24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Moto wawaka sekta ya madini

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MOTO umewaka katika sekta ya madini baada ya uhakiki kubaini kuwa leseni 18,341, hazijalipiwa ana na kwa ujumla wake zinadaiwa Sh. bilioni 116.67.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko, ameagiza pia kusimamishwa kazi kwa watumishi watano waliotoa leseni za uchimbaji mdogo wa madini kwa watu ambao sio Watanzania jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Jijini hapa, alisema kuna baadhi ya maeneo yalitengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo likiwemo eneo la Melela Demarcated Mkoani Morogoro ambapo leseni zimetolewa bila kufuata taratibu.

Biteko aliagiza wahusika  watatu waliohusika ambao hakutaka majina yao yaandikwe  wasimamishwe kazi na hatua za kinidhamu zichukuliuwe.

“Katibu Mkuu kama ambavyo mimi na wewe tuliagizwa waziwazi na Rais John Magufuli Januari 22, pale Dar es Salaam kuhusu kusafisha wizara kama ambavyo tayari ulishafanya kwa wale zaidi ya 60.

“Hawa nao wawajibishwe leo (jana) haiwezekani tutenge maeneo kwa wachimbaji wadogo, wao wakafanye wanavyojisikia wao kwa tamaa zao hatutawavulimia,”alisema Waziri Biteko.

Waziri Biteko alisema wafanyakazi wengine wawili waliosimamishwa ni wale waliotoa leseni kwa raia wa kigeni

Waziri huyo alisema kifungu cha 8(2) cha sheria ya madini mwaka 2010 na marekebisho yake mwaka 2017 kinakataza leseni ndogo za uchimbaji kutolewa kwa wageni lakini cha ajabu leseni 17 zimetolewa kinyume.

Hata hivyo leseni namba PML003227NZ, PML003387NZ, PML003427NZ zimetolewa kwa mtu ambaye siyo mtanzania (Raia kutoka Kenya) lakini pia maombi yake namba PML12823/NZ, PML13036/ZN, PML13066/NZ, PML14632/NZ, PML23158/NZ, PML23159/NZ, PML25398/NZ, PML25786/NZ na PML25789NZ yapo katika hatua mbalimbali ya kupatiwa leseni  kinyume cha sheria kwa watu ambao siyo Watanzania.

”Naiagiza tume ya madini kufuta leseni 17 zilizotolewa na maombi hayo mara moja na wahusika wote walioshiriki katika utoaji leseni hizo wawili ambao hakutaka majina yao kutajwa wasimamishwe kazi na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za utumishi kuanzia leo,”alisema Waziri Biteko.

UHAKIKI WA LESENI

Waziri Biteko alisema katika uhakiki wa leseni matokeo yameonesha kwamba hadi kufikia Februari 2019, leseni 18,341 kati ya 30,973 ambazo zipo hai zinadaiwa sh. bilioni 116.67

Alisema  leseni za utafiti Sh. bilioni 61.67, za uchimbaji mkubwa Sh. bilioni 6.41, uchimbaji wa kati sh. bilioni 28.28 na uchimbaji mdogo Sh. bilioni 19.51.

“Kwa kuwa leseni za utafiti 110 na za uchimbaji wa kati 52 zilikuwa tayari zimeshapewa hati za makosa, naiagiza tume ya madini kufuta leseni hizo ndani ya siku saba na ziandikiwe hati za madai mara moja

“Wakishindwa kulipa madeni hayo ndani ya siku 30 wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kifungu cha 93 cha sheria ya madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017,”alisema.

Aidha, aliiagiza tume hiyo kuziandikia hati za makosa leseni zote 18,341 zinazodaiwa ili zilipe madeni ndani ya siku 30, wakishindwa kulipa leseni zifutwe na ziondolewe kwenye mfumo ndani ya siku saba baada ya mwisho wa hati ya makosa kwa mujibu wa kifungu cha 63 cha sheria hiyo.

ATAKA STAMIKO  WALIPE ADA

Katika hatua nyingine Waziri Biteko ameliagiza Shirika la Madini la Taifa (Stamico) linalomilikiwa na Serikali  kulipa ada ya kila mwaka kama ilivyo watu wengine.

“Sasa hapa nafahamu kuwa zipo leseni nyingine zinamilikiwa na Serikali kupitia Stamiko wanamiliki, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), nafahamu kwamba hata ile leseni ya NDC ya Liganga na Mchuchuma  ukienda kule wanakuambia mradi umeanza  lakini hakuna kinachoendelea.

“Wamehodhi maeneo hakuna mtu anayeweza kuomba kule akapewa, wapo wawekezaji wengi wana uwezo wanataka kufanya kazi lakini kitu kinachotia aibu hii leseni ya NDC na mbia mwenzake yenyewe peke yake inadaiwa Dola za Marekani 375,000 ada ya mwaka hawalipi wapewe hati za makosa ‘Default notice’ bila kuangalia sura.

Alisema haiwezekani wanawabana wananchi wa kawaida na kuiacha Serikali kupitia Stamico ikishindwa kulipa.

“Haiwezekani tunawabana wananchi wa kawaida halafu leseni zinazochukuliwa na Serikali kupitia makampuni yake zenyewe zina enjoy tuu kwakuwa sheria hii haijambagua mtu hata NDC wapelekewe,”

“Na mimi nitaona fahari sana nikifuta hii leseni, tutakuwa tunapeleka ujumbe kwamba hatuonei mtu wala hatupendelei mtu maana wapo watu wengi wana uwezo wa kufanya kazi kama hawawezi wapelekee hati za makosa ‘Default notice’ kwa siku 30 hizo leseni zote futa tutafute mwekezaji mwingine ambaye yupo makini ‘Serious,”alisema Waziri Biteko.

 UCHENJUAJI ENEO MOJA

Waziri huyo alisema kuwa kumekuwa na tabia ya wachimbaji hasa wadogo kujenga mitambo ya kuchejua dhahabu bila kufuata taratibu na kwamba hadi kufikia Februari, mitambo takribani 639 haikuwa na leseni.

“Hali hiyo imekosesha Serikali jumla Sh. bilioni 1.76 zitokanazo na ada ya maombi na ya mwaka ya mitambo.

Alisema kutokana na hali hiyo Serikali itatenga eneo moja kwa ajili ya kuchenjua madini ili kuiwezesha Serikali kupata mapato.

APIGA MARUFUKU UTOAJI WA LESENI MPYA

Vilevile Biteko amepiga marufuku  Tume ya madini kutoa leseni mpya kwa kampuni au mtu binafsi aliyepewa hati ya makosa na kushindwa kurekebisha makosa hayo kwa kuwa ni kinyume na kifungu cha 31(b) cha sheria ya amdini 2010 na marekebisho yake 2017.

Alisema kuna baadhi ya watu na makampuni yamekuwa yakiomba leseni nyingi za utafiti na uchimbaji wakati hawana uwezo  wa kuyafanyia kazi huku akitolea mfano Christopher Eliofo na kampuni yake ya Ntoku Limited wenye maombi ya leseni zaidi ya 700 katika maeneo mbalimbali nchini na ameshindwa kulipia hata ada ya maombi.

“Kitendo hiki kinawanyima haki watu wengine bila sababu za msingi na mtu huyu amekuwa akiingilia maeneo ya watu wengine na kusababisha migogoro isiyokuwa ya lazima.

“Naagiza tume ya madini kufuta maombi ya leseni za watu au makampuni yote ambayo yameshikiliwa bila sababu na kuandaa utaratibu wa ukomo wa leseni kwa mtu au kampuni moja,”alisema.

Aliwaasa wachimbaji wote nchini hasa wadogo kuomba leseni katika maeneo yatakayoachwa wazi ili kujiepusha na uchimbaji usio rasmi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles