NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MPIGACHAPA Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo, ametoa mwezi mmoja kwa watu wanaojihusisha na utengenezaji wa vyeti bandia vya Serikali kujisalimisha kabla hawajachukuliwa hatua za sheria.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam liliwakamata watu watatu ambao walikutwa na vyeti bandia vya kidato cha nne, vyeti vya uuguzi, stika za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), vyeti vya kuzaliwa na vyuo vya ufundi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Chibogoyo alisema wanakusudia kuendesha msako nchi nzima kuwabaini watu hao na kuwachukulia hatua za sheria.
“Baada ya muda tuliotoa kuisha tutafuatilia mkoa hadi mkoa kuhakikisha tunadhibiti nyaraka bandia,” alisema Chibogoyo.
Aliwataka Watanzania kuacha kutumia vibaya bendera, nembo na wimbo wa taifa kwa sababu ni vielelezo vya taifa.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na ile inayopendekezwa, zote zinaelekeza kuhusu matumizi bora ya vielelezo vya taifa kama vile bendera, nembo na wimbo wa taifa.
“Bendera iheshimiwe, hairuhusiwi kupeperusha bendera iliyotoboka, kupauka au chafu. Katika maeneo mengine unaweza kukuta bendera inapandishwa au kushushwa lakini watu wamekaa chini na wengine wanaendelea na shughuli zao,” alisema Kibogoyo.