29.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

Msekwa atoa sababu mbili kupinga matokeo utafiti wa Twaweza

Na EVANS MAGEGE

SIKU moja baada ya Taasisi ya Twaweza kutoa ripoti ya utafiti inayoonyesha kushuka kwa umaarufu wa Rais Dk. John Magufuli kutoka asilimia 96 mwaka 2016 hadi asilimia 55 mwaka huu. Baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wamekuwa na maoni mbalimbali kuhusu  utafiti huo.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu Spika mustaafu wa Bunge, Pius Msekwa alisema hakubariani na ripoti hiyo ya utafiti wa Twaweza.

Msekwa alitoa sababu mbili kutetea hoja yake ambazo ni kutoamini sampuli iliyotumiwa kufanya utafiti pamoja kupinga sababu ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kuwa ndio chanzo cha kushusha umaarufu wa Rais.

Akitetea hoja yake ya kutoamini sampuli iliyotumiwa kufanya utafiti huo, Msekwa alisema  sampuli hiyo haiakisi mtazamo mzima wa hali nchini nzima ilivyo.

Alisema sampuli ya watu 1,000 haiwezi kutoa uamuzi wa wapigakura wanaokadiriwa kufika milioni 25 sasa.

“ Binafsi siwezi kuikubari ripoti hiyo hata kidogo, watu 1,000 hawawezi kutoa hukumu ya mtazamo wa nchi nzima,” alisema Msekwa.

Akitetea hoja yake ya pili ambayo ni  kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kuwa imeua  upinzani hivyo kutoa mtazamo wa kwamba ndio chanzo cha Rais kupoteza umaarufu alisema sababu hiyo haina ukweli wowote.

Kwanza alihoji kwa kusema kuwa kama  kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kumeua upinzani  kwa nini CCM haiathiriwi?

“ Wanatakiwa wajue kwamba baada ya uchaguzi mkuu, siasa huamia bungeni, huko ndiko ushindani wa hoja zitatakiwa kutumika, nje ya jukwaa hilo ni kusubiri Tume ya Uchaguzi(Nec) kufungua kampeni za uchaguzi,” alisema Msekwa.

Ukiachia mbali maoni ya Msekwa, mtaalamu wa siasa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasi na Maendeleo(Chadema), Profesa Mwesiga Baregu  alisema kuporomoka kwa umaarufu wa Rais kunatoa tafsiri ya kwamba wananchi wameamua kuitisha Serikali yao.

Akitetea hoja yake Profesa Baregu alisema  kushuka kwa umaarufu wa Rais, kunamaanisha kuwa ni ujumbe unapelekwa kwake kwamba mategemeo ya wananchi kwa uongozi  wake hayajatimizwa.

Kwa muktadha huo aliongeza kuwa, kawaida hali ikiendelea kuwa kama ilivyo sasa, anaamini utafiti kama huo ukifanyika mwakani, kwa msingi wa kitakwimu itakuwa rahisi kuchora msitari wa kufanyika tafiti tatu na kuonyesha wazi kuwa umaarufu wa Rais umeporomoka hadi kufikia asilimia 30.

“ Nadhani huo ni ujumbe mkubwa sana sio tu kwa maana ya yeye mwenyewe au kwa CCM kuamini kuwa wanaendelea kukaa madarakani bali wanatakiwa kujitathimini  ni wapi amekosea, ni wapi wamefanya vizuri na sio kufikiri wao  na mipango ya yao ya stiegler’s gorge, Reli ya Standard gauge au ununuzi wa ndege,” alisema Profesa Baregu.

Alikwenda mbali katika kujenga hoja ya kuchambua sababu ya kushuka kwa umaarufu wa Rais, ambapo alisema watu  hawajisikii kuwa wako huru kwa sababu wanahisi  kuwapo mazingira ya kutishwa tishwa .

Aliongeza kwa kusema tafsiri ya demokrasia, watu wanahisi kuwa wamepoteza uhuru wao wa kufanya maamuzi.

Alisema kwamba hisia za wengi zinaona kwamba ushirikishwaji wa jamii katika kutoa maoni au mawazo ya kutatua matatizo yanayoikabiri  umekuwa mdogo na badala yake watu wachache au mmoja ndiye amekuwa muamuzi wa yote.

Alisema kutokana na mtazamo huo, Rais anatakiwa kutafuta namna ya kwenda pamoja na jamii.

“ Kuna msemo wa kiafrika usemao kwamba kama unataka kwenda karibu nenda peke yako, lakini kama unasafari ndefu kama hii ya Rais Magufulia  nenda na wenzako.

“Tunamuona Rais anasafari ndefu lakini anakwenda haraka kuliko wenzake, utamsikia Rais kwa kauli zake akisema mnanikwaza au mnanichelewesha  sasa suala la kujiuliza kukuchelewesha kwani wao ndio wenye shughuli?,” alisema Profesa Baregu.

Akizungumzia vyama vya siasa kushuka alisema kawaida lazima vishuke kwa sababu hamasa ya siasa hapa nchi imepooza.

Akitolea mfano Chadema alisema sio kwamba chama hicho hakina matatizo matatizo,  lakini  chanzo cha matatizo yaliyopo sasa ni  kwa kiasi kikubwa kinatokana na kazi ya Serikali ya kuzima siasa za chama hicho kwa kila njia.

Alisema kwamba kwa sasa kuna viongozi tisa wa juu wa chama hicho wanakabiriwa na kesi mahakamani na kila siku au kila wiki wanatakiwa kufika mahakamani.

Pia aliongeza kuwa kuzuiliwa kwa mikutano ya hadhara nako kumechangia kushusha umaarufu wa vyama katika jamii.

Katika hoja hoja hiyo  alisema kwamba  kwa sasa kuna ombwe  kubwa la idadi watu ambao hawana upande wowote na watu hao wengi wao wanatoka CCM ambao wanajiita CCM wafu.

Akifafanua madai ywa kwamba CCM imeongeza idadi takribani milioni sita tangu Rais Dk. Magufuli aingie madarakani, Profesa Baregu alisema  inawezekana watu wakawa na kadi za chama lakini mioyo yao haiku ndani ya CCM.

Alisema kwamba   inawezekana watu wengi wanatumia kadi za chama hicho kama bima  ili wasije wakazurika  kutokana na mazingira yalivyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji mustaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema matokeo ya utafiti huo hayajamshangaza kwani aliyatarajia.

Bisimba alisema mwanzo wa utawala wa Rais John Magufuli ulipokelewa kwa kishindo lakini baadaye watu hawakupata walichokitarajia.

“Sishangai sana matokeo hayo kwani mwanzo wa utawala wa Magufuli ulipokelewa kwa kishindo watu wakimuona kama mkombozi wa dhiki zao.  Siku mia moja za Magufuli, ITV walirusha kipindi walichohoji watu. Kila aliyehojiwa alieleza kuwa anamkubali na wengi walisema ‘pamoja na kuwa sikumchagua ninamfurahia utendaji wake’,”.

“Hasa walivutiwa na kuondoa sherehe za Uhuru kufanya usafi, kuzuia safari za watendaji serikalini, kutamka masuala ya kushughulikia mafisadi. Muda unavyokwenda kuna vitu watu wanategemea hawavioni,” alisema Bisimba.

Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Dk. Azaveli Lwaitama  alionyesha wasiwasi wa utafiti huo kuhusu kigezo cha sampuli na historia ya taasisi yenyewe ya utafiti ambayo siku za nyuma ilionekana kuibeba CCM.

Pamoja na kuonyesha wasiwasi huo lakini Dk. Lwaitama alisema sio jambo la kupuuza matokeo ya utafiti huo.

Alijenga hoja yake kwa kusema suala la uchumi limebeba mambo yote kuhusu Rais Dk. Magufuli. Akifafanua hoja yake alisema awali watu wengi walijenga matumaini makubwa kuhusu Rais, wakati yeye akifanya mambo mengi makubwa ambayo hayawaongezei kipato wananchi.

Alisema Rais, anafanya mambo makubwa sana  ambayo faida yake haiwezi kuoneka kwa watu sasa, hivyo mazingira hayo yamepoteza matumaini ya wengi ambao kiuhalisia hali ya uchumi mifukoni mwao ni hoi.

“ Kuna mambo makubwa anayafanya Magufuli , mfano ununuzi wa ndege, mradi wa  Stiegler’s gorge pamoja na  Reli ya Standard gauge, haya mambo faida yake sio ya leo au kesho. Sasa kwa mtu aliyekuwa na matumaini kwake Rais wakati anaingia madarakani atamuungaje mkono sasa wakati mwenyewe ananjaa?, uchumi umempiga mifukoni na hana jinsi kama alizoea kula milo mitatu kwa siku  sasa anakula mmoja tena kwa kusuasua? Kwa msingi huo lazima umaarufu wake Rais upungue,” alisema Dk. Lwaitama.

Aliongeza kwamba ndani ya CCM kwenyewe hakukaliki, baada ya ripoti ya uchunguzi wa mali za chama watu hawajui mustakabari wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,587FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles