Na Khelef Nassor, Zanzibar
MOTO umeteketeza hoteli ya Kitalii ya Konokono Beach Resort iliyopo Kijiji cha Michamvi Mkoa wa Kusini Unguja na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 400.
Hoteli hiyo inayomilikiwa na mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar, Amina Karume, iliteketea jana kwa moto huo ambao chanzo chake ni vijana wawili waliokuwa wakichoma majani jirani na hoteli hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu moto huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saadi, alisema moto huo umeteketeza hoteli hiyo inayomilikiwa na wawekezaji watatu akiwamo mwekezaji mzalendo, Amina Karume na Wataliani wawili, ambao ni Andrea Schampo na Luca Gambirula.
Alisema moto huo umeteketeza nyumba tatu na mgahawa mmoja ndani ya hoteli hiyo.
Kamanda Saadi, alisema baada ya kupata taarifa za moto huo, jeshi la polisi kwa kushirkiana na kitengo cha Zimamoto, waliwahi katika eneo la tukio na kuuzima.
Alisema chanzo cha moto huo ni watu wawili waliokuwa wakichoma majani ambao ni Meshak Amos Elisha (50) na Mohammed Abdalla Hassan.
Alisema watu hao walikuwa wakichoma majani hayo katika eneo la hoteli hiyo na Zamzam Maalim Rashid, mkazi wa Dar es Salaam.
“Wakati wa kuchoma moto ndani ya uzio huo, ulizuka upepo mkali majira ya saa tano na nusu na ukasababisha moto ule kuruka juu na kusababisha nyumba moja ya makuti karibu na hoteli ile kuungua moto na kusababisha hasara hiyo,” alisema Kamanda Saadi.
Hata hivyo, aliwataka wananchi kupuuza taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa kwa kulihusisha tukio hilo na masuala ya siasa.
Vipeperushi vyazagaa
Katika hali ya kushangaza jana mjini wa Unguja, vipeperushi vilionekana katika maeneo mbalimbali ambayo kuna wafuasi wa CUF.