24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MPANGO WA MATOKEO MAKUBWA SASA WAVUNJWA

Rais Dk. John Magufuli, akizungumza na watumishi wa iliyokuwa Ofisi Rais Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) waliokuwa wakisimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa(BRN),Ikulu Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli  ameagana na wafanyakazi wa iliyokuwa Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (President’s Delivery Bureau – PDB),  ambao wamehamishiwa katika ofisi na taasisi nyingine za Serikali   kuendelea na utumishi wa umma.

Wafanyakazi hao ndiyo walikuwa wakisimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now – BRN).

Kutokana na uamuzi huo sasa ni wazi mpango huo wa BRN umevunjwa rasmi.

Rais Dk. Magufuli alikutana na kuagana na waliokuwa wafanyakazi wa BRN Ikulu   Dar es Salaam jana.

Aliwashukuru kwa kazi nzuri waliyoifanya wakiwa PDB na amewataka kuendelea kulitumikia Taifa kwa juhudi na maarifa wakiwa katika ofisi nyingine walizopangiwa.

“Natambua kuwa nyie ni wafanyakazi wazuri wenye ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya Taifa letu.

“Mmetoa mchango mkubwa mlipokuwa PDB nategemea mtaendelea hivyo na hata zaidi katika ofisi mbalimbali mlizopangiwa, mkachape kazi kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania,”  alisema Rais Dk. Mafuguli.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, Katibu Mkuu wa Utumishi, Dk. Laurian Ndumbaro.

Wakati huo huo,   Rais Magufuli amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa miundombinu ya mabwawa ya maji kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Alijadiliana nao kuhusu utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project) ambao una uwezo wa kuzalisha megawatt 2,100 za umeme.

Rais  amekutana na wataalamu hao ikiwa ni utekelezaji wa nia yake ya kuhakikisha mradi huo unaanza kujengwa haraka iwezekanavyo na kuzalisha umeme mwingi utakaosaidia kuharakisha maendeleo   nchini, hususan ujenzi wa viwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles