MOURINHO: RONALDO KURUDI UNITED HAIWEZEKANI

0
549

MANCHESTER, ENGLAND


KOCHA wa Klabu ya Manchester United, Jose Mourinho, ameweka wazi kuwa hana mpango wa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

Kocha huyo amesema kwamba, haiwezekani kwa upande wake kumsajili Ronaldo, kwa kuwa hayupo kwenye mipango yake ndani ya kikosi hicho.

Ronaldo alihusishwa kutaka kujiunga na kikosi chake hicho cha zamani mara baada ya tuhuma ya ukwepaji kodi nchini Hispania. Mchezaji huyo aliweka wazi kuwa hana mpango wa kuendelea kuwa na kikosi hicho msimu ujao, hivyo lazima aondoke.

Ronaldo, mwenye umri wa miaka 32, aliwahi kucheza soka katika klabu ya Manchester United kwa misimu sita na kufanikiwa kupata mataji matatu ya Ligi Kuu na taji la Klabu Bingwa Ulaya, kabla ya kujiunga na Real Madrid, ambapo huku nako alifanya kazi na Mourinho, lakini hawakuwa na maelewano mazuri hadi Mourinho anaondoka.

Kuhusishwa kwa Ronaldo kutaka kujiunga na Manchester United kuliwapa mashabiki maswali mengi, kwamba mchezaji huyo ataweza kufanya kazi tena na Mourinho ambaye alikuwa na mgogoro naye.

“Manchester United haipo kwenye mipango yoyote ya kuitaka saini ya Ronaldo kwa kipindi hiki cha majira ya joto. Tunajua Ronaldo ni mchezaji bora ndani ya kikosi chake cha Real Madrid na tunaamini ataendelea kuwa hapo.

“Kama ana mipango ya kutaka kuondoka Madrid inawezekana, lakini kwa upande wetu hatujafikiria kumleta kikosini. Siwezi kupoteza muda wangu kumfuatilia mchezaji ambaye hayupo kwenye mipango yetu na haiwezekani kumsajili,” alisema Mourinho.

Ronaldo, ambaye ni raia wa nchini Ureno, wakati anakipiga katika kikosi cha Manchester United aliwahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi mara nne mfululizo, huku akitwaa mara mbili uchezaji bora wa mwaka, kabla ya kuchukua tuzo ya kiatu cha dhahabu msimu wa 2007-08, baada ya kufunga mabao 31 katika michezo 34 ambayo alicheza.

Staa huyo kwa sasa anashika nafasi ya pili kwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or, huku akichukua mara nne, wakati Lionel Messi wa Barcelona akiongoza kuchukua mara tano.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here