Mrisho Ngassa njia nyeupe kurejea Yanga

Mrisho Ngassa
Mrisho Ngassa
Mrisho Ngassa

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KIUNGO mshambuliaji wa Tanzania, Mrisho Ngassa, amevunja mkataba na klabu yake ya Free State ya Afrika Kusini, sasa huenda akarejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga katika dirisha dogo la usajili.

Ngassa alijiunga na Free State Mei mwaka jana ambapo alisajiliwa na kocha Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne, ambaye kwa sasa anaifundisha Mbeya City inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana Dar es Salaam kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa baada ya kuona hapati namba ndani ya Free State, Ngassa ameona arejee nyumbani na kuomba mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wampe nafasi katika kikosi hicho.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa Yanga ilimtaka Ngassa kuvunja mkataba wake na klabu hiyo ili iweze kumsajili.

Inadaiwa Ngassa alikutana na viongozi wa Yanga kipindi alichokuja nchini ambapo klabu hiyo ya Jangwani ilikuwa inacheza Fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Azam FC.

Ngassa alitakiwa na viongozi wa Yanga kuvunja mkataba wake na Free State kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kumnunua na pia aandike barua Shirikisho la Soka nchini (TFF) ya kuomba kufanya mazoezi na Yanga hadi kipindi cha dirisha dogo la usajili kitakapofika.

“Kwa muda mrefu Ngassa aliomba arejee Yanga ambapo aliaminika, lakini kwa kuwa hakuondoka vizuri viongozi walimtaka akavunje mkataba wake ndipo wampe nafasi katika kipindi cha dirisha dogo,” alisema mtoa habari wetu.

Kwa upande wake Ngassa alisema ameomba kuvunja mkataba baada ya kuona mahali alipo hakuna mwelekeo wa kufikia malengo yake aliyojiwekea, hivyo ameona bora arejee nyumbani ambako Yanga ipo tayari kumpokea.

“Napenda timu inayoshinda mataji, hivyo naondoka Free State na kwenda kujiunga na klabu yenye kushinda mataji, baadaye itajulikana ni timu gani tusubiri,” alisema.

Ngassa amefundishwa na makocha wanne, Denis Lavagne raia wa Ufaransa, Mjerumani Ernst Middendorp, Mtaliano Giovanni Solinas na Lavagne, ambaye amechangia Ngassa kuomba kuondoka kutokana na kutompa nafasi katika kikosi chake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here