24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MPC yapandisha Riba ya Benki Kuu kutoka Asilimia 5.5 hadi 6

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imepandisha Riba ya Benki Kuu kutoka asilimia 5.5 iliyotumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 hadi asilimia sita ambayo itatumika katika robo ya pili ya mwaka yaani Aprili hadi Juni, mwaka huu.

Akizungumza leo Aprili 4, 2024 jijini Dar es Salaam Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), Emmanuel Tutuba amesema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Aprili 3, mwaka huu na umezingatia tathmini ya mwelekeo wa uchumi iiliyofanyika Machi, mwaka huu.

“Kamati imeona umuhimu wa kuongeza Riba ya Benki Kuu hadi asilimia sita itakayokuwa na wigo wa asilimia mbili juu na chini, ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei siku zijazo kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa dunia,” amesema Gavana Tutuba.

Amesema kutokana na tathmini ya mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati imebaini kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ukuaji wa uchumi uliimarika katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi.

“Mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sambamba na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha, bei za bidhaa katika soko la dunia imebaki tulivu. Mathalan, bei ya mafuta ghafi ilikuwa wastani wa dola za marekani 80 kwa pipa, wakati bei ya dhahabu imeendelea kubaki juu, ikiuzwa kwa wastani wa dola za Marekani 2,071 kwa wakia moja,” amesema.

Gavana Tutuba amesema hali hiyo inatarajiwa kuendelea katika kipindi kijacho cha mwaka huo na matarajio hayo yanaweza kuathiriwa na uamuzi wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi (OPEC+) kuhusu kiwango cha uzalishaji pamoja na migogoro ya kisiasa inayoendelea.

MWENENDO WA UCHUMI

Kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchini, Kamati imeridhishwa na kuendelea kwa uchumi, licha ya changamoto zilizotokana na mtikisiko katika uchumi wa dunia.

Alisema hali hiyo ya kuimarika kwa uchumi inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo, hususan robo ya pili ya mwaka huu.

MAENEO YALIYOFANYIWA TATHMINI

Gavana Tutuba ametaja maeneo mahususi ya mwenendo wa uchumi yaliyofanyiwa tathmini na Kamati kuwa ni ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka 2023, kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022.

“Aidha, ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024. Mwenendo huu unatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali hususan katika ujenzi wa miundombinu unaolenga kuongeza uwekezaji kwa sekta binafsi.

“Vilevile, sekta binafsi imeendelea kuchangia katika kuimarika kwa uchumi kutokana na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Hali hii inadhihirika kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi na uwekezaji kutoka nje ya nchi,” ameeleza.

Tutuba amesema mwenendo wa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa wa kuridhisha na umekadiriwa kukua kwa zaidi ya asilimia sita kwa mwaka 2023 kutokana na kuimarika kwa shughuli za uchumi, hususan utalii.

“Mwenendo huu wa kuridhisha wa ukuaji wa uchumi nchini unatarajiwa kuendelea katika kipindi kijacho cha mwaka 2024. Hali hii inatokana na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji, mvua za kutosha katika maeneo mengi nchini na kuendelea kuimarika kwa uchumi wa dunia,” amesema.

Pili, mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu, kwa wastani wa asilimia 3.0 kwa robo ya kwanza ya mwaka huu, kiwango hicho kilikuwa ndani ya lengo la nchi la mfumuko wa bei usiozidi asilimia tano na vigezo vya kikanda kwa jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama.

Amesema hali hiyo inatokana na utekelezaji wa sera madhubuti ya fedha na uwepo wa chakula cha kutosha nchini.

Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei umeendelea kupungua kufikia karibu lengo la asilimia tano kutokana na kupungua kwa bei za chakula na bidhaa zisizo za chakula.

Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa mdogo na tulivu kutokana na utekelezaji wa sera thabiti ya fedha na upatikanaji wa chakula cha kutosha.

Tatu, utekelezaji wa sera ya fedha katika robo ya kwanza ya mwaka huu, uliiwezesha riba ya mikopo ya siku saba katika soko la jumla la fedha baina ya benki kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3.5 hadi 7.5, kama ilivyotarajiwa.

“Ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi uliendelea kuwa imara, kwa wastani wa takriban asilimia 17. Mikopo hiyo ilielekezwa zaidi katika shughuli za kilimo, uchimbaji wa madini, usafirishaji na uzalishaji viwandani. Mikopo kwa sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuongezeka katika kipindi kijacho cha mwaka huu kutokana na kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji,” amesema.

Nne, Utekelezaji wa sera ya bajeti ulikuwa wa kuridhisha, ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka huu, mapato ya Serikali yalikuwa takriban asilimia 95 ya lengo kwa Tanzania Bara.

Kwa upande wa Zanzibar, mapato ya ndani yalivuka lengo kwa asilimia 6.4 kutokana na maboresho katika usimamizi wa kodi na kuongezeka kwa utayari wa wananchi kulipa kodi.

Pia matumizi ya Serikali yameendelea kufanyika kulingana na rasilimali zilizopo, huku deni la Taifa likiendelea kuwa himilivu.
Tano, Nakisi ya urari wa biashara nje ya nchi iliendelea kupungua kutokana na kupungua kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi.

“Katika mwaka unaoishia Februari mwaka huu, nakisi ilipungua kufikia dola za kimarekani milioni 2,701.4 kutoka dola za kimarekani milioni 5,133.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

“Kwa upande wa Zanzibar, nakisi ya urari wa biashara pia ilipungua. Nakisi ya urari wa biashara inatarajiwa kuendelea kupungua na kufikia asilimia 3.2 ya Pato la Taifa kwa kipindi kilichobaki cha mwaka huu,” amesema.

Tutuba amesema akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha, kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 5.3 mwishoni mwa Machi, mwaka huu sawa na miezi 4.4 ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.

Thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilipungua kwa asilimia 1.8 katika robo ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 1.6 katika robo ya mwisho ya mwaka 2023.

Amesema hali hiyo ilitokana na msimu wa mapato madogo ya fedha za kigeni pamoja na mazingira ya kiuchumi duniani.

“Kamati pia ilijadili kuhusu changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni nchini na kujiridhisha kwamba hatua za kuongeza upatikanaji na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotekelezwa hivi sasa zinatarajiwa kupunguza changamoto hiyo ndani ya muda mfupi ujao,” amesema.

Sita, sekta ya fedha imeendelea kuwa imara na thabiti huku viashiria vyote vya uthabiti vikiwa ndani ya wigo unaokubalika kisheria.
Tutuba alisema sekta ya kibenki imeendelea kuwa na ukwasi na mtaji wa kutosha, huku ikiendelea kutengeneza faida.

“Ubora wa rasilimali za benki ulikuwa wa kuridhisha, ambapo uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ulikuwa asilimia 4.3 ambayo iko ndani ya wigo unaokubalika wa uwiano wa chini ya asilimia tano ya mikopo yote,” amesema.

UMOJA WA MABENKI NCHINI

Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki nchini, Theobat Sabi amesema kutokana na riba hiyo wananchi wategemee kuona viwango vya mikopo chechefu kushuka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles