23.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 27, 2023

Contact us: [email protected]

Mpango wa kuifumua Dar waiva

William Lukuvi
William Lukuvi

Na GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM

WAKATI Serikali ikiwa katika mchakato wa kuhamia rasmi makao makuu ya nchi mkoani Dodoma, imeweka wazi kwamba mpango wa kulifumua upya Jiji la Dar es Salaam na kulifanya kuwa kitovu cha biashara sasa umeiva.

Akizungumza na wadau mbalimbali wa uwekezaji katika ujenzi jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema mchakato wa kupata Mpango Mpya wa Mji ‘City Master Plan’ wa Dar es Salaam tayari umeanza.

Alisema Mpango Mpya wa Mji wa                 Dar es Salaam unatarajiwa kupatikana kabla ya Desemba mwaka huu ambapo kampuni kutoka Italia kwa kushirikiana na Watanzania wanaifanyia kazi.

“Pamoja na kuhamia Dodoma ni lazima  tuifumue Dar es Salaam na kuifanya kuwa kitovu cha biashara kwa kuwa na majengo ya kisasa yatakayokuza uchumi wetu.

“Tunatarajia kutumia Dola milioni 300 kwa ajili ya kupiga picha toka angani kwa ndege ili kuipata Dar es Salaam vizuri na kutengeneza mpango mji utakaokuwa wa kisasa,” alisema Waziri Lukuvi.

Pia Waziri Lukuvi aliwahamasisha wadau hao kujiandaa kuwekeza Dar es Salaam na Dodoma kwa kuwa Serikali itakapohama jijini majengo yote ya Serikali yatahitaji uwekezaji.

“Hii ni fursa ambayo mnatakiwa kuiangalia kwa karibu kwani kwa upande wa Dodoma kutahitajika huduma nyingi ikiwemo ya majengo ambayo yatakuwa ya makazi, ofisi na huduma nyingine za kiuchumi.

“Na wakati huo huo Serikali itakapohamia Dodoma, jiji hili litatakiwa kuwa na mwonekano wa kisasa ili liwe na mvuto wa kibiashara na kukuza uchumi wetu,” alisema Waziri Lukuvi.

Pamoja na kuwahamasisha wadau hao ambao wengi ni wamiliki wa makampuni ya ujenzi, Waziri Lukuvi aliwataka kuhakikisha wanatumia teknolojia za kisasa na kuwa na majengo yenye ubora na imara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,729FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles