25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MSALABA MWEKUNDU WATAJA SABABU WATU KUFARIKI DUNIA

Na CHRISTINA GAULUHANGA – DAR ES SALAAM


CHAMA Cha Msalaba  Mwekundu Tanzania (TRCS), kimesema watu wengi nchini hufariki dunia kwa sababu ya kukosa huduma ya kwanza.

Akizungumza   na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TRCS, Julius Kejo alisema kuna umuhimu wa chama hicho kuwezeshwa  kujenga wigo mpana nchini utakaosaidia kuokoa jamii   panapotokea majanga ya moto na ajali pia.

Alisema hakuna nchi yoyote itakayoona uchungu kwa kuondokewa na wananchi kwa sababu ya huduma hafifu hivyo ni vema wadau mbalimbali wakajitokeza  kuunga mkono jitihada zinazofanywa na chama hicho kuokoa maisha ya watu.

“Hakuna atakayeona uchungu zaidi ya sisi wenyewe hivyo ni muda muafaka sasa kwetu kujiunga na Chama cha Msalaba Mwekundu pamoja na kukiwezesha kiweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Kejo.

Alisema chama hicho kimejiwekea mikakati mbalimbali ya kuwafikia watu na jamii nyakati zote katika hali mbalimbali bila ubaguzi.

Alisema chama hicho kilianzishwa chini ya sheria Namba 71 ya Bunge ya Desemba mwaka 1962 ambako hadi sasa ina miaka 52   nchini.

“Pamoja na changamoto mbalimbali zinazokikabili chama hiki ikiwa ukosefu wa rasilimali za kutosha hata hivyo kimefanikiwa kutoa huduma mbalimbali kwa watanzania na wageni wakiwamo wakimbizi waliopo katika kambi za Nyarugusu, Mtendeli na Nduta mkoani Kigoma katika wilaya za Kasulu na Kibondo,”  alisema Kejo.

Meneja Maendeleo ya chama hicho, Rhobi Wambura alisema wamekuwa mstari wa mbele kutoa huduma wakati wa maafa mbalimbali ikiwamo mafuriko, njaa, tetemeko, ajali za nchi kavu na majini na  mlipuko wa mabomu.

“Watanzania wamepatiwa mafunzo kuhusu njia na majukumu ya chama cha msalaba mwekundu pamoja na kuheshimu nembo yake,” alisema Rhobi.

Alisema wamekuwa wakitoa mafunzo ya kuhudumia huduma ya kwanza, kuelimisha jamii umuhimu wa kutoa huduma ya kwanza na kujiunga na chama hicho.

Alisema hadi sasa chama hicho kipo katika mikoa 20 ambako kuna matawi madogo 300 ya Tanzania Bara na Zanzibar ambayo ni pamoja na Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Kigoma, Kagera, Dodoma, Tabora, Rukwa, Mbeya, Njombe  Iringa, Singida, Shinyanga, Simiyu na Manyara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles