Msako wa usafi sasa nyumba kwa nyumba, mabasi ya abiria

0
762

Ramadhan Hassan -Dodoma

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imewataka maofisa afya kukagua mabasi ya abiria kama yanafanyiwa usafi na kunyunyuziwa dawa (fumigation), mashuka na mataulo kwenye nyumba za wageni pamoja na usafi wa nyumba kwa nyumba ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Hayo yalielezwa jana jijini hapa na Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na maafisa afya wa Mkoa wa Dodoma.

Alisema maofisa afya wanajukumu la kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika kwa kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuhakikisha magari yanasafishwa na kunyunyuziwa dawa kabla ya safari ili kukabiliana na magonjwa ambayo sio ya kuambukiza.

“Tunaposafiri ni lazima tuhakikishe vyombo vya usafiri vinakuwa safi na salama, wamiliki wa vyombo vya usafiri  fanyeni fumigation ili kama kuna wadudu wa kuambukiza mfano malaria wanfe,”alisema.

Subi alitaja maagizo mengine ni mikoa yote nchini kufanya ukaguzi maalum wa usafi unavyotekelezwa katika maeneo yao na kuhakikisha nyumba za kulala wageni mashuka na mataulo yanakuwa safi, na yanapigwa pasi ili kuua vijidudu vya maambukizi  vya  magonjwa.

Maagizo mengine ni kuhakikisha masoko yanakuwa safi, kukagua magari ambayo yanasafirisha nyama kama ni masafi na kufanya ukaguzi wa wa usafi nyumba kwa nyumba.

“Kagueni pia katika taasisi za umma kama wanafanya usafi, lakini kubwa ofisa afya usikae ofisin,i toka nenda nje utajua matatizo yapo wapi na yanatakiwa kutatuliwaje,”alisema.

Katika hatua nyingine Dk.Subi alisema Wilaya ya  jombe imekuwa ya mfano  kwa kuweza kujenga vyoo bora kwa asilimia 95 hivyo kutokuwa na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu.

Alisema Serikali imefanya juhudi kuhakikisha ugonjwa wa kipindupindu unapotea nchini kwa kusimamia ujenzi wa  vyoo bora na sehemu za kunawia mikono ambapo vijijini vimejengwa vibuyu chirizi.

Alisema wameendelea kuhakikisha ugonjwa wa ebola hauingii nchini licha ya kuripotiwa nchini Congo ambapo zaidi ya watu 13,400 wameambukizwa huku watu 2,200 wakiwa wameishafariki.

“Tumeendelea kufunga mashine za kisasa katika maeneo ya mipakani ikiwemo maeneo ya jirani na Congo ili kuweka tahadhari ya ugonjwa wa ebola katika hilo tumefanikiwa kwa kaisi kikubwa,”alisema.

Alisema mwaka 2015 maambukizi ya malaria yalikuwa ni asilimia 14.7 ambapo kwa mwaka 2017 yameshuka na kufikia asilimia 7.3 ambapo alisema hayo ni mafanikio makubwa.

Kwa upande wake, Ofisa Afya Mkoa wa   Dodoma, Dk. Carle Lyimo, alisema kwa Mkoa wa Dodoma  wanakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watu kutupa taka ovyo, uwepo wa inzi wengi na abiria kutupa taka ovyo pamoja na kujisaidia njiani.

“Tuna mkakati tunauita mita tani kila mmoja lazima afanye usafi mita tano, lengo ni kuhakikisha maeneo yote yanakuwa safi lakini ni lazima kuwe na muongozo wa mama lishe na baba lishe  na mfumo wa ukusanyaji taka,”alisema.

Alisema ili wafanikiwe ni lazima kila ofisa afya apewe eneo la ukaguzi, kuwe na daftari eneo alilokagua na kuboresha ufanyaji usafi wa kila  Jumamosi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here