Na GRACE SHITUNDU -DAR ES SALAAM
NAIBU Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza amesema malalamiko yanayotolewa na vyama vya siasa kuhusu kuenguliwa wagombea wao katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa yamesababishwa na wao wenyewe.
Nyahoza alitoa kauli hiyo baada ya kutafutwa na MTANZANIA Jumapili lililotaka kufahamu kauli ya Ofisi ya Msajili kama mlezi wa vyama vya siasa nchini kuhusu malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya vyama vya upinzani, hususani Chadema na ACT Wazalendo, vikidai wagombea wao kuenguliwa kwa hujuma na hata kufikia hatua ya kujitoa kushiriki uchaguzi huo.
Miongoni mwa malalamiko ambayo yalitolewa na vyama hivyo, ni pamoja na wagombea wao kuenguliwa au kuwekewa pingamizi kwa sababu ya kukosa sifa kutokana na kukosea kujaza fomu zao.
Mengine ni wagombea kuenguliwa kwa sababu ya kujaza jina la chama kwa kifupi mfano, Chadema badala ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo au ACT Wazalendo badala ya Alliance for Change and Transparency.
Akizungumza na gazeti hili, Nyahoza alisema matatizo na malalamiko mengi yanayovikumba vyama vya upinzani katika uchaguzi huu, yanatokana na kutozingatia sheria na kanuni zilizowekwa.
“Hivi vyama mara kwa mara tunaongea nao kuhusu kuzingatia sheria na kanuni, sasa kama watakuwa hawazisomi na kuzifuata watakuwa wanalalamika mara kwa mara,” alisema Nyahoza.
Kuhusu fomu inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya mgombea mmoja ambaye amekatwa baada ya kuandika kwa kifupi ACT Wazalendo na kuelezwa na msimamizi wa uchaguzi huo kwamba chama hicho hakipo kwenye orodha ya msajili, alisema chama hicho kimesajiliwa kwa jina la Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) na sio ACT Wazalendo, hivyo hilo ni kosa.
“Hiyo wanayosema ni kifupi ni kama ilivyo CCM kwa Chama Cha Mapinduzi, lakini huwezi kuandika CCM tu kwani inaweza ikawa inamaanisha kitu kingine.
“Sisi kama walezi siku zote tumekuwa tukiwasisitiza kuzisoma na kuzingatia sheria, lakini kama baba unasema na mtoto hafuati matokeo yake ndiyo hayo,” alisema Nyahoza.
Alisema kuwa vyama vyote vya siasa vina wanasheria na watu waliobobea kwenye mambo hayo, ambao wana uwezo wa kuwaongoza wanachama wao katika mambo hayo muhimu.
Wakati Naibu Msajili akisema hayo, siku moja baada ya Chadema kutangaza kujiondoa katika uchaguzi huo, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alitoa kauli ya kushangazwa kwake na hatua hiyo iliyofanya na Chadema.
Aidha alikiri ni kweli kuna fomu zina makosa katika kujaza, lakini mchakato wa rufaa upo kwani kanuni haijamfunga mtu yeyote kudai haki ya kukata rufaa.