27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MOTO WATEKETEZA MIZIGO JNIA

JKNIA

Na ASHA BANI

MOTO mkubwa umezuka katika chumba cha mizigo ya abiria ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kuteketeza mizigo yote.

Moto huo ulitokea saa tano usiku wa kuamkia jana katika uwanja huo na kuteketeza mizigo yote iliyokuwa katika chumba kinachomilikiwa na Kampuni ya Swissport huku Serikali ikilazimika kuunda tume kuchunguza chanzo chake.

Baada ya moto huo kutokea ilimlazimu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Professa Makame Mbarawa, kukatisha ziara yake ya kikazi na kurejea haraka Dar es Salaam kwenda kuona athari za moto huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana uwanjani hapo, Profesa Mbarawa, alisema hataki kusikia taarifa za kwamba ni mapenzi ya Mungu bali anataka kufahamu ukweli wa chanzo cha moto huo ulioleta hasara.

Baada ya ukaguzi wa chumba hicho kilichokuwa na majivu ya mizigo iliyoteketea, alisema tume aliyoiunda ina watu 12 na itaongozwa na Joseph Nyahende kutoka ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).

Alisema anatarajia kupata ripoti ya kitaalamu kutoka kwa tume hiyo itakayosaidia kubaini kiundani juu ya chanzo hasa kilichosababisha moto huo.

“Sitarajii kusikia moto umesababishwa na Mungu, hakuna moto unaotokana na sababu hiyo, kila moto una chanzo chake na aliyesababisha hivyo nitaweza kuwaelewa kama mtanipa sababu,” alisema.

Kuhusu kuendelea na shughuli za usafiri ndani ya viwanja hivyo, Profesa Mbarawa, alisema zinaendelea kama kawaida ambapo awali zilisitishwa na kuhamishiwa katika jengo la kwanza la abiria (terminal one).

Alisema baada ya moto kutokea walichofanya cha kwanza ni kuudhibiti ili usiweze kusambaa katika maeneo mengine ambayo hayajaathirika na kisha kukatafutwa njia za kurudisha huduma kwa abiria.

Naye Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha, alisema bado hawajafanya tathmini na gharama za mizigo iliyokuwa imehifadhiwa katika chumba hicho hadi hapo watakapokamilisha uchunguzi.

Katika hatua nyingine, Mbarawa, ameitaka Swissport kutambua kuwa Serikali ipo makini na inafahamu shughuli zake.

Pia aliipa miezi miwili kujitafakari kama ina uwezo wa kuendelea kutoa huduma kama inavyotakiwa huku akiwa anapitia mkataba wao kama utakuwa unakiukwa.

“Miezi miwili ya kujitafakari na mkataba wenu naupitia kama mnaukiuka nawafutia leseni yenu haraka,” alisema.

Pia alisema kwa kipindi cha muda mrefu Swissport imekuwa ikifanya fitina kwa kampuni mwenza aliyepewa kibali na Serikali kushindwa kufanya kazi.

Alisema kulikuwa na mchakato wa kupata kampuni nyingine ya kuendesha shughuli za mizigo na ikapatikana ya Nas Airco–Dar lakini inashindwa kuendelea na kazi.

“Kutokana na hilo basi naendelea kufanyia kazi taarifa hizo na endapo zikibainika kuwa na ukweli sitaivumilia Swissport, nitahakikisha nachukua hatua stahiki,” alisema.

Pia alisema kabla ya kutokea kwa moto huo aliwahi kupanga kukutana na Swissport lakini akapata taarifa kuwa viongozi wote wako likizo akasitisha.

“Kama mnataka kuendelea na huduma zenu ziwe nzuri basi endeleeni, lakini kila kukicha mmekuwa ni watu wa kulalamikiwa jambo ambalo halipendezi na mnawanyima imani wateja wenu,” alisema.

Profesa Mbarawa alisema anafahamu sheria iliyopo inawapa kiburi kwa kuwa wakionekana na hatia katika utoaji huduma watalipa Dola 5,000 za Marekani.

Alisema anajiandaa katika Bunge lijalo atafanya kila liwezekanalo kupeleka muswada wa dharura ili baadhi ya sheria zirekebishwe kuendana na wakati.

Akizungumza kwa ufupi kuhusu madai hayo, Mkurugenzi wa Swissport, Mrisho Yasini, alisema ameyapata malalamiko hayo kwa mara ya kwanza, hivyo atayafanyia kazi na kuyatolea ufafanuzi kwa vyombo vya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles