CHELSEA hatimaye imefikia uamuzi mgumu kabisa wa kumtimua kocha wao kipenzi, Jose Mourinho ikiwa ni miezi saba tu tangu kocha huyo aimbiwe wimbo wa kishujaa baada ya kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa England.
Uamuzi wa Bodi ya Chelsea umetangazwa jana jioni na umeelezwa kuchangiwa na matokeo mabaya ya timu hiyo katika Ligi Kuu ya England (EPL) msimu huu, ambapo timu hiyo inashika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 15 kutokana na michezo 16 iliyocheza.
Kufungwa na vinara wa ligi hiyo Leicester City mabao 2-1 na kuwafanya wawe nyuma kwa pointi 20 nyuma ya timu hiyo, kulimfanya mmiliki wa Chelsea, Roman Abromovic kuitisha kikao cha bodi ambacho kwa pamoja kilifikia uamuzi mgumu licha ya malalamiko ya kocha huyo aliyoyatoa kwamba anahujumiwa na wachezaji wake.
Mara tu baada ya uamuzi huo wa Bodi ya Chelsea kutangazwa, tayari majina manne ya makocha nguli wa soka barani Ulaya yametajwa katika kikao hicho kizito yakihusishwa na kuchukua nafasi ya Mreno huyo maarufu kwa jina la The Special One.
Makocha wanaotajwa ni pamoja na Diego Simeone raia wa Agentina anayeifundisha timu ya Atletico Madrid ya Hispania, Pep Guardiola wa timu ya Bayern Munich ya Ujerumani, Carlo Ancelotti ambaye ni kocha huru na Ronald Koeman ambaye ni kocha wa Southampton.