27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MSAJILI ALIYESIMAMISHWA KAZI NA MWIGULU ARUDISHWA KAZINI

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM


MSAJILI wa Taasisi za Kidini, Maryline Komba, ambaye alisimamishwa kazi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Mwigulu Nchemba, amerudishwa kazini.

Komba alisimamishwa kazi Juni 8, mwaka huu kupisha uchunguzi kuhusu waraka wa maelezo alioutoa kwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheli Tanzania (KKKT), jambo ambalo lilizua taharuki kwa jamii.

Kurudishwa kwa msajili huyo, kulibainika jana Dar es Salaam baada ya kuwasili kwa Waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Komba alikuwa mmoja wa viongozi waliompokea waziri huyo sambamba na kuhudhuria kikao cha ndani.

Katika kikao hicho, Waziri Lugola aliwataka watendaji wa wizara kubadilika na kutimiza majukumu yao badala ya kufanya kazi kwa mazoea.

Mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo, aliiambia MTANZANIA kuwa Mwigulu hakuwa na mamlaka ya kumsimamisha kazi Komba.

“Mama Komba siku zote alikuwa kazini kwani mwenye wajibu wa kusimamia nidhamu kwa watendaji ni Katibu Mkuu na si Waziri… ndiyo maana leo Komba alikuwa ni mmoja wa watendaji wa wizara ambao wamempokea waziri wetu mpya.

“Tuna imani sasa tunakwenda kufanya kazi kwa nidhamu na utendaji wa hali ya juu maana tunajua sasa hata Rais (Dk. John Magufuli) ametutaka kufanya kazi kwa weledi na kujituma zaidi na waziri wetu anakuja kutupa nguvu mpya kwenye utendaji na tunaamini kwa uwezo wake Mungu tutafika kwenye kile ambacho tunatakiwa kufanya bila kuvunja sheria wala kumwonea mtu,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa wizara hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Hata hivyo, katika makabidhiano ya ofisini jana, Lugola alipokewa na Naibu Waziri, Hamad Mussa Masauni.

Katibu Mkuu, Meja Jenerali Jacob Kingu na naibu wake, Ramadhan Kailima walikabidhiwa ofisi na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Balozi Simba Yahya.

Awali akizungumza na watendaji wa wizara hiyo, Waziri Lugola alitangaza leo kuanza ziara ya kikazi mkoani Mbeya.

Hatua ya Lugola kuanzia Mbeya imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli, kumtaka achukue hatua za kukabiliana na ajali zinazoendelea kutokea kwenye mkoa huo ambazo hadi sasa  zimegharimu maisha ya takribani watu 40.

Juzi akiwaapisha mawaziri na makatibu wakuu hao, Rais Magufuli alieleza sababu kadhaa zilizomfanya kufanya mabadiliko kwa kumwondoa Mwigulu kwenye Baraza la Mawaziri ikiwa ni pamoja na kushindwa kusimamia na kuchukua hatua katika sakata la mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises ya kufunga teknolojia ya kisasa kwenye vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles