27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

MRADI WA ADGG KULETA TIJA SEKTA YA UFUGAJI

Na AMINA OMARI


TAKWIMU kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula na Kilimo (FAO) za mwaka 2013, zinaonyesha Tanzania kuwa ni nchi ya tatu kwa wingi wa ng’ombe barani Afrika, ikiwa na jumla ya ng’ombe  24,531,673, ikitanguliwa na Ethiopia na Sudani.


Kwa upande wa uzalishaji wa maziwa, Tanzania inashikilia nafasi ya tatu barani Afrika, huku jirani yake Kenya ikiwa kinara wa uzalishaji huo.

Pamoja na wingi wa mifugo iliyokuwa nayo, Tanzania bado haijapata mafanikio makubwa
 kutokana na kushindwa kuwekeza kikamilifu katika uzalishaji wa ng’ombe bora pamoja na biashara ya maziwa.


Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuboresha sekta hiyo. Moja kati ya jitihada hizo, ni Mradi wa kitaifa wa Kuboresha Ng’ombe wa Maziwa (ADGG) uliozinduliwa hivi karibuni jijini Tanga.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela ambaye alimwakilisha Waziri wa  Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba, alisema mradi huo umelenga kumkomboa mfugaji kuondokana na ufugaji wa kimazoea ikiwemo kutokuwa na uhakika wa malisho hususani katika kipindi cha kiangazi.

Kupitia mradi huo, alisema wafugaji watafundishwa mbinu bora za ufugaji zitakazowasaidia kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maziwa pamoja na kuwa na mifugo michache wanayoweza kuimudu.


“Wafugaji wataweza kufuga kisasa kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano na wataweza kupata taarifa kuhusu hali za afya ya mifugo yao, ikiwemo muda wa ng’ombe akiwa na joto kupitia simu za mkononi,” alifafanua.

Katika utekelezaji wa mradi huo, anasema Serikali imedhamiria kuendesha zoezi la sensa ya mifugo ili kuweza kupata takwimu sahihi za ng’ombe waliokuwepo pamoja na ubora wake kwa ajili ya mipango endelevu ya kimaendeleo katika sekta ya maziwa hapa nchini.

Ofisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Abdallah Temba, alisema kwa mujibu wa takwimu walizozifanya mwaka 2014, walibaini idadi ya ng’ombe wa maziwa kufikia 780,000 na kuongeza kuwa, hawakuweza kupima ubora wao hususani katika wingi wa uzalishaji wa maziwa pamoja na ubora wa bidhaa hiyo.
 

“Sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa hapa nchini imekuwa na changamoto kuu mbili ambazo ni uhaba wa malisho pamoja na vinasaba vya ng’ombe bora ambao watakuwa na uwezo wa kuzalisha maziwa mengi,” anasema Temba.
 

Licha ya changamoto hizo, anasema Serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuagiza ng’ombe kutoka nje ya nchi kwa ajili ya mbegu ili kuongeza uzalishaji wa maziwa.
 

“Wizara imekuwa ikichukuwa jitihada mbalimbali ikiwemo kufungua mashamba ya kuzalisha mifugo pamoja na vituo vya kuuza mitamba ili kuhakikisha tunaleta mabadiliko katika sekta hiyo,” alibainisha ofisa huyo.
 

Mradi wa ADGG unatekelezwa katika nchi mbili ambazo ni Tanzania pamoja na Ethiopia kwa majaribio kabla ya kusambazwa katika nchi nyingine za Afrika.
 

Msimamizi Mkuu wa mradi huo katika ngazi ya kimataifa, Dk. Alliy Mwai, anasema Tanzania ina dhamana kubwa ya kuhakikisha mradi huo unakuwa ni wenye mafanikio ili kuhakikisha nchi nyingine zinanufaika na mradi huo.
 

Alisema mradi utasaidia kujua namna ya kutumia ng’ombe bora ambao wanatoa maziwa mengi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa za maziwa zenye tija na faida kwa wafugaji pamoja na Serikali kwa ujumla.
 

 “Wafugaji walikuwa wanafuga bila kuwa na elimu ya kuhifadhi kumbukumbu za taarifa ya utoaji wa maziwa wa mifugo yao, hivyo kutokujua kama mifugo hiyo imepunguza uzalishaji au la,” alieleza  Dk. Mwai.

Msimamizi wa mradi huo kitaifa, Dk. Eliamoni Lyatuu, alisema kupitia mradi huo wanatarajia kubadilisha sekta ya ufugaji kutoka wa kimazoea na kuingia kwenye ufugaji unaoendana na matumizi ya sekta ya mawasiliano ya kiteknolojia.
 

Alisema mradi umelenga kutoa elimu ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji wa kutumia ng’ombe wachache, lakini wanaotoa mavuno mengi ambayo yatasaidia kuongeza uzalishaji wenye tija.
 

Pamoja na mambo mengine, mradi utawezesha wafugaji kuwakutanisha na maofisa ugani kwa
urahisi na kuweza kuunda mtandao wa mawasiliano ambao wataweza kutatua changamoto zinazokabili sekta hiyo kwa urahisi.
 

“Tutaweza kufuatilia mwenendo wa matukio kwenye shamba la mfugaji kama makuzi ya ndama na matukio mengine ya uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa kila mwezi pamoja na kutoa mrejesho wa moja kwa moja kwa mfugaji kupitia simu ya kiganjani,” amesema Dk. Lyatuu.
Mwakilishi wa wafugaji wa Jiji la Tanga, Regina Msuya, alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo wafugaji ni kutokuwa na elimu sahihi juu ya matumizi ya madawa kwa ajili ya mifugo hiyo
pamoja na kutokuwa na uhakika wa kupata ndama bora ambao wataweza kuwapatia mavuno mengi na bora kwa kipindi kirefu.

“Tunanunua majike ya ng’ombe kwa bei kubwa, huku tukihakikishiwa kuwa wana uwezo wa kutoa maziwa mengi lakini baada ya muda maziwa yanapungua na kuwa hasara kwa wafugaji,” amesema Msuya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles