27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Msajili ajibu hoja vyama vya kisiasa

PATRICIA KIMELEMETA

MSAJILI wa Vyama Vya Siasa  amevitaka vyama vilivyoitisha mkutano wa kuupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vyaSiasa kuacha propaganda za kupotosha muswada huo kwa sababu hatua zote za mchakato wa maboresho walishirikishwa.

Ametoa kauli hiyo siku moja baada ya kufanyika mkutano wa vyama 15 vya siasa ambavyo pamoja na mambo mengine,vilitangaza kuupinga hadharani Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa vikidai unatengeneza kaburi la vyama vya siasa na demokrasia nchini.

Akijibu hoja za viongozi wa vyama hivyo kwenye mahojiano yaliyofanyika  Dar es Salaam jana, Msajili Msaidizi wa vyamavya Siasa, Sisty Nyahoza alidai  kilichosemwa na viongozi hao ni upotoshaji na kutengeneza propaganda zauongo.

Alisema lengo la serikali katika sheria mpya ni kuhakikisha   vyama vya siasa nchini vinapata sheria bora inayokwenda na wakati ambayo itatoa nafuu kwa vyama vya siasa kuendesha shughuli zao kwa uhuru na kwa mujibu wa katiba za vyama vyao.

Alisema  hakuna kipengele ambacho kinampa mamlaka msajili kuingilia uamuzi wa ndani ya vyama vya siasa.

Kwa mujibu wa Msajili, ameshangazwa kusikia  marekebisho hayo yanakwenda kuua au kukandamiza vyama vya siasa wakati siyo kweli kwa sababu vyama hivyo vilitoa maoni yao wakati wa mchakato wa maoni mpaka hatua ilipofikia.

“Sasa kama wanaona muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa unakwenda kuua au kuvikandamiza vyama kwa nini walitoa maoni yao?.

“Kwa sababu tuliwashirikisha hatua zote pamoja na kuitisha mikutano ya kujadili, kama waliona kunà dosari kwa nini wasingesema mapema mpaka wamesubiri usomwe kwa mara ya kwanza bungeni.

“Waache unafiki,wasiwaaminishe wananchi kwa propaganda za uongo,” alisema Nyahoza.

Alisema  kilichofanyika kwenye muswada huo ni maboresho ya kawaida ambayo vyama na serikali wamekuwa wakifanya kwenye sheria au katiba zao  kuhakikisha wanapata sheria bora.

Alitoa mfano wa Chama Cha ACT-Wazalendo ambacho alisema kiliwahi kufanya marekebisho ya katiba yake, vivyo hivyo kwa msajili wa vyama vya siasa kufanya maboresho ya sheria zake.

Alisema hakuna kipengele ambacho kinaonyesha msajili anaweza kuingilia uamuzi wa vyama.

Alisisitiza hoja hiyo ni dhaifu kwa sababu kila chama kinaongozwa na katiba yake, hivyo  kuwaaminisha wananchi katika hoja hiyo ni kupotosha ukweli.

“Kwa mfano, sheria ya zamani inasema chama au mtu akifanya makosa iwe madogo au makubwa katika chama, chama hicho kifutwe,lakini muswada huu umesema chama au mtu katika chama akifanya makosa aonywe na msajili au kupewa adhabu ndogo ya kusimamisha kwa muda kutojihusisha na shughuli za siasa ama kulipa faini,” alisema.

Alisema katika muswada huo mpya hakuna kipengele kinachowazuia wanasiasa kuhama chama, kugombea   baada ya kuhama au kujiunga na vyama vingine, bali wanasiasa watafanya hivyo kwa mujibu wa katiba ya chama alichotoka au anachokwenda na   msajili hatahusika na lolote katika jambo hilo.

Alisema mpaka sasa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria bado inaendelea na mchakato wa kukusanya maoni.

Alisema kama wanaona kuna shida walipaswa kuwasilisha maoni yao na kuainisha vipengele ambavyo wanaona vina matatizo  viweze kufanyiwa marekebisho na siyo kuwadanganya wananchi kama walivyofanya.

Alisema kama wanadhani serikali ina nia ya kufuta vyama vyama vya upinzani au kuvikandamiza siyo kweli  kwa sababu serikali hiyo hiyo ndiyo iliyoanzisha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 baada ya kuona kuna umuhimu wa kuwapo   vyama hivyo.

Msajili wa vyama vya siasa ni mlezi wa vyama hivyo na   ataendelea kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na katiba na si vinginevyo,  alisema.

Aliwataka wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao kuusoma muswada huo  waweze kuuelewa jambo ambalo linaweza kuepusha upotoshaji.

Kauli za viongozi wa upinzani juzi.

Katika mkutano wao   juzi, viongozi wa vyama 10 walidai   sheria hiyo haina manufaa wala maslahi kwa umma wa Watanzania kwa sababu utaondoa uhuru wa kufanya siasa.

Mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma), Hashim Rungwe, alitaja sababu tano zilizowasukuma kutumia Siku ya kumbukumbu ya Uhuru wa Taifa kuupinga muswada huo aliodai unaonekana kuwa na nia ya kurudisha nyuma demokrasia nchini.

Rungwe  alisema maeneo wanayoyapinga katika muswada huo ni kuua sheria namba 5 ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 iliyoweka utaratibu wa kuwapo  mfumo wa vyama vingi kwa lengo la kujenga demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Alisema lakini muswada huo  unampa mamlaka makubwa Msajili ambaye atakuwa si msajili tena bali mdhibiti wa vyama vya siasa ambako kifungu namba 4 kinafanyiwa marekebisho kumpa nguvu hiyo.

Alisema mswada huo umejaa adhabu za jinai na kufanya shughuli za vyama vya siasa kuwa jinai wakati ni haki ya  katiba. Vifungu vipya vyote vimeweka adhabu ya faini au kifungo au vyote hata kwa mambo madogo kama vile kukosea taarifa au msajili akitaka kujua taarifa za vikao vya chama,” alisema.

Rungwe alisema kifungu cha 3 ambacho kinafanyia marekebisho kifungu cha 4 kinatoa mamlaka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mfumo wa uchaguzi wa ndani wa chama na kuamua nani awe kiongozi wa chama wakati yeye si mwanachama wa chama husika.

Alisema eneo jingine ni kifungu cha tano ambacho kinatunga kifungu cha 5A kinachotoa sharti kuhusu elimu ya uraia/mafunzo ya kujenga uwezo yanayotolewa na taasisi au mtu aliyesajiliwa nchini au nje ya nchi kuomba kibali kwa Msajili kabla ya kufanya hivyo, lengo likiwa kuvidhibiti vyama vya siasa kuwa na uhusiano na taasisi au mashirika ya kimataifa.

Alieleza kuwa muswada huo pia unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kutaka taarifa yoyote kutoka kwenye chama au kiongozi wa chama kupitia mamlaka jumuishi na kupitia kifungu cha 5B, asipopewa hata kama ni taarifa za siri wanachama na viongozi wanakabiliwa na adhabu ya faini au kifungo.

Alisema kifungu kipya cha 6A(3) kinaingilia utaratibu wa katiba za vyama kwa kutoa sharti kuwa Mkutano Mkuu au Kamati Kuu havitakiwi kukasimu mamlaka yake kwa vyombo vingine ndani ya chama, suala ambalo halikubakili kwa vile  hata Bunge hukasimu mamlaka yake kwa kamati zake na kuziruhusu kutoa uamuzi kwa niaba ya Bunge zima.

Rungwe aliainisha kuwa kifungu kipya cha 8D(2) kinampa msajili mamlaka ya kuamuru chama kufuta au kurekebisha kifungu chochote cha katiba yake.

Alieleza pia kifungu cha 8E kinazuia vyama kuwa na kikundi cha ulinzi suala ambalo si zuri kwa kuwa kwa mujibu wa katiba, ulinzi ni jukumu la kila mtu.

“Lakini pia kuna kifungu cha 21E kinachompa msajili mamlaka ya kumsimamisha au kumfukuza uanachama mwanachama wa chama cha siasa.

“Lengo hapa ni kuwaondoa viongozi wa vyama wanaoikosoa Serikali kwa kuwa akimsimamisha uanachama na uongozi wake unakoma.

“Pia kuna uwezekano msajili akatumia kifungu hiki nyakati za uchaguzi kama wa urais, ubunge na udiwani kuwafukuza wagombea ambao wanaonekana kukubalika na hivyo kuwafanya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa,” alisema.

Alisema kifungu cha 6A(6) kinazuia vyama vya siasa kufanya shughuli za harakati au kuweka shinikizo kwa umma kuhusu masuala yanayowahusu watu hivyo kinafuta dhima ya chama cha siasa kama chombo cha kupinga ukandamizwaji na kutetea haki.

“Kwa hiyo kupitia kifungu hiki, sasa vyama vya siasa havitatakiwa kuwatetea wafanyakazi, wakulima, wavuvi na makundi ya  jamii kwa kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa ni kufanya harakati,” alisema.

Akizungumzia mchakato wa kupitishwa muswada huo, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema waliotunga muswada huo tayari wameshatunga na kanuni hatua inayoonyesha dharau kwa Bunge.

Mwakilishi wa CUF, Joram Bashange alisema muswada huo  una mazingira  magumu.

Viongozi waliotia saini tamko hilo na majina yao kwenye mabano ni Katibu Mkuu Chadema, Vicent Mashinji, ACT-Wazalendo (Yeremia Maganja) na Chaumma (Hashim Rungwe).

Wengine ni ADC (Doyo Hassan), CCK (David Mwaijojele), CUF (Joram Bashange), DP (Georgia Mtikila), NCCR-Mageuzi (Martin Mung’ong’o), NLD (Tozi Matwanga) na UPDP (Fahmi Dovutwa).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles