MRADI  KAPUNGA RICE WABADILI  MAISHA WAKULIMA MBARALI

0
1930

Na MWANDISHI WETU-MBEYA


KILIMO ni moja ya shughuli kubwa katika kuinua uchumi wa Tanzania, ambapo asilimia 74 ya Watanzania wanaendesha maisha yao kutokana na kazi hiyo.

Pamoja na hilo, sekta hiyo imekuwa ikichangia asilimia 24  ya Pato la Taifa.

Hadi mwaka 2016, Tanzania ilikuwa na ekari  zaidi ya milioni  44  za ardhi inayofaa kwa ajili ya kilimo, lakini ni asilimia 33 tu iliyokuwa ikitumika kwa ajili ya shughuli hiyo.

Asilimia 70 ya wananchi masikini wanaishi katika maeneo ya vijijini na wengi wao wamekuwa wakijihusisha na sekta hiyo ya kilimo.

Ardhi ni hazina muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula na kati ya mazao makuu tisa ya chakula nchini ni mahindi, mtama, mchele, ngano, maharagwe, mihogo, viazi vitamu na ndizi.

Katika eneo la Mlima Chimala uliopo katika Wilaya ya  Mbarali mkoani Mbeya ambao upo Kusini mwa Tanzania, kuna eneo lenye ukubwa wa ekari 5,500 ambalo limetengwa na  kuendelezwa kupitia Mradi wa Kilimo cha Mpunga unaojulikana kama Kapunga Rice Project Limited.

Mradi huo wa Kapunga Rice project si kwamba umekuwa ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo, bali pia umeweza kubadili maisha ya wakulima wadogo wadogo.

Wakibadilisha uzoefu na waandishi wa habari, baadhi ya wakulima walisema huko nyuma walikuwa wakizalisha kiasi kidogo cha mpunga, lakini tangu mradi huo wa Kapunga Rice project Limited uanze, mambo yamebadilika na hali yao kimaisha imekuwa nzuri.

Mmoja wa wakulima hao, Charles Komba ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Kapunga, anasema  kutokana na hali hiyo, kwa sasa benki zimekuwa zikimkopesha bila wasiwasi.

“Kipindi cha miaka ya nyuma tulikuwa hatuzalishi mchele kwa ajili ya biashara na kama tulikuwa tukijaribu kufanya hivyo, tulikuwa tukizalisha kwa kiasi kidogo.

“Lakini tangu mradi huu wa Kapunga Rice uanzishwe, kwa sasa tuna uhakika wa kuzalisha mazao mengi na tuna uhakika wa soko,” anasema Komba.

Akiunga mkono kauli hiyo ya  Komba, mkulima mwingine, Evariste Mgiye, anasema kupitia mradi huo ameweza kupata mbinu za kuendesha kilimo cha kisasa, matumizi ya mbolea, mbegu bora na  jinsi ya kutafuta masoko.

Akizungumza kuhusu manufaa ya matumizi ya mbegu bora, mkulima mwingine, StumaiTandila, anasema kwa sasa ana uhakika wa kupata tani tisa kutoka katika eneo lenye ukubwa wa hekta moja tofauti na kipindi cha nyuma alipokuwa akizalisha tani moja kutoka eneo lenye ukubwa kama hilo.

“Mbegu kutoka Kapunga zinazalisha mazao mengi kwa sababu kwa sasa naweza kupata zaidi ya tani tisa za mavuno kutoka ndani ya hekta moja, kiasi ambacho nilikuwa siwezi kukipata katika kipindi cha nyuma,” anasema mkulima huyo.

Mbali na kupata mazao mengi, Flora Mwaipaja anasema mpunga wanaouzalisha kwa sasa ni bora katika mauzo sokoni.

“Ni bidhaa ambayo inauzika na wala huwezi kupata shida kutafuta soko bora la mchele. Umesaidia kubadilisha maisha yangu na kwa sasa namiliki nyumba ya wageni mjini Mbeya kutokana na biashara hii ya kilimo cha mchele,” anasema.

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya Maendeleo na Ushirika (CRDB), Wilaya ya  Mbarali, Ruhore Masaka, anasema wakulima wamenufaika na mradi huo na umewapa uhakika wa kuwakopesha.

“Tangu tumeanza kuwakopesha fedha, hatujawahi kukutana na matatizo katika marejesho kwa sababu biashara yao ni nzuri na inatoka. Wanavuna, wanauza na kurejesha mikopo yao kwa wakati,” anasema Masaka.

Meneja wa mradi huo, Edward Rweyendara, anasema kwa sasa wana uhusiano wa karibu na maelfu ya wakulima wadogo wadogo na karibu familia 350 za wakulima zimenufaika  na upatikanaji wa mashamba, mbegu, mbolea, vifaa vya kilimo, mavuno na usafiri kutoka mashambani katika vinu vya kukoboa mpunga.

“Tumebadili maisha yao kwa kuwapa mbinu za kutumia kilimo cha kisasa. Tunawasaidia wakulima kwa kuwapa mbegu bora kutoka Kituo cha Utafiti Dakawa  kwa sababu mbegu walizokuwa nazo kipindi cha nyuma walikuwa wakizalisha chini  ya tani moja kutoka eneo la ekari moja, lakini baada ya kuanza kutumia mbegu hizi wana uhakika wa kuzalisha wastani wa tani  6.5  kwa kila ekari,” anasema  Rweyendara.

Mbali na wakulima, Rweyendara anasema wanatumia teknolojia ya kisasa ili kuboresha ekari 3500 za ardhi kwa ajili ya kilimo cha  umwagiliaji.

“Tumewapa ajira za kudumu Watanzania 160 wakati wa msimu wa mavuno, tumekuwa tukishirikiana moja kwa moja na wafanyakazi  zaidi ya 3000 kila siku,” anasema meneja huyo.

Anasema katika shughuli hizo za kilimo, wanatumia mitambo ya kupandikiza, kunyunyizia kemikali kwa kutumia dawa za kupuliza ambazo hutumiwa na wakulima na kuwawezesha kuhudumia eneo lenye ukubwa wa ekari  135 kwa siku.

Anasema kwa kutumia njia hiyo ya kisasa, wana uhakika wa kupata wastani wa tani  22,000 za mchele kwa kila mwaka.

“Watu zaidi ya 10,000 wa jumuiya zilizotuzunguka, wamefaidika moja kwa moja au katika shughuli mbalimbali zinazohusiana na kilimo.

“Kupitia mpango huu, wakulima wamepata faida kubwa kwa kuboresha na kuwa na kilimo endelevu. Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii na wakulima wadogo wadogo kuanzia kupanda, kuvuna hadi masoko na kuongeza uchumi wao,” anasema.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni alitembelea mradi huo wakati alipokuwa mkoani Mbeya katika ziara ya kikazi, huku akiupongeza kwa kuwezesha kuboresha maisha ya kisasa kwa wakazi wa eneo hilo.

“Hatutaki kusikia juu ya kushindwa kwa mradi huo, kutokuelewana na wafanyakazi. Tunataka kusikia habari njema kwamba wafanyakazi wanafanya kazi vizuri na kulipwa na mradi huo unaendeleza shughuli zake za uwekezaji wake,” anasema.

 

MAJUKUMU KATIKA USHIRIKI WA SHUGHULI ZA KIJAMII

 

Mbali na kilimo, mradi huo wa  Kapunga Rice  umekuwa ukishiriki katika shughuli za kijamii, ambapo umejenga na kuboresha huduma za miundombinu za kijiji.

Miongoni mwa huduma hizo za kijamii ni ujenzi wa Shule ya Msingi  Kapunga B ambayo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya  300, Ujenzi wa Kituo Cha Polisi Chimala na Kituo cha Afya  Mapogoro  kwa gharama ya Sh milioni 700.

Kitu hicho cha afya kinatarajia kuhudumia zaidi ya watu 18,000 waishio ndani ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Jiwe la Msingi la Kituo cha Afya liliwekwa na Samia Suluhu wakati alipotembelea Kijiji cha  Kapunga  hivi karibuni.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here