24.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

MOROCCO: TATIZO LA SOKA LETU NI KUOKOTANA KWA VIONGOZI

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


TAMAA za kufika mbali  katika michuano ya kimataifa  inatazamwa kuwa chachu na msukumo wa wadau na wapenda soka ndani ya nchi kuona labda tatizo kushindwa kufika huko linatokana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au  klabu kutokuwa watu sahihi wa mchezo huo.

Si katika klabu wala timu ya Taifa, kila viongozi wanaoingia madarakani wanaonekana kulaumiwa kwa kushindwa kubadili upepo na kuonekana labda ndio sababu ya kuishia hatua za awali katika michuano ya kimataifa ambayo kwa muda timu za taifa zimekuwa zikishiriki.

Maslahi binafsi na kushindwa kuwa na uzalendo imeonekana kuwa ndio sababu ya soka la nchi hii kushindwa kuwa imara na kulegalega kadri siku zinavyojengea.

Kocha wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Hemed Morocco anasema kwamba, “Ubinafsi ndio uliotufikisha hapa, si visiwani Zanzibar wala Bara baadhi ya viongozi wa klabu ni wachumia tumbo hawana uzalendo wala mapenzi ya kile wanachokifanya.

“Viongozi hao wanarudisha nyuma maendeleo ya soka nchini kwani bado wanaokotana na kupeana nyadhifa mbalimbali ndani ya klabu, hivyo vyama vya soka vya mikoa na Shirikisho wanatakiwa kuangalia jambo hili kwa kina kwani lipo na ni hatari kwa maendeleo ya mchezo huu,”anasema Morocco.

Kocha huyo wa zamani wa klabu ya Mwadui FC ya Shinyanga ya Ligi Kuu Tanzania Bara, anaamini kwamba TFF, vyama vya Soka vya mikoa au Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) havipaswi kulaumiwa kwani matatizo makubwa katika mchezo huo nchini yapo zaidi kwenye klabu.

“Ukiangalia kwa juu utaanza kuulaumu uongozi wa TFF na mambo mengine mengi ila tatizo kuu lipo katika klabu kwani hawajui kuwa kupitia wawo tunaweza kuwa na vipaji lukuki na kuendeleza soka la nchi hii.

Morocco anasema changamoto nyingine ni wachezaji wenyewe kushindwa kujituma pamoja na kuwa na elimu ndogo ya soka.

“Mbali na kutopita shule za soka, tatizo lingine ni kukosa elimu ya kawaida ambayo ndio msingi wa mambo mengi uwanjani hivyo kufanya hata makocha wakigeni kupata ugumu wa kuwafundisha timu zetu hapa nchini.

“Wenzetu kutoka Uganda wachezaji wao wengi wanatoka katika vyuo vikuu, ndio maana tunaona wanafanya vizuri katika michuano mbalimbali,”anasema Morocco.

Akizungumza hamasa ya mchezo wa soka Zanzibar, Morocco alisema imeongezeka baada ya michuano ya CECAFA ambayo ilimalizika hivi karibuni kwa timu ya taifa ya visiwa hivyo kuwa nafasi ya pili.

“Hamasa imeongezekana pamoja na ushindani kwa kuwa kila mchezaji anacheza ili aitwe kwenye timu ya taifa hiyo inasaidia kupata wachezaji wazuri ingawa changamoto kubwa ipo kwa Ligi Kuu kukosa wafadhili,”anasema Morocco.

Kocha huyo ambaye yupo katika mipango ya kutafuta timu ya kufundisha nje ya Tanzania amesema kushindwa kuwa na ufadhili ndiko kumesababisha klabu za visiwani humo kushindwa kufanya usajili wa maana.

“Hakuna usajili wa maana, nani anataka kuja Zanzibar kucheza soka la kulipwa wakati hakuna wafadhili?”anahoji Morocco.

Morocco anaongeza kwamba klabu ndogo za chini zinahitaji msaada mkubwa ili ziweze kufika malengo ikiwamo kuinua vipaji.

“Wachezaji wengi wazuri wanatoka katika timu za chini, tena wanapatika mikoani, kwa mfano upande Bara mikoa ya Mwanza, Bukoba, Dar es Salaam na Morogoro kuna vipaji vingi sana huko ndiko wanapopatika wachezaji wazuri katika timu za hapa nchini,”anasema Morocco.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles