26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mpango kuwezesha vijana walioshindwa kumaliza shule waja

Na ANDREW MSECHU

ASASI ya Maendeleo ya Jamii (OCODE), inaandaa mpango maalumu wa kuwasaidia vijana wa kiume (wavulana) waliokosa fursa za kuendelea na shule, ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Ofisa Mawasiliano wa OCODE, Martha Chiduo anasema mpango huo unaowachukua vijana na kuwapa stadi za maisha kwa mwaka mmoja unatarajiwa kutekelezwa jijini Dar es Salaam kwa hatua ya awali kisha wataangalia namna ya kuupanua katika mikoa mingine nchini. 

Anasema wamefikia hatua hiyo baada ya mpango wa awali uliosaidia wasichana 344 kufundishwa stadi za maisha kwa miezi tisa na kupatiwa vifaa vya kuanzia maisha kuonyesha mafanikio.

Anasema katika mpango huo uliopewa jina la ‘Bonga’ ikimaanisha ‘Tuzungumze’, wamelenga kusaidia wasichana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 19, ambao kwa sababu mbalimbali wameshindwa kuendelea na shule katika mfumo rasmi, ili waweze kuwa wazalishaji na kupunguza mzigo kwa familia zao.

Anasema wanufaika ni wasichana walioshindwa kumaliza elimu ya msingi na waliomaliza elimu hiyo lakini wameshindwa kuendelea na elimu ya sekondari aidha, kutokana na mimba za mapema, kuolewa na mazingira mengine yanayotokana na ugumu wa maisha.

“Tulianza na mpango wa kuwasaidia wasichana walioshindwa kumaliza shule kupitia mpango maalumu wa Bonga, ambapo tulisajili wasichana 406 kwenye Kata ya Msongole, ambao walipata elimu ya ufundi. Kati yao 344 walifanikiwa kuhitimu baada ya miezi tisa,” anasema Martha.

Anafafanua kwamba katika mpango huo, wasichana hao wamekuwa wakifundishwa stadi muhimu za maisha kwa miezi sita ili waweze kujitambua vyema na kujiamini na kuwajengea moyo wa kujitolea.

Mkurugenzi wa asasi hiyo, Joseph Jackson, anayataja maeneo wanayopatiwa mafunzo hayo kwa miezi sita kuwa ni masuala mtambuka ikiwamo ya jinsia, haki za binadamu, kujitambua, afya ya msingi, kuzijua taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali, pia masuala yanayohusu Ukimwi na VVU.

Joseph anasema kwa miezi mitatu ya mwisho, wasichana hao wamekuwa wakifundishwa ufundi stadi kutokana na kile wanachohitaji kujifunza na wanapewa ujuzi wa kukifanya na kukisimamia, ambapo baada ya mafunzo hupewa vifaa kwa ajili ya kuanza kufanyia kazi stadi hizo.

Anasema stadi wanazopatiwa ni zile za ufundi stadi kwa mujibu wa chaguo la kila mmoja, hasa kwenye maeneo ya ushonaji, uokaji vyakula, kutengeneza nywele, upikaji vyakula kwa ajili ya sherehe na migahawa na upambaji katika sherehe na matukio.

Anasisitiza kuwa nia hasa ni kuwafanya wasichana wajisimamie na kujitegemea katika biashara zinazotokana na stadi hizo, kuwa huru na kuwa watu wanaoheshimika katika jamii zao.

Anasema baada ya kuanza mpango huo kwa mafanikio, kwa sasa wanaangalia namna ya kuwasaidia vijana wa kiume ambao pia wamekosa fursa za kuendelea na masomo kwa sababu mbamlimbali ikiwamo umasikini wa familia, ili waweze kujitegemea kikamilifu.

“Sasa hivi tunaandaa mpango wa kuwasaidia pia wavulana waliokosa nafasi ya kuendelea na shule katika mpango maalumu wa kuwapa elimu ya ufundi kwa miezi 12, ambayo tunaamini itawasaidia kujitegemea katika maisha yao,” anasema.

Usaidizi kwa shule

Joseph anasema hiyo ni sehemu tu ya shughuli za taasisi hiyo, ambayo imekuwa ikisaidia kuendeleza sekta ya elimu nchini katika ngazi ya shule za awali na za msingi hasa kwa shule zilizokuwa zikikosa fursa miongoni mwa shule za serikali.

Anasema asasi hiyo ya OCODE iliyosajiliwa rasmi mwaka 2003 imekuwa ikisaidia kuboresha mazingira ya utoaji elimu ikiwamo miundombinu na kutoa vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule hizo ili kuhakikisha kunakuwapo mazingira rafiki ya kufundishia kwa walimu na ya kujifunzia kwa wanafunzi. 

Anaeleza kuwa pamoja na kuboresha miundombinu, wamekuwa wakijenga, kukarabati majengo ya madarasa na vyoo, kuboresha mifumo ya maji, kununua vifaa ikiwamo vitabu na madawati, kutoa misaada ya vifaa vya kufundishia kwa shule husika.

Anasema kwa sasa tayari shule 13 katika manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam zimeshanufaika na mpango huo, nne katika Manispaa ya Temeke, tano Manispaa ya Ilala na nne Manispaa ya Kinondoni.

Anazitaja shule hizo kuwa ni Buza, Bwawani, Mtoni Kijichi na Kibonde Maji katika Manispaa ya Temeke, Msongola, Yange yange, Nzasa II, Viwege na Tungini katika Manispaa ya Ilala na shule za Tumaini, Kawe A, Bunju A na Mtambani katika Manispaa ya Kinondoni.

“Lakini pia tumekuwa tukijishughulisha na kujenga uwezo kwa kutoa mafunzo ya walimu kazini kwa kuwasaidia kuongeza mbinu za ufundishaji na kujenga uwezo kwa walimu wa masomo maalumu,” anasema.

Anaongeza kuwa wamekuwa pia wakitoa mafunzo kwa kamati za shule kuziwezesha kutambua wajibu na majukumu yao na namna wanavyoweza kutumia nafasi yao kuunganisha uongozi wa shule, wazazi na wanafunzi katika kudai stahiki zao serikalini.

Anasema kwa sasa wanalenga pia kuwawezesha wazazi wenye wanafunzi katika shule wanazozisaidia ili wapate uwezo wa kuongeza kipato cha familia na kuwasaidia watoto wao waweze kuendelea na shule.

Anasema hiyo iko chini ya mpango maalumu wa kuwezesha maisha chini ya utaratibu uliopewa jina la Community Managed Microfinance (CMMF) wenye lengo la kuwapa elimu ya masuala ya kifedha na mikopo watu walio kwenye jamii zilizokosa fursa.

Anasema walengwa hasa wa mpango huo ni wanawake na vijana katika maeneo ambayo wanasaidia miradi ya elimu hasa kwa nia ya kuwajengea uwezo wa kujiunga katika vikundi, kuzalisha fedha kwa wiki na kupata uwezo wa kukopa kwa vikundi, hatua inayowasaidia kuongeza kipato.

Anaeleza kuwa tayari wana vikundi 50 ambavyo vimeshafikisha wanachama zaidi ya 1000 katika maeneo ambayo taasisi hiyo imefika, hatua ambayo wanaona itakuwa na msaada mkubwa kwa wanafamilia.

Anasema mpango huo pia unahusisha utoaji wa elimu ya kijitambua na ya ujasiriamali lengo likiwa ni kuhakikisha familia zinakuwa na uhakika wa kipato kwa ajili ya kuwasaidia watoto wao. 

Mpango wa vijana

Anasema OCODE pia ina mpango maalumu wa kuwaunganisha vijana ulioanza mwaka 2006, unaowapa vijana nafasi ya kukuatana kila Alhamisi kwa ajili ya kujadiliana kuhusu maisha yao, changamoto zinazowakabili na kupanga kwa pamoja namna ya kuisadia jamii ikiwamo usafi wa mazingira na shughuli za kujitolea.

“Lengo la mpango huu ni kuwapa ufahamu wa sera zinazowahusu vijana nchini, kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto za vijana ikiwamo afya, elimu, ushirikiano wao na suala zima la ajira, pia kuna namna ya kukabuliana na changamoto hizo.

Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Magreth Kuhulla, anasema unahusisha pia kuwaendeleza vijana na kuwapa uwezo wa kujiajiri, kwa kuwa miongoni mwa washiriki wengi ni wachezaji wa mpira wa miguu, wanatumia pia fursa hiyo kujadili masula ya michezo,” anasema.

Magreth ambaye baada ya kushiriki mpango huo nchini Norway na kurejea hapa nchini ambapo anaendelea kujitolea, anasema kwa sasa OCODE inashirikiana na Stromme Foundation ya Norway ambayo pia imekuwa ikisimamia mpango huo wa kubadilishana vijana kupitia mpango maalumu wa ‘Act Now’, unaowapa vijana maalumu stadi za uongozi.

“Kupitia mpango huo, tunabadilishana. Vijana kutoka nchini wanatembelea Norway na kujifunza kwa miezi kumi wakati vijana kutoka Norway wanakuja nchini na kujifunza kwa miezi sita. Katika kipindi hicho wanakuwa wakifanya kazi za kujitolea chini ya mradi maalumu wa Stromme. Mpango huu unalenga zaidi ushirikiano wa kimaendeleo, ukiangalia zaidi kuhusu umasikini na namna ya kuutokomeza,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles