23.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

MPANGO KABAMBE WA MAJI WAHITAJIKA NCHINI

Bwawa la Nyumba ya Mungu Kilimanjaro

 

Na LEONARD MANG'OHA,

MIONGONI  mwa changamoto inayowakabili wananchi wa maeneo mbalimbali nchini ni ukosefu wa maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku na shughuli za kiuchumi.

Maeneo mengi ya nchi upatikanaji wa maji umeendelea kuwa tatizo na kikwazo kwa  shughuli mbalimbali za maendeleo kutokana na wananchi kutumia muda mwingi kutafuta bidhaa hiyo muhimu zaidi maishani.

Mijini hata vijijini kote hali ya upatikanaji wa maji si yenye kuridhisha japo kwa kiasi fulani maeneo ya mijini kuna unafuu kiasi Fulani, lakini huko vijijini hali si ya kuvumilika kwani katika baadhi ya maeneo hakuna tofauti kati ya wanyama na binadamu wote hujikuta wakitumia chanzo kimoja cha maji, ambapo wananchi hulazimika kutumia maji yanayotumika kunyweshea mifugo.

Kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za uzalishaji ni kama kuhujumu uchumi kwani Tanzania si miongoni mwa nchi zenye uhaba wa maji kama ilivyo nchi nyingi za Afrika hususani zilizo katika jangwa.

Tanzania ina vyanzo vya maji baridi yanayofaa kwa matumizi ya binadamu na shughuli nyingine za kilimo vinavyofikia kilomita za mraba 54,277, ambayo ni maziwa makuu matatu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa.

Yapo pia maziwa madogo yapatayo 29 kama vile Natron, Eyasi na mengineyo mengi, ipo mito na maeneo oevu karibu kila pembe ya nchi.

Tatizo lililopo ni kushindwa kusambazwa kwa maji haya katika maeneo mengi ya nchi hususani yenye uhitaji mkubwa wa maji na maeneo ya uzalishaji.

Binafsi sioni sababu ya kukosekana kwa maji ya uhakika katika mikoa kama vile Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Kigoma na Mara ambayo imegusa moja kwa moja katika vyanzo vya maji kama vile ziwa Viktoria na Tanganyika.

Pamoja na maeneo haya kuwa katika eneo hili, bado wakazi wake hawana uhakika wa kupata maji safi na salama hususani katika maeneo ya pembezoni mwa miji.

Katika miaka ya hivi karibuni, Serikali ilitekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Viktoria kwenda Kahama hadi Shinyanga ambao pia umewezesha kutoa huduma ya maji katika vijiji 58 vilivyopitiwa na mradi.

Lengo la mradi huo uliogharimu Sh bilioni 242 ambazo ni fedha za ndani ulilenga kufikisha maji katika migodi mbalimbali ya madini iliyopo mkoani Shinyanga, kurahisisha uendeshaji shughuli katika migodi hiyo ambayo imekuwa nguzo kuu ya uchumi katika mkoa huo.

Mradi huu unaelezwa kuwa na uwezo wa kuhudumia watu wapatao zaidi ya laki nne, ukiwa na uwezo wa kutoa maji kiasi cha mita za ujazo 80,000 kwa siku, huku ukitegemewa kuongeza usambazaji wa maji hadi kufikia mita za ujazo 120,000 na kuwafikia watu milioni moja ifikapo mwaka 2025.

Iko miradi kadhaa ambayo Serikali imekuwa ikitekeleza katika maeneo mengi nchini ukiwamo ule wa Kidunda unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 300.

Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi, anasema maji ni kitu muhimu katika mchakato wa kuendesha shughuli yoyote; iwe ya kijamii au hata ya kiuchumi.

Anasema katika wakati huu Taifa linapopambana kuelekea uchumi wa viwanda, mahitaji ya maji ni makubwa katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali katika sekta hiyo.

Viwanda vya vinywaji, nguo, katani na migodi mbalimbali ni maeneo yatakayokuwa na uhitaji mkubwa wa maji ili kujiendesha.

Anasema ikiwa hakutakuwa na maji ya uhakika itasababisha bidhaa zinazozalisha kuuzwa kwa bei ya juu, hivyo kushindwa kumudu ushindani katika soko dhidi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

Anaamini kuwa viwanda vingi nchini vitakuwa ni vile vinavyotegemea malighafi za kilimo kufanya uzalishaji, hivyo maji yanahitajika kuwezesha kilimo endelevu kisichotegemea mvua za misimu ili kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kutosha.

Profesa Damian Gabagambi ni Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, anasema ikiwa hayatapatikana maji ya uhakika uchumi wa viwanda ni ndoto.

Anasema mahitaji ya maji katika viwanda ni makubwa hivyo ni lazima kuhakikisha upatikanaji wa maji ya kutosha kwa matumizi ya viwanda.

“Mfano kiwanda cha mkonge kinatumia kati ya lita 36,000 hadi 50,000 kwa saa, viko viwanda vingapi na vinahitaji maji kiasi gani na viwanda vya aina nyingine pia vinahitaji maji. Shida ni kuwa maji hayo hayarudishiwi kutumika tena yaani ‘recycle’.

Nikubaliane na wewe kuwa vyanzo vya maji tulivyonavyo havijatumika kuhakikisha maji yanasambazwa katika maeneo mbalimbali na watu wakaweza kuyatumia kuzalisha mazao ya kilimo ambayo naamini yatategemea zaidi kilimo,” anasema Profesa Gabagambi.

Anasema bado hakuna mipango mizuri ya kuvuna maji yanayotokana na mvua ili yatumike kwa matumizi mbalimbali na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya maji vya asili ambavyo anasema vimekuwa vikipungukiwa maji si tu nchini bali duniani kote.

Cha ajabu ni kuwa maji kama rasilimali hutumiwa vibaya kama vile hakuna shida kuyapata na hakuna anayejali umuhimu wake.

Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Makampuni ya Said Salimu Bakharesa and Company Limited, Husein Ally, anasema kati ya viwanda vyote vya kampuni hiyo ndicho pekee kimeunganishwa na maji kutoka idara ya maji ya Jiji la Dar es Salaam.

Anasema wamelazimika kutumia maji ya visima walivyochimba wenyewe ili kuwezesha uzalishaji.

Mtaalamu wa Umwagiliaji kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Andrew Tarimo, anasema: “Tunapaswa kuelewa maji tuliyonayo si mengi kama wengi wanavyofikiria kutokana na kupungua kwa kina cha maji karibu katika vyanzo vyote.

Anasema ili kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji cha uhakika, ni vema kufahamu kiwango cha maji kilicho ardhini (ground potential water) ambacho kinaweza kutumika kwa umwagiliaji na si maji yanayotiririka.

Anasema kutegemea maji kutoka vyanzo kama vile Ziwa Viktoria kunahitaji gharama kubwa kusukuma kwenda katika maeneo ya uzalishaji hivyo kutumia maji yanayopatikana ardhini ni njia pekee inayoweza kuleta tija katika kilimo.

“Ni lazima tuwekeze kwenye ‘ground potential water’ na kuwapo kwa usimamizi wa maji ambao bado ni mgogoro kwani katika maeneo mengi utaona ni jinsi gani watu wanachimba visima karibu na vyoo bila kuzingatia sheria. Siamini kuwa wanapata ushauri wa kitaalamu,” anasema Profesa Tarimo.

Anasema kwa sasa mvua zimepungua katika maeneo mengi nchini ambapo huanza kwa kuchelewa na kumalizika kwa wakati ule ule kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Anatolea mfano Wilaya ya Mbarali kuwa wananchi wa eneo hilo walikuwa wakiotesha mpunga kuanzia Novemba na walitegemea zaidi mvua za misimu, lakini kwa sasa hali imebadilika ambapo wakulima wamekuwa wakichelewa kuotesha mpunga na kulazimika kuchimba visima kumwagilia mashamba hayo.

Anasema kwa sasa Tanzania inaweza kwenda Afrika Kusini kuomba msaada wa chakula ikiwa imekumbwa na upungufu wa chakula kutoka nchi zisizo na mvua nyingi kama Afrika Kusini.

Anasema wastani wa mvua kwa nchi hiyo ukitoa Mji wa Cape Town, ni milimita 400 kwa mwaka, wakati maeneo yanayopata kiasi kidogo sana cha mvua nchini mikoa ya Dodoma na Singida wastani wake wa mvua kwa mwaka ni mm 600.

Anasema wakulima wengi wamekuwa wakifikiria zaidi kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa na mabwawa makubwa ambayo si rahisi kuyapata kutokana na kugharimu fedha nyingi kuyajenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,293FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles