26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

MPANGO WA KUBAINI VYETI FEKI UTEKELEZWE KILA KONA

TATIZO la kughushi nyaraka ni ugonjwa ulioikumba jamii yetu kwa muda mrefu sasa. Baadhi ya watu wamekuwa wakighushi vyeti vya shule, vyeti vya kuzaliwa, leseni na hata vyeti vya ndoa.

MTANZANIA Jumamosi tunaamini kwamba wakati Serikali ina jukumu la kuwabaini na kuwashtaki watuhumiwa, jamii inalo jukumu kubwa la kubadili mtazamo. Tuache kutaka kufanikisha mambo yetu yote kwa njia za mkato.

Serikali ya sasa imeonesha mwanga wa kutaka kufuta tatizo hilo, lakini kwa kweli itachukua muda kwani ulikuwa ni mtindo wa maisha wa baadhi ya Watanzania wengi kwa muda mrefu ukichagizwa na mdudu rushwa.

Rais Dk. John Magufuli, ameweka wazi kwamba hatakubali katika utawala wake kuruhusu watu wasio na sifa kujiunga na elimu ya juu au kusaidiwa kughushi vyeti kwa nia ya kupata kazi au nyadhifa fulani.

Akiwa pale bandarini aliwahi kusikika akisema kuwa bora watumishi wa umma waridhike na vyeti walivyonavyo kwani watapangiwa kazi kulingana na vyeti vyao halali. Rais alisema njama zozote za kutaka kughushi vyeti ili kupata cheo kikubwa zaidi ni kujitakia matatizo na akasema Serikali yake haitawavumilia watumishi kama hao. Bila shaka rais alikuwa akimaanisha kwamba hatomwonea haya mtu yeyote hata akiwa na cheo kikubwa kiasi gani. Hili ni jambo ambalo MTANZANIA tunaliunga mkono kwa dhati.

Tumemsikia Rais akisema hivi karibuni kwamba tayari Serikali imegundua kuwa watumishi 9,000 waliajiriwa kwa vyeti vya kughushi. Tunasema idadi ya watumishi wa umma wasio na vyeti halali inaweza kuwa kubwa zaidi kama uchunguzi ukifanywa kwa kina zaidi na bila upendeleo au kumwonea haya mtu yeyote.

Tunaamini Magufuli ataishughulikia mapema orodha hiyo mara uchunguzi utakapokamilika. Bila shaka walioghushi vyeti si walimu na polisi tu bali pia wamo vigogo wenye nyadhifa kubwa serikalini na kwenye mashirika ya umma.

Ukweli ni kwamba, elimu ni mchakato wa kutafuta maarifa na ujuzi ili kupata moja ya nyenzo za kuboresha maisha. Tatizo linaanza pale baadhi ya Watanzania wanapougeuza mchakato wa elimu kuwa wa kutafuta vyeti ili kujipatia kazi nzuri au kupanda vyeo kwenye utumishi wa umma.

 

Tunapozungumzia kughushi vyeti watu hudhani wahusika ni watu wa kawaida tu. Nina hakika zoezi la kuhakiki vyeti vya shule hasa vile vya kidato cha nne likifanyika kwa uthabiti na bila upendeleo litabaini kuwa wapo pia vigogo ambao vyeti vyao vya elimu vina utata!

Kwa kuwa walimu, polisi, manesi na watumishi wengine hushtakiwa mahakamani pale inapobainika walighushi vyeti basi mamlaka zifuate mkondo huo huo kwa vigogo na watu wengine. Kama kuna wabunge walioghushi vyeti basi nao waanikwe.

Watumishi wasio na sifa ni chanzo cha kukosa ufanisi mahala pa kazi na watu kuishia kuilaumu Serikali nzima. Ni hatari zaidi kama jamii itaendelea kuwafumbia macho watu walioghushi vyeti hasa wale walioko kwenye maeneo nyeti kama hospitali.

Kama kweli wananchi wanataka kupata huduma bora basi yawapasa kuiunga mkono Serikali katika kuwabaini wale wanaoishi kwa vyeti vya rafiki zao, ndugu ama marehemu jamaa zao. Tunaamini zoezi hili litaboresha utendaji mahala pa kazi na kupunguza idadi ya wafanyakazi vilaza.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles