27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mourinho: Afcon itampa Salah Ballon d’Or

LONDON, ENGLAND

ALIYEKUWA kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, ameweka wazi kuwa, nyota wa Liverpool, Mohamed Salah anaweza kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or msimu huu endapo atafanikiwa kutwaa taji la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Salah amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Jurgen Klopp ndani ya Liverpool kwa kipindi cha misimu miwili mfululizo, mchezaji huyo amefanikiwa kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu England mara mbili mfululizo, huku msimu wa 2017-18 akitajwa kuwa mchezaji bora wa England.

Katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu aliweza kufunga bao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Tottenham na kuifanya Liverpool kuwa mabingwa mara sita wa Kombe hilo.

Kwenye tuzo za Ballon d’Or, tangu mwaka 2008, mshambuliaji wa Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi na nyota wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo wamekuwa wakitawala tuzo hiyo, lakini mwaka jana walikutana na ushindani mkubwa kutoka kwa nyota wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia, Lukas Modric ambaye alitwaa tuzo hiyo.

Lakini Mourinho anaamini Salah ambaye amewahi kuwa mchezaji bora wa Afrika mara mbili, msimu huu anaweza kutwaa tuzo hiyo kama ataweza kuisaidia timu yake ya taifa Misri kuchukua taji la Afcon.

Michuano hiyo inatarajia kuanza kutimua vumbi Juni 21, huku Misri wakiwa wenyeji wa michuano hiyo na wanapewa nafasi kubwa ya kuwa mabingwa kwenye ardhi ya nyumbani.

“Kama Salah anataka kuwa mchezaji bora wa dunia katika tuzo za Ballon d’Or basi ni lazima apambane kuhakikisha anatwaa taji la Mataifa ya Afrika.

“Michuano hiyo inatarajia kufanyika huko nchini Misri, hivyo lazima ahakikishe anaipigania timu yake kuweza kufanya vizuri kwenye ardhi ya nyumbani,” alisema Mourinho.

Timu ya taifa ya Misri ipo kundi A, ambapo katika kundi hilo kuna timu kama vile Zimbabwe, DR Congo na Uganda, mchezo wao wa kwanza utapigwa dhidi ya Zimbabwe, Juni 21, jijini Cairo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles