21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 16, 2022

Morogoro waanza kampeni kusajili watoto

Ashura Kazinja-Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, amewataka wananchi mkoani hapa kuhakikisha kila mtoto chini ya miaka mitano anasajiliwa kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na kupewa cheti cha kuzaliwa.

Alitoa rai hiyo jana kwenye ufunguzi wa kampeni ya usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano. 

Aliwataka viongozi  wa mkoani humo kuhakikisha wasajili hawaweki urasimu wa aina yoyote kama kudai fedha kwa wananchi ili huduma hiyo isigeuzwa mradi wa kujipatia kipato kwa mtu binafsi.

 “Wananchi wa Morogoro tubadilike na kujenga utamaduni wa kufuata mambo muhimu mapema, tuchukue nyaraka zetu zote muhimu za utambulisho ikiwemo vyeti vya kuzaliwa watoto mapema na kuzitunza vizuri ili tuepuke kuwa watu wa matukio” alisema Sanare.

Naye Mtendaji Mkuu RITA, Emmy Hudson, alisema hali ya usajili nchini na utunzaji wa kumbukumbu bado hauridhishi, hivyo kusababisha Serikali kukosa takwimu muhimu kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya taifa kama vile afya, elimu na maendeleo ya jamii.

“Bila kujua idadi ya wananchi ambao inao serikali haiwezi kutoa huduma kwa ufanisi, lakini maswala ya utawala bora hayawezi kufanikiwa, pia kwa mwananchi mmoja mmoja nyaraka hii ni muhimu kama utambulisho na katika upatikanaji wa haki na huduma mbalimbali” alisema Hudson.

Alisema nyaraka hizo zinamsaidia mwananchi kupata haki ya urithi, kupata ajira na huduma nyingine za matibabu na kwamba bila cheti hicho mtu hawezi kupata bima ya afya wala kugaiwa urithi kwani lazima utambuliwe kwa majina na vinasaba.

Alisema kwa mujibu wa takwimu ya sensa ya mwaka 2012 ni asilimia 13.4 tu ya wananchi wa Tanzania bara ndio walikuwa wamesajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa na hivyo kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi yenye viwango vya chini kabisa vya usajili Afrika.

Alisema katika tathmini iliyofanyika katika maeneo mbalimbali nchini, sababu zinazosababisha wananchi wengi kutosajiliwa na kupata vyeti kwa wakati ni pamoja na umbali toka makazi ya wananchi mpaka ofisi za wakuu wa wilaya, uelewa mdogo wa umuhimu wa cheti cha kuzaliwa, ada ya cheti na nyinginezo ambazo tayari zimeshafanyiwa kazi.

Kwa upande wake  Mwenyekiti Halmashauri ya Morogoro, Kibena Kingo, alisema mtoto anapozaliwa hospitali anapewa kadi ili imsaidie katika usajili, lakini muda unapokuwa mrefu akisubiri kupata pesa 10,000 au 20,000 ya usajili kadi inapotea na kumbukumbu muhimu za mtoto pia.

“Kubwa kabisa ambalo nimelipenda mbali na kupeleka huduma karibu na jamii ni kuondosha ada ya usajili, nayo pia ilikuwa kwa wananchi wengine ni shida mtu alikuwa anaona kutoa 20,000 au 10,000 kusajili anaona bora abaki na mtoto” alisema kibena. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,814FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles