MSANII wa nyimbo za asili, Mrisho Mpoto, amezindua mfuko wake wa Mpoto Foundation wenye makao yake makuu katika Kijiji cha Kibamba Kitongoji cha Bogolwa Wilaya ya Pwani, utakaokuwa na lengo la kusaidia vijana waweze kutimiza ndoto zao kwa kupitia ajira binafsi.
Kwa mujibu wa Mpoto, mfuko huo utasaidia vijana wasio na kazi waweze kufanya kazi za kujiajiri wenyewe ili kupitia kazi hizo waweze kutimiza ndoto zao.
“Project hii itawasaidia vijana kuondoa dhana kwamba mjini ndio kuna kazi pekee wakati hata kijijini unaweza kujiajiri kwa kutumia kilimo, sanaa na mambo mengine mengi,” alifafanua.
Katika hatua nyingine Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Alnajem, alizindua mradi wa kisima cha maji kwa ajili ya kusaidia wanakijiji wa kitongoji hicho kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na ukosefu wa maji safi na salama.
Alnajem alisema mradi huo umetokana na ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na nchi yao huku akiahidi kusaidia maeneo mengine yenye uhitaji mbalimbali ambao unatokana na ushirikiano wao na Tanzania.