27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Mr Kuku afikishwa kizimbani

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MFANYABIASHARA Tariq Machibya (29), maarufu Mr Kuku, amefikishwa mahakamani akituhumiwa kwa mashtaka saba ikiwemo kutakatisha jumla ya Sh bilioni 17 kwa kuendesha biashara ya upatu bila leseni.

Mfanyabiashara huyo ambaye ni mkazi wa Oysterbay, Dar es Salaam, alisomewa mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai, shtaka la kwanza mshtakiwa anadaiwa kusimamia biashara ya upatu.

Inadaiwa  kati ya Januari 2018 na Mei, mwaka huu, maeneo tofauti Dar ea Salaam alijihusisha na biashara hiyo kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma kwa kujifanya  watafanya ujasiriamali wa ufugaji kuku na watapata faida asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa uwekezaji wa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kibiashara kuliko mtaji uliokusanywa.

Shtaka la pili, anadaiwa kukubali kupokea fedha kutoka kwa umma. Katika kipindi hicho anadaiwa kupokea Sh bilioni 17.

“Shtaka la tatu kutakatisha fedha,  anadaiwa kati ya Aprili 26, mwaka jana na Januari 26, mwaka huu maeneo tofauti Dar es Salaam, alijihusisha na miamala ya Sh 6,477,297,614.83 kwa kuzitoa kutoka akaunti ya Mr Kuku iliyopo CRDB, huku akijua ni zao la kusimamia biashara ya upatu.

“Katika shtaka la nne, anadaiwa kutakatisha, inadaiwa kati ya Januari 17, mwaka huu na Machi 30, mwaka huu Dar es Salaam, alijihusisha na miamala ya Sh 629,249,576.36 kwa kutoa kwenye akaunti namba 0152480653700 huku akijua fedha hizo ni zao la upatu.

“Shtaka la tano anadaiwa kutakatisha Sh 1,366,718,045.46 huku akijua ni zao la kuendesha biashara hiyo ya upatu, anadaiwa kuzitoa katika akaunti ya Mr Kuku namba 0150481394800 iliyopo Benki ya CRDB,” alidai Wankyo.

Alidai katika shtaka la sita mshtakiwa alitakatisha Dola za Marekani 107,893.73, anadaiwa kuziingiza katika akaunti ya Mr Kuku kati ya Januari 17 mwaka huu na Januari 30 mwaka huu Benki ya CRDB tawi la Viva Tower Kinondoni.

Katika shtaka la mwisho mshtakiwa huyo anadaiwa kutakatisha Dola za Marekani 146,300 kwa kuziingiza katika akaunti ya Mr Kuku iliyopo CRDB  huku akijua ni zao la biashara hiyo ya upatu aliyokuwa akiendesha bila leseni.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote, upelelezi haujakamilika na kesi itatajwa Agosti 24, mwaka huu na amerudishwa rumande.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles