27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

MOSES MKANDAWILE: Mkongwe aliyegeukia ujasiriamali (2)

NA HENRY PAUL

WIKI iliyopita SPOTI KIKI Jumatatu, lilitoa makala sehemu ya kwanza ya golikipa mahiri wa zamani wa Simba na timu ya Taifa Stars, Moses Mkandawile ambaye alikuwa anazungumzia kwa kifupi shughuli anazofanya hivi sasa baada ya kustaafu kucheza soka la ushindani miaka ya nyuma.

Pia katika makala hiyo, Mkandawile ametoa ushauri kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuwanoa waamuzi watakaochezesha ligi mbalimbali msimu huu wa 2016/2017 kufuata sheria 17 za soka ili kuondoa hali ya kuvurunda. Sasa endelea na makala haya ya leo kujua mengine mengi zaidi.

Akiwaasa wachezaji watakaocheza ligi mbalimbali msimu huu kuanza kujiandaa vizuri ili waonyeshe viwango vyao ambavyo vitafanya michuano iwe na msisimko na ushindani, Mkandawile anawapa ushauri akisema:

“Misimu iliyopita wapenzi wa soka nchini walishuhudia ligi zetu nchini hususani ligi kuu kutokuwa na msisimko na ushindani moja ya sababu ni kutokana na kwamba wachezaji wetu hawajiandai vizuri kukabiliana na michuano hiyo.

“Laiti kama wachezaji wangekuwa wanajiandaa vizuri na kufuata maelekezo ya walimu wao tungeshuhudia viwango vikubwa vya soka vikionyeshwa huku ligi zikiwa na ushindani mkubwa na ingekuwa ni vigumu kubashiri mshindi.

“Lakini kutokana na baadhi ya timu kutojiandaa vizuri huzipa nafasi kubwa timu zinazojiandaa vyema kuweza kuibuka na ushindi ambapo mchezo unachezwa upande mmoja tu na ni rahisi mno kubashiri mshindi.

“Hivyo kuondoa hali hii ni vyema timu zijiandae vizuri kusudi ushindani uonekane na wapenzi wa soka nchini washuhudie viwango vizuri vya soka vikionyeshwa na timu zote zinazoshiriki ligi na si kwa baadhi ya timu tu.

“Pia kwa upande mwingine nawashauri viongozi wa klabu kwa kushirikiana na makocha katika kusajili wachezaji kuweka kipaumbele wachezaji wazawa wenye viwango vizuri kuliko kukimbilia kusajili wachezaji kutoka nje ambao baadhi yao viwango vyao vya soka havitofautiani na wachezaji walionao.

“Kwa kuwapa kipaumbele wachezaji wazawa wenye viwango vikubwa vya soka kutaifanya timu yetu ya Taifa Stars kuwa nzuri, kwani baadhi yao watachaguliwa kuchezea timu hiyo ambapo kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kuinua kiwango chetu cha soka ambacho hivi sasa kinaonekana kusuasua.

“Pia tabia ya kuwapa kipaumbele wachezaji wa kigeni na kuacha wachezaji wetu wazawa ni kupoteza pesa nyingi, kwani wachezaji hawa kutoka nje wanapewa fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwa matumizi mengine.

“Pamoja na viongozi wa klabu kuwapa kipaumbele wachezaji wazawa, pia hivi sasa ni wakati mwafaka kwa viongozi hao kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo, kwani hao ndio wanaweza kuinua kiwango cha soka letu kuliko wachezaji wenye umri mkubwa.

“Kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo ndiyo njia pekee na sahihi ambayo inainua kiwango cha soka, kwani nchi nyingi duniani zinatumia njia hii na zimekwishaachana siku nyingi kuwategemea wachezaji wenye umri mkubwa.

Mkandawile anamalizia kwa kuungana na wadau wengi wa soka wanaosema kuwa pamoja na kuwekeza soka kwa vijana wenye umri mdogo, pia ni vyema Shirikisho la soka nchini kwa kushirikiana na klabu, wadau wa soka kuanzisha shule nyingi za kufundishia mchezo huu wa soka ‘academies’, kwani ndiyo njia mojawapo inayoweza kutunasua kutokuwa kichwa cha mwendawazimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles