24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MOROCCO KUWEKEZA SEKTA YA UMEME, CHUMA NCHINI

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Cliford Tandari

Na LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

WAWEKEZAJI kutoka Morocco wameonyesha nia ya kuwekeza katika sekta ya umeme, uchimbaji na utengenezaji wa bidhaa za chuma na ujenzi kama hatua ya ushirikiano kati ya nchi hiyo na Tanzania.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Cliford Tandari, Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa kujadili namna ya kutumia fursa na rasilimali za Afrika kufikia uchumi wa kati.

Mkutano huo uliwahusisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania na Morocco, sambamba na benki ya Afrika, mambo kadhaa yalijadiliwa.

“Tunaendelea kufanya majadiliano ili tuyalete mambo haya mezani na kuwakutanisha wa wafanyabiashara wa hapa nyumbani watakaoweza kushirikiana kutumia fursa hizi kufanya biashara ambazo zitapunguza tatizo la ajira” alisema Tandari.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk.Khalid Salum Mohammed, alisema ushirikiano wa biashara baina ya nchi za Afrika  utapanua wigo wa masoko na kuharakisha maendeleo ya bara hilo.

Alisisitiza juu wa umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi za Afrika katika kukuza uchumi kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

“Kwa sasa uchumi wetu ni kati ya bara hili (Afrika) na nje ya Afrika, sasa ni vema kuhakikisha tunaimarisha ushirikiano kati yetu.

“Katika mkutano wa kukuza uchumi kule Arusha uliohudhuriwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, walikubaliana kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Afrika, nashukuru Serikali imeanza kutekeleza yale yaliyoafikiwa kuhusu ukuaji wa bara letu” alisema Waziri Mohammed.

Aliongeza kuwa katika majadilano hayo wametumia fursa hiyo kuwashawishi Morocco kuwekeza katika sekta ya uvuvi hususan wa kina kirefu cha bahari ili kuongeza tija na kuboresha miundombinu katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Morocco nchini, Ahdelilah Benryane, alisema nchi yake imelenga kuongeza uwekezaji katika Bara la Afrika na kutekeleza maazimio ya kuongeza uwekezaji kama ilivyoafikiwa na Umoja wa Afrika (AU).

Aliongeza kuwa nchi hiyo inaangalia uwezekano wa kuanzisha ushirikiano baina ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Morocco kuwezesha kuwapo kwa safari za ndege kutoka Dar es Salaam na Zanzibar kwenda nchini humo.

“Miaka ya 1960 tulikuwa tukipigania mapinduzi wa Morocco, sasa huu ni muda wa kuhakikisha tunafanya mapinduzi ya biashara barani kwetu” alisema Benryane.

Naibu Mkurugenzi wa Benki ya Afrika (BOA), Wasia Mushi, alisisitiza kuhusu umuhimu wa ushirikiano katika kukuza uchumi na kubadilishana utaalamu kati ya Serikali na sekta binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles