na hayo yaliyotokea, ambapo Masele alijibu:

“Nimekuwa ‘busy’ (tingwa) na kazi, sijaweza kufuatilia wala kuzungumza na watu lakini naamini mtu yeyote mpenda haki ambaye anachukizwa na vitendo viovu ikiwamo unyanyasaji wa kijinsia ya wanawake mahala pa kazi, watoto wa shule na watu wote kwenye jamii zetu ni lazima aniunge mkono kwenye vita hii ambayo napambana nayo,” alisema Masele. 

Juzi Spika Ndugai alitangaza kusitisha uwakilishi wa Mbunge Masele katika Bunge la Afrika hadi Kamati ya Maadili itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Spika Ndugai alisema Masele ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), ana matatizo ya kinidhamu ikiwemo kugonganisha mihimili.

Alisema Masele amekuwa akipeleka maneno ya uongo kwenye ngazi ya juu ya Serikali na kwamba amekuwa akiitwa tangu Jumatatu arejee nchini kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge lakini aligoma.

Alisema mbali na kamati hiyo ya Bunge, Masele pia anasubiriwa na kamati ya chama chake ambayo nayo ina mambo ya kumhoji.

Ndugai alisema alimwandikia barua Rais PAP, Dang, kumweleza juu ya kusitisha kwa muda uwakilishi wa Masele kwenye Bunge hilo ili arudi nyumbani kujibu mambo yanayomhusu.

Jana kwa mara nyingine tena sakata hilo liliibuka bungeni baada ya Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), kutaka apewe ufafanuzi kuhusiana na jambo hilo.

Msigwa ambaye alisimama baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, akitaka kujua kosa linalomsibu Masele.

“Bunge limekuwa likichagua wawakilishi mbalimbali katika maeneo mojawapo ni Wabunge wa Afrika, nilitaka nipewe mwongozo wako kwa sababu Bunge hili ndilo limechagua wawakilishi Wabunge wa PAP.

“Sasa inapotokea Mbunge mwenzetu anakuwa ‘suspended’ (simamishwa) wakati Bunge tuliomchagua hatujajua kosa lake uhalali huo unatoka wapi? Kwa sababu hao watu tunaowachagua kutuwakilisha hawajateuliwa na mtu ni Bunge, tulipiga kura hapa wakatuwakilishe kwenye mabunge mbalimbali.

“Nilitaka kujua hawa wawakilishi wetu wanakuwa ‘suspended vipi? Ili tuone tunawakilisha taifa vipi, maana haya mambo mtu anawakilisha taifa halafu anasimamishwa tu kuna kitu.

“Bila Bunge kujadili na mtu anayeliwakilisha taifa analeta sifa kwa taifa, inatuchafua kama Taifa, nilitaka nipate Bunge linakuwa na nguvu kiasi gani la kuwalinda hawa tunaowachagua kuwakilisha nchi yetu,” aliuliza Msigwa.

Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Chenge, alimtaka Msigwa kuwa na subira kwani mambo bado hayajakaa vizuri.

“Mheshimiwa Msigwa kanuni zetu Waswahili tunasema, tusiwahishe mambo jana (juzi) Mheshimiwa Spika amelisemea hapa na ameelekeza linaenda wapi. Litakapokuja sasa ndio utapata nafasi ya kuyasema hayo na kuuliza usaidiwe. Bado huo mlango haujafungwa uwe na subira,” alisema Chenge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles