24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mpango wa Brexit wapata pigo jingine Uingereza

LONDON, UINGEREZA

MPANGO wa Waziri Mkuu Theresa May kuhusu kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU), maarufu kama Brexit umepata pigo jipya.

Hali hiyo imekuja baada ya Spika wa Bunge, John Bercow kutangaza kuwa mpango huo hauwezi kupigiwa tena kura bungeni, isipokuwa pale utakapofanyiwa marekebisho makubwa.

Katika tangazo la kushtukiza juzi jioni, Spika Bercow alisema wabunge hawawezi kuupigia kura mpango ule ule walioukataa awali katika msimu huu huu wa Bunge.

Akitumia kigezo cha mwaka 1604, Spika Bercow alisema itakuwa kinyume cha sheria kwa Serikali kuwasilisha tena mpango uliokwishapingwa na wabunge.

Tangazo hilo la Spika Bercow limekuja wakati Serikali ya May inahangaika kuwashawishi wabunge kuukubali mpango huo, ambao tayari wamekwishaupiga chini mara mbili, ikitarajia kuwa ungepigiwa kura tena wiki hii.

Spika Bercow alitoa ufafanuzi kuhusu tangazo lake, akisema hataki lichukuliwe kama kauli ya mwisho kuhusu Brexit, bali kama sharti ambalo Serikali inapaswa kulitimiza, ili yeye aweze kuandaa kura ya tatu bungeni kuamua juu ya mpango huo.

Waziri wa Brexit, Steve Barclay akijibu tangazo la Spika Bercow alisema hiyo inamaanisha hakutakuwa na upigaji kura leo na hivyo Uingereza itachelewa kidogo kuondoka EU.

”Ni uamuzi muhimu ambao bila shaka unahitaji kutazamwa kwa makini. Tutautafakari kwa kina na tutachukua uamuzi ipasavyo,” alisema Barclay.

Chanzo kutoka Serikali ya May kimeliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), kwamba hatua ya Spika Bercow ni ishara kuwa anataka kuchelewesha Brexit kwa muda mrefu, ambapo Bunge litachukua udhibiti wa mchakato mzima likinuia kufikia makubaliano inayotaka na EU.

Waziri Mkuu May alitazamia kuwa mpango wake ungeshinda safari hii iwapo ungepigiwa kura leo kisha kusafiri kuelekea Brussels, Ubelgiji kuomba kucheleweshwa kwa tarehe ya Uingereza kuondoka rasmi EU hadi Juni 30.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles